Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

GAZA: Mashambulizi yakiendelea, huduma za afya taaban, ‘ni dimbwi la damu’

Mvulana mwenye umri wa miaka 3, ambaye nyumba yake ilishambuliwa kwa bomu, anapata nafuu katika hospitali ya Nasser baada ya kukatwa sehemu ya mguu wake wa kulia.
© UNICEF/Abed Zaqout
Mvulana mwenye umri wa miaka 3, ambaye nyumba yake ilishambuliwa kwa bomu, anapata nafuu katika hospitali ya Nasser baada ya kukatwa sehemu ya mguu wake wa kulia.

GAZA: Mashambulizi yakiendelea, huduma za afya taaban, ‘ni dimbwi la damu’

Amani na Usalama

Wahudumu wa afya huko Ukanda wa Gaza leo jumanne wameendelea na kazi ya kuokoa maisha ya manusura wa mashambulio ya makambora yakiwemo mashambulio karibu na kambi ya wakimbizi kwenye eneo hilo lililozingirwa na Israel, mashambulio ambayo yameripotiwa kuua zaidi ya wtu 100, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la afya, WHO.

Mratibu wa Timu ya Matabibu wa Dharura Sean Casey amesema wagonjwa zaidi ya 100 walifikishwa Jumatatu kwenye hospitali ya Al-Aqsa ndani ya muda wa dakika 30, kufuatia milipuko karibu na kambi ya wakimbizi ya Al-Maghazi.

Wagonjwa wote hao walikuwa wanahitaji matibabu ya dharura wakiwa na majeraha makubwa,  amesema Afisa huyo wa WHO akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Amesema huku wagonjwa hao wakiletwa hospitali, takribani maiti wengine 100 walifikishwa muda huo huo.

Wamenasa chini  ya vifusi

Nayo Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, OHCHR, imeelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya mashambulizi makubwa ya mabomu yanayoendelea kufanywa na jeshi la Israel katikati ya Gaza, ambapo zaidi ya mashambulizi 50 kutoka angani yameripotiwa kufanyika tangu tarehe 24 mwezi huu wa Desemba.

Mashambulio hayo yameripotiwa kuua zaidi ya wapalestina 100 tangu siku hiyo ambapo OHCHR inasema, “hii inatia zaidi wasiwasi kwa ripoti ya kwamba jeshi la Israel limeagiza wakazi walioko kusini mwa eneo la Wadi Gaza, wahamie eneo la kati la Gaza na Tal a-Sultan.” 

Kambi tatu za wakimbizi zilipigwa kwa makombora, amesema msemaji wa OHCHR, Seif Magango kwenye taarifa iliyotolewa leo, akitaja kambi hizo kuwa ni Al Bureij, Al-Nuseirat na Al-Maghazi. 

“Makombora mawili yalipiga makazi sav ana kuua tarkibani wapalestina 86 na kujeruhi wengine wengi,” amesema Magango huku akiongeza kuwa, “idadi isiyojulikana ya watu yaaminika wamefukiwa kwenye vifusi.”

Tedros achukizwa

Kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa X (zamani ukijulikana kama Twitter) Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amelaani mauaji yanayosababishwa na mashambulizi ya kutoka angani yanayofanywa na jeshi la Israel dhidi ya Gaza ikiwa ni kisasi cha mashambulizi yaliyofanywa na Hamas tarehe 7 mwezi Oktoba mwaka huu. Takribani watu 1,200 waliuawa na wengine 240 walitekwa nyara siku hiyo.

“WHO ina wasiwasi mkubwa juu ya mzigo mkubwa kwa hospitali chache zinazoendelea kutoa huduma kwenye eneo hilo kutokana na kuendelezwa kwa chuki kati ya pande mbili hizo. Hospitali zilizosalia wazi ni chache ambapo nyingi zao uwezo wa kutoa huduma uko taabani,” alisema Dkt. Tedros siku ya Jumatatu.

Kupitia ukurasa wake wa X, Bwana Casey ameelezea hali katika hospitali ya Al-Aqsa kuwa ni dimbwi la damu. Alionesha Ahmed, mvulana mwenye umri wa miaka tisa ambaye alikuwa amalala kwenye sakafu ya hospitali hiyo baada ya kujeruhiwa kwa kiasi kikubwa na mlipuko wakati akivuka mtaa mmoja karibu na Nuseirat.

“Tumeona watoto, wanawake, vijana wa kiume, wazee wakivuja damu,” amesema Bwana Casey, huku akiongeza kuwa wagonjwa hawawezi kuhamishiwa eneo lingine kwa ajili ya matibabu ya kuokoa maisha yao.

“Damu imetapakaa kila mahali kwenye hizi hospitali. Tunaona wagonjwa wako na viwewe, damu kila mahali, tulishasema, ni mauaji.”

Shule ya Nuseirat iliyoko Gaza Kati inayoendeshwa na UNRWA sasa ni makazi ya maelfu ya watu waliofurushwa makwao kutokana na mashambulizi yanayoendelea Gaza.
UN News/Ziad Taleb
Shule ya Nuseirat iliyoko Gaza Kati inayoendeshwa na UNRWA sasa ni makazi ya maelfu ya watu waliofurushwa makwao kutokana na mashambulizi yanayoendelea Gaza.

Mapigano usiku kucha

“Hakuna mahali salama Gaza,” amesema Bwana Casey. “Hivi sasa hapa Rafah nje ya mlango wa jengo hili niliko, meta 50 hivi, kuna kambi ya maelfu ya watu ambao wamesaka hifadhi hapa. …wanaishi kwenye makazi yaliyofunikwa kwa karatasi za nailoni. Jana usiku tulisikia mashambulizi usiku kucha huku kukiwa na ripoti za kuweko kwa majeruhi wengi, wakipelekwa hospitali zilizoko hapa kusini.”

Uwezo wa hospitali Gaza hivi sasa ni takribani asilimia 20 ya kabla ya tarehe 7 Oktoba mashambulizi yalipoanza. “Takribani hospitali zote zimeacha kufanya kazi.”

Wanasubiri kufa

Bwana Casey amezungumzia pia wagonjwa walioko mahututi huko Gaza Kaskazini ambao kwa sasa wanasubiria kufa tu kwani hospitali ya mwisho iliyokuwa inatoa huduma imefungwa na sasa wako kwenye viwanja vya kanisa wakilala kwenye viti.

“Kiwango cha uharibifu ni kikubwa, barabara zimesheheni vifusi hivyo ni vigumu kufikia wahitaji.”

“Bado tunahitaji kuchukua hatua zaidi kusafirisha hawa wagonjwa, lakini fursa ya kufanya hivyo inazidi kuwa fingu kila uchao kwani ufikiaji wa hospitali ni mgumu,” amesema Bwana Casey.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya Gaza, takribani watu 20,000 yaaminika wameuawa tangu kuanza kwa mapigano Oktoba 7, mwaka huu.