Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu wa UN wapinga utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa kutumia gesi ya nitrojeni hypoxia

Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulika na masuala ya mateso, na Adhabu nyingine za Kikatili, za Kinyume cha utu au za Kushusha hadhi, Alice Jill Edwards.
UN Video
Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulika na masuala ya mateso, na Adhabu nyingine za Kikatili, za Kinyume cha utu au za Kushusha hadhi, Alice Jill Edwards.

Wataalamu wa UN wapinga utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa kutumia gesi ya nitrojeni hypoxia

Haki za binadamu

Wataalamu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa akiwemo Alice Jill Edwards, anayeshughulikia masuala yanayohusu mateso, na Adhabu nyingine za Kikatili, za Kinyama au ya Kushusha, hadhi leo Januari 3 mjini Geneva-Uswisi wameelezea wasiwasi wao kuhusu kukaribia kutekelezwa kwa hukumu ya kifo kwa kutumia gesi ya nitrojeni hypoxia dhidi ya Kenneth Eugene Smith hapa nchini Marekani.  

Wataalamu hao wanaamini kuwa njia hii ya utekekezaji wa hukumu ya kifo ambayo haijawahi kufanyiwa majaribio ya utekelezaji inaweza kumfanya anayeuawa atendewe ukatili, unyama au udhalilishaji au hata kuteswa na kwamba hakuna ushahidi wa kisayansi wa kuthibitisha vinginevyo. 

Smith alipatikana na hatia ya kuua kwa kukodiwa mwaka wa 1988 na kuhukumiwa kifungo cha maisha bila msamaha kwa kura 11 za kukubali  na 1 ya kupinga. Hata hivyo, hakimu aliyetoa hukumu alipuuza pendekezo la kifungo cha maisha na akamhukumu kifo. 

Kenneth Smith, ambaye amekuwa akisubiri kunyongwa kwa zaidi ya miaka thelathini, amepangwa kunyongwa Januari hii tarehe 25, 2024, katika Jimbo la Alabama hapa Marekani. Mamlaka huko Alabama hapo awali zilijaribu kumuua Smith mnamo Novemba mwaka juzi 2022 kwa kutumia sindano ya sumu, lakini jaribio hilo lilishindikana. 

Itifaki ya 'Utekelezaji wa hukumu ya kifo' iliyoidhinishwa hivi karibuni ya Jimbo la Alabama, inaruhusu matumizi ya gesi ya nitrojeni. "Tuna wasiwasi kwamba nitrojeni hypoxia inaweza kusababisha kifo cha uchungu na cha kufedhehesha," wataalam wamesema na kuonya kuwa utekelezaji wa majaribio kwa mtu kuvuta gesi - kama vile nitrojeni haipoksia - huenda utakiuka marufuku ya mateso na adhabu nyingine za kikatili, za kinyama au za kudhalilisha. 

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wameeleza masikitiko yao kuhusu kuendelea kwa hukumu ya kifo nchini Marekani, ambayo inakinzana na mwelekeo wa kimataifa wa kukomesha hukumu ya kifo. Unyongaji ulioshindikana, ukosefu wa uwazi wa itifaki za kunyongwa na utumiaji wa dawa ambazo hazijajaribiwa kuwanyonga wafungwa nchini Marekani zimeendelea kuvutia tahadhari za mifumo ya Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na taratibu maalum. 

Wataalamu hao wamebainisha kuwa adhabu zinazosababisha maumivu makali au mateso, zaidi ya madhara yanayotambuliwa kisheria huenda zinakiuka Mkataba dhidi ya Mateso ambayo Marekani inashiriki, na Baraza la Kanuni za Ulinzi wa Watu Wote Chini ya Aina Yoyote ya Kizuizini au Kifungo kinachohakikisha kwamba hakuna mfungwa atakayefanyiwa majaribio ya kitabibu au kisayansi jambo ambalo linaweza kudhuru afya yake. 

Walikata rufaa kwa mamlaka ya Shirikisho na Jimbo nchini Marekani na Jimbo la Alabama kusitisha utekelezaji wa Kenneth Smith na wengine wowote walioratibiwa kutekelezwa kwa njia hii, ikisubiri kuhakikiwa kwa itifaki ya utekelezaji.