Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

GAZA: Mashambulizi yakishamiri, njaa na magonjwa navyo vyatawala

Mtoto mwenye umri wa miaka minane akisubiri mgao wa chakula huko Rafah, kusini mwa Gaza
© UNICEF/Abed Zagout
Mtoto mwenye umri wa miaka minane akisubiri mgao wa chakula huko Rafah, kusini mwa Gaza

GAZA: Mashambulizi yakishamiri, njaa na magonjwa navyo vyatawala

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya usaidizi wa kiutu hii leo Jumanne yameendelea kuelezea wasiwasi wao mkubwa juu ya hatma ya raia walionasa kwenye mapigano huko Ukanda wa Gaza wakati huu kukiwa na ripoti ya kwamba jeshi la Israel limeendelea na mashambulizi kwenye miji ya kusin mwa Gaza ya Deir al Balah, Khan Younis na Rafah huku vikundi vya kipalestina vilivyojihami vikirusha makombora usiku kucha kuelekea Israel.

Maonyo ya hivi karibuni zaidi yametoka kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA na lile la mpango wa chakula, WFP, ambapo kwa pamoja wameangazia tishio la njaa na magonjwa kwenye maeneo yaliyofurika watu, ambako makumi ya maelfu ya watu wamejihifadhi kukwepa mashambulizi ya mabomu kwenye eneo la kati na kaskazini mwa Gaza.

Mlo kwa tabu

“Kila mtu Gaza ana njaa! Kula mlo mmoja kwa siku ni kawaida na kila siku mtu anahaha kujikimu,” WFP imesema kupitia chapisho lake kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X zamani Twitter. “Watu mara nyingi wanashinda njaa au wanalala njaa. Watu wazima hawali chakula ili watoto wao waweze kula.”

Zaidi ya watu milioni moja sasa wanasaka usalama kwenye mji wa kusini wa Rafah ambao tayari umejaa watu wengi, imesema UNRWA na kuongeza kuwa mamia ya maelfu wanalala maeneo ya wazi bila kuwa na nguo za kutosha za kujikinga na baridi.

Watoto wasio na mlo wa kutosha wako hatarini zaidi wakati huu ambapo “nusu ya wakazi wa Gaza wanahaha njaa,” watoa misaada kutoka Umoja wa Mataifa wameonya wakinukuu tathmini ya ukosefu wa uhakika wa kupata chakula.

Magonjwa ya maambukizi yanasambaa

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO nalo linapazia athari mbaya za mzozo unaoendelea likisema kuna hatari kubwa ya magonjwa ya milipuko kusambaa.

Tangu Oktoba 7, 2023 mapigano yalipoanza, kumekuweko na wagonjwa 179,000 wa magonjwa ya njia ya hewa, wagonjwa 136,000 wa kuhara miongoni mwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, na wagonjwa 55,400 wa vidonda na chawa.

Tangu shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023, lililosababisha vifo vya watu 1,200 na wengine 240 watekwe nyara, mapigano kwenye ukanda wa Gaza, na mashambulizi kutoka angan ina ardhini  na vile vile baharini yanayofanywa na jeshi la Israel (IDF) yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 22,000 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, kwa mujibu wa maafisa wa afya wa Palestina.

Takwimu za IDF zilizotolewa Desemba 30, 2023 zinadokeza kuwa askari 168 wa Israel wameuawa tangu kuanza kwa operesheni za kijeshi za ardhini huko Gaza na wengine 955 wamejeruhiwa.

Wizara ya afya Gaza nayo inaripoti kuwa zaidi ya wapalestina 200 wameripotiwa kuuawa tangu jana jumatatu pekee hadi leo, huku wengine 338 wamejeruhiwa.

Maelfu wahofiwa kufa

Wakati huo huo, WHO katika taarifa yake mpya inasema watu wengine 7,000 kwa sasa hawajulkani waliko au wamefukiwa kwenye vifusi.

Ripoti hiyo pia inasema watu 600 wameuawa kufuatia mashambulizi 300 kwenye hospitali tangu Oktoba 7, mashambulizi ambayo yameharibu hospitali 26 na magari ya wagonjwa 38.

Kati ya watu milioni 1.93 waliofurushwa makwao Gaza, 52,000 ni wajawazito ambao wanajifungua watoto 180 kila siku, kwa mujibu wa WHO. Imeelezwa pia wagonjwa 1,100 wanahitaji huduma ya kusafisha figo kila siku, 71,000 ni wagonjwa wa kisukari na 225,000 wanahitaji tiba dhidi ya shinikizo la damu.

Huduma za afya zinarejeshwa

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA nayo imesema kuwa mamlaka za afya Gaza nazo zimeweza kurejesha huduma katika baadhi ya hospitali kaskazini mwa Gaza.

Hospitali hizo ni pamoja na ile ya Ahli Arab, Patients Friends Charity, Al Helou, Al Awda na vituo vingine vya afya.

“Hii imefanyika kukiwa na hatari kubwa ya mazingira tunamofanyia kazi kwani mashambulizi yanaendelea kwenye viunga vya makazi ya watu na vituo vya afya,” imesema OCHA.

Zaidi yah apo, Wizara ya Afya huko Gaza, UNRWA na WHO wanaratibu mpango wa kufufua upya huduma za afya ili kukidhi mahitaji ya wakimbizi wa ndani.

Janga Ukingo wa Magharibi

Wakati huo huo, OCHA imeripoti tukio la kwanza la kuvunjwa kwa makazi ya wapalestina kwenye Ukingo wa Magharibi huko al-Maniya mjini Bethlehem, tukio ambalo ni la kwanza kwa mwaka huu wa 2024.

Baadhi ya wapalestina 300, wakiwemo watoto 79 wameuawa kwenye Ukingo wa Magharibi tangu Oktoba 7, wakati huu mashambulizi kutoka jeshi la Israel pamoja na walowezi wa kiyahudi yakiendelea, mashambulizi ambayo yamelaaniwa na Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataia kuhusu haki za binadamu, Volker Türk.

Kabla ya shambulizi lililofanywa na Hamas Oktoba 7, wapalestina 200 tayari walikuwa wameuawa kwenye Ukingo wa Magharibi mwaka jana wa 2023, ikiwa ni idadi kubwa katika kipindi cha miezi 10 tangu Umoja wa Mataifa uanze kuweka kumbukumbu mwaka 2005.