Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Iran na IAEA wapitisha mambo matatu kuhusu nyuklia

Mkurugenzi Mkuu wa IEAE Rafael Mariano Grossi akizungumza na waandishi wa habari
IAEA/Dean Calma
Mkurugenzi Mkuu wa IEAE Rafael Mariano Grossi akizungumza na waandishi wa habari

Iran na IAEA wapitisha mambo matatu kuhusu nyuklia

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki, IAEA na shirika la nishati ya atomiki nchini IRAN, AEOI yamekubaliana mambo makuu matatu kwa lengo la kuimarisha usalama wa nyuklia nchini humo.

Makubaliano hayo yamefikiwa hii leo mwishoni mwa ziara ya Mkurugenzi Mkuu wa IAEA nchini humo Rafael Mariano Grossi.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa leo mjini Tehran nchini Iran na Mkuu wa IAEA Bwana Grossi na Mkuu wa AEOI Mohammad Eslami imetaja mambo hayo kuwa ni mosi, mazungumzo kati ya IAEA na Iran yatafanyika kwa njia ya ushirikiano na kwa kuzingatia uwezo wa IAEA na haki na wajibu wa Iran kwa kwa mujibu wa makubaliano ya kina ya usalama wa nyuklia.

Pili, ni kuhusu masuala yaliyosalia kuhusu usalama wa nyuklia yakihusisha maeneo matatu ambapo Iran imeeleza utayari wake wa kuendeleza ushirikiano na kutoa taarifa zaidi na ruhusa ya kufika maeneo hayo ili kutatua masuala yaliyobakia.

Jambo la tatu ni kwamba Iran kwa hiari itaruhusu IAEA itekeleze hatua sahihi ya shughuli za uthibitishaji na ufuatiliaji. Mifumo ya utekelezaji itakubaliwa kati ya pande mbili hizo kufuatia mkutano wa kitaalamu utakaofanyika punde mjini Tehran.

Grossi alikutana pia na Rais wa Iran

Taarifa hiyo ya pamoja imetolewa baada ya mikutano ya ngazi ya juu aliyofanya Bwana Grossi na viongozi waandamizi wa Iran akiwemo Rais Ebrahim Raisi na Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian.

Mikutano hiyo ya ngazi ya juu ilijadili umuhimu wa kuchukua hatua ili kufanikisha ushirikiano na kuharakisha suluhisho sahihi la masuala yaliyosalia kuhusu usalama kwenye mitambo ya nyuklia.

Pande zote mbili, yaani Iran na IAEA zinatambua kuwa mazungumzo ya aina hiyo yatafanikisha makubaliano kati yao.