Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres alaani shambulio Iran lililoua zaidi ya watu 100

Mji wa Kerman ulioko kusini-mashariki mwa Iran
© Unsplash/Mahdi Karbakhsh Ravari
Mji wa Kerman ulioko kusini-mashariki mwa Iran

Guterres alaani shambulio Iran lililoua zaidi ya watu 100

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulio lililofanyika hii leo huko nchini Iran na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 100, huku mamlaka za Iran zikiripoti kuwa zaidi ya watu 170 wamejeruhiwa.

Shambulio hilo kwenye mji wa Kerman limetokea wakati wa kumbukizi ya miake minne tangu kuuawa mwaka 2020  kwa Qassim Suleimani aliyekuwa afisa wa ngazi ya juu kabisa kwenye jeshi la nchi hiyo.

Suleimani  aliuawa kwa shambulio kutoka ndege isiyo na rubani kwenye mji mkuu wa Iraq, Bagdad miaka minne iliyopita.

Wahusika wa shambulio wawajibishwe

Taarifa iliyotolewa leo na Florencia Soto Nino wa Ofisi ya Msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnukuu Katibu Mkuu akitaka wahusika wa shambulio hilo lililosababisha pia majeruhi kadhaa wawajibishwe.

Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopotezwa wapendwa wao na serikali ya Iran huku akiwatakia ahueni ya haraka waliojeruhiwa.

Ripoti zadadavua kilichotokea

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa mabomu mawili yalilipuka karibu na kaburi la Suleimani karibu na msikiti wa Saheb al-Zaman mjini Kerman.

Ripoti hizo zinadokeza kuwa mabomu yaliyokuwa yametegwa kando mwa barabara yaliteguliwa kutokea mbali, hivyo kusababisha vifo vingi na mkanganyiko, kwa kile ambacho mamlaka za Iran zimeita kuwa ni shambulio la kigaidi.

Ripoti hizo zinasema kulingana na ukubwa na kiwango cha milipuko hiyo idadi ya watu waliokufa inaweza kuongezeka na hadi sasa hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na shambulio hilo.