Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi Yemen yaendelea kuwa ‘mwiba’ kwa raia

Picha: EPA-EFE/Yahya Arhab
Wayemeni wanakagua kijengo liloporomoshwa na mlipuko wa kombora.

Mashambulizi Yemen yaendelea kuwa ‘mwiba’ kwa raia

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umesema idadi ya raia waliofariki dunia kwenye mashambulizi huko Yemen kwa mwezi uliopita wa Aprili ni kubwa kuwahi kushuhudiwa mwaka huu wa 2018.

Idadi hiyo ilikuwa 236 ikilinganishwa na vifo 180 mwezi uliotangulia wa Machi.

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema ina wasiwasi mkubwa kutokana na kuendelea kuongezeka kwa wahanga wa kiraia kwenye mapigano yanayoendelea nchini Yemen.

Mathalani mashambulizi ya hivi karibuni kwenye maeneo yenye raia wengi ikiwemo shambulio la anga lililofanywa jumatatu kwenye ofisi ya rais mjini Sana’a.

Ofisi hiyo imenukuu watu walioshuhudia tukio  hilo wakisema jengo hilo lilishambuliwa tena dakika 7 baada ya shambulio la kwanza na kusababisha majeruhi wengi miongoni mwa wahudumu waliokimbilia eneo hilo kutoa huduma ya kwanza.

Ravina Shamdasani ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi.

(Sauti ya Ravina Shamdasani)

“Tuna wasiwasi mkubwa juu ya ongezeko hili kubwa la raia wanaoathiriwa na mashambulio haya. Tunatoa wito tena kwa pande husika kwenye mzozo kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu.”

Yemen imekuwa kaika mzozo tangu mwaka 2015 ambapo muungano unaoongozwa na Saudia umekuwa ukipambana na kundi la Houthi katika kupata udhibiti wa taifa hilo.