Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Maisha yarejea hali ya kawaida huko Fataki, Ituri baada ya mashambulizi kutoka CODECO

Bukavu, Kivu Kusini. Uchaguzi wa Rais na wabunge umefanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, 20 Desemba 2023.
MONUSCO/Michael Ali
Bukavu, Kivu Kusini. Uchaguzi wa Rais na wabunge umefanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, 20 Desemba 2023.

DRC: Maisha yarejea hali ya kawaida huko Fataki, Ituri baada ya mashambulizi kutoka CODECO

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kazi ya kuhesabu kura inaendelea baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Jumatano na kuendelea katika baadhi ya maeneo jana Alhamisi, huku ikielezwa kwamba jimboni Ituri, maisha  yamerejea katika hali ya kawaida kwenye eneo la Fataki baada ya mwaka mmoja wa mashambulizi kutoka kwa wanamgambo waliojihami wa kundi la CODECO. 

Radio Okapi ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MOMUSCO imegusia zaidi kituo cha biashara cha FATAKI kilichoko mji mkuu wa Ituri, Bunia ambako CODECO kwa mwaka mzima walikuwa wakishambulia mara kwa mara. 

Mathalani mwezi Mei mwaka huu, CODECO walishambulia eneo la Djugu na kuua raia 38, hali iliyosababisha wakazi wengine kukimbilia eneo la Djahiba lililoko kilometa 5 kutoka kituo cha MONUSCO

Sababu ya maisha kurejea kwenye hali ya kawaida ni doria za magari na za miguu zinazofanywa na askari wa jeshi la serikali, FARDC na walinda amani wa MONUSCO kwenye eneo hilo. 

Usalama umeimarika, wakazi wanaendelea na biashara sambamba na ukulima mashambani. 

Wakati huo huo, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi nchini DRC, CENI imesema kazi ya kupiga kura kwenye maeneo yaliyoshindwa kufanya hivyo imekamilika jana Alhamisi na kwamba hakuna eneo lolote lile lililopiga kura leo Ijumaa. 

Matokeo rasmi ya uchaguzi wa Rais yanatarajiwa kutangazwa tarehe 31 mwezi huu na kisha Rais mteule ataapishwa tarehe 24 Januari mwaka 2024.