Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makaburi mawili yenye jumla ya miili 49 yabainika jimboni Ituri, DRC

Watoto wakimbizi wa ndani katika kambi moja iliyoko mjini Djugu jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC
UN /Eskinder Debebe
Watoto wakimbizi wa ndani katika kambi moja iliyoko mjini Djugu jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC

Makaburi mawili yenye jumla ya miili 49 yabainika jimboni Ituri, DRC

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO  umebaini makaburi mawili ya halaiki katika mji wa Bunia jimboni Ituri.

Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq amewaambia waandishi wa habari jijini New York, Marekani kuwa kaburi moja katika kijiji cha Nyamamba lilikuwa limezikwa miili 42 ya raia wakiwemo wanawake 12 na watoto 6.

Na katika kaburi linigne likiwa na miili 7 ya wanaume liligundulika katika kijiji cha Mbogi.

“Vijiji vyote hivyo viwili viko takribani kilometa 30 mashariki mwa mji wa Bunia,amesema Bwana Haq.

Amenukuu MONUSCO ikisema kuwa walinda amani walikuwa kwenye doria baada ya kupata ripoti ya kwamba wapiganaji wa kikundi cha CODECO walishambulia maeneo hayo mwishoni mwa wiki na ndipo walipobaini makaburi hayo.

Makaburi yalibainika wakati MONUSCO wakiwa kwenye doria

Tayari MONUSCO inasaidia mamlaka za Mahakama nchini DRC kuchunguza mashambulio hayo huku ikitoa wito kwa wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

Kubainika kwa makaburi hayo kunakuja wakati hali ya usalama imezorota kwa kiasi kikubwa katika miji ya Djugu na Mahagi jimboni Ituri.

Tangu mwezi Desemba mwaka jana wa 2022, MONUSCO imeripoti kuwa takribani raia 195 wameuawa na wengine 68 wamejeruhiwa huku 84 wakitekwa nyara katika matukio kadhaa yanayodaiwa kufanywa na makundi yaliyojihami ya CODECO na Zaire.

Mashambulizi haya ya karibuni Zaidi yameongeza idadi ya wakimbizi wa ndani hadi kuwa zaidi ya milioni 1.5 jimboni Ituri na wakati huo huo kukwamisha ufikishaji misaada ya kibinadamu kwa wale wanaohitaji.