Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio nchini Iran, Katibu Mkuu UN alaani vikali, atuma salamu za rambirambi

Barabara Kuu ya Hakim, kwenye mji mkuu wa Iran, Tehran
Unsplash/Mehrshad Rajabi
Barabara Kuu ya Hakim, kwenye mji mkuu wa Iran, Tehran

Shambulio nchini Iran, Katibu Mkuu UN alaani vikali, atuma salamu za rambirambi

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulio la kigaidi kwenye kaburi takatifu la Shah Cheragh huko Shiraz nchini Iran.

Shambulio hilo lilitokea jana Jumatano ambavyo vyombo vya habari vinaripoti kuwa watu 15 waliuawa kwenye shambulio hilo na makumi kadhaa wamejeruhiwa.

 

Taarifa za awali zinasema washambuliaji watatu walifyatulia risasi mahujaji na watumishi katika lango la kaburi hilo ambalo ni eneo takatifu la waumini wa madhehebu ya Shia.

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa jijini New  York, Marekani, kikundi cha Islamic State kimedai kuhusika na shambulio hilo.

 

Katibu Mkuu amesema vitendo vya aina hii vya kulenga maeneo ya kidini na kuabudu ni vya kikatili.

“Nasisitiza wahusika wa ukatili huu dhidi ya raia wanaotekeleza haki yao ya kuabudu wafikishwe mbele ya sheria,” amesema Guterres.

 

Ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao pamoja na serikali ya Iran huku akitakia ahueni ya haraka majeruhi.