Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waasi wa CODECO waua raia Ituri, Bintou kuhusu Baraza

Walinda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO wako chonjo kuhakikisha kuna usalama na hapa ni Djugu jimboni Ituru ambako walifika kuweka doria baada ya ripoti za kuweko kwa kikundi cha CODECO ambacho hushambulia raia.
MONUSCO/Force
Walinda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO wako chonjo kuhakikisha kuna usalama na hapa ni Djugu jimboni Ituru ambako walifika kuweka doria baada ya ripoti za kuweko kwa kikundi cha CODECO ambacho hushambulia raia.

Waasi wa CODECO waua raia Ituri, Bintou kuhusu Baraza

Amani na Usalama

Mashambulizi yanayofanywa na waasi wa kundi la CODECO jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC yameendelea ambapo katika tukio la hivi karibuni waasi hao walishambulia eneo la Djugu jimboni humo na kuua raia 17. 

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari jijini New York, Marekani hii leo kuwa waasi hao waliua watu hao katika mashambulio mawili tofauti. 

“Waasi hao pia walifyatulia risasi walinda amani wa Umoja wa Mataifa walio kwenye ujumbe wa kulinda amnai MONUSCO, pamoja na askari wa jeshi la serikali ya DRC, FARDC ambao walikuwa wanaendesha doria ya pamoja kwenye eneo hilo la Djugu,” amesema Dujarric. 

Hata hivyo amesema wakati wa tukio hilo, walinda amani na wanajeshi wa FARDC walijibu mashambulizi yaliyowezesha kufurumusha waasi hao waliokuwa wamejihami. 

Wakati huo huo katika eneo la Drodro na Roe, kusini-mashariki mwa jimbo la Ituri, walinda amani wa MONUSCO wameendelea kuchukua hatua za kuimarisha ulinzi kutokana na ukosefu wa usalama unaosababishwa na waasi wa CODECO. 

“Wenzetu wamefanikisha usafiri wa raia 28 wengi wao wanawake kutoka Drodro kwenda Roe ambako ni makazi ya wakimbizi wa ndani,” amefafanua msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa. 

Kwa sasa MONUSCO inawapatia hifadhi ya muda raia kwenye kituo chake kilicho Drodo kufuatia waasi hao wa CODECO kushambulia eneo karibu na kanisa. 

Taarifa hizi zinatolewa wakati kesho jijini New York, katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC na Mkuu wa MONUSCO, Bintou Keita atahutubia Baraza hilo kuhusu hali ya usalama nchini humo.