Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MAKALA: Jamii yasimama kidete Malawi kulinda mtoto wa kike dhidi ya mila potofu

UNFPA imepatia mafunzo kuhusu usawa wa kijinsia na haki wanachama wa Mtandao wa Mlirima huko Chikwawa nchini Malawi.
UNFPA MALAWI
UNFPA imepatia mafunzo kuhusu usawa wa kijinsia na haki wanachama wa Mtandao wa Mlirima huko Chikwawa nchini Malawi.

MAKALA: Jamii yasimama kidete Malawi kulinda mtoto wa kike dhidi ya mila potofu

Wanawake

Fanny Galeta, msichana mwenye umri wa miaka 16, hakuwa na uhakika jinsi ya kuitikia alipogundua sherehe yake ya kupelekwa unyagoni ilikuwa imeshapangwa. "Hakuna mtu anaweza kukuaambia ukweli kuhusu kile kinachotokea huko,"

Msichana huyu ameliambia shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uazi, UNFPA huko Malawi akisema kuwa, “mambo mengi yanafichwa. Nilijaribu kuwafikia marafiki zangu waliokuwa hapo, nao walicheka tu. Waliniambia itabidi nijitafutie mwenyewe.”

Katika makala iliyochapishwa kwenye wavuti wa UNFPA, inaelezwa kuwa, hatua hiyo haikuwa chaguo lake. 

Kambini kuna wazee wanawake wakifundisha watoto elimuy ya ngono

Punde, Fanny aliandamana na mama yake hadi kwenye kambi ndani kabisa ya msitu karibu na kijiji chao huko Chikwawa, ambako alilakiwa na wanawake wazee wanne. Hakuondoka kambini kwa majuma matatu yaliyofuata.

“Sheria zilikuwa ngumu; hatukupaswa kwenda nje au kuona mtu yeyote wakati wa kukaa kwetu. Hata wale waliotuletea chakula hawakuruhusiwa kuzungumza nasi,” anasema Fanny.

Alibaini kuwa baadhi ya vipengele vya sherehe vilikuwa vya manufaa, kama vile masomo ya usafi wakati wa hedhi na upishi. Lakini mengine, kama kipengele cha 'elimu ya ngono', ambapo mmoja wa wanawake wazee aliwafundisha wasichana jinsi ya kufanya ngono, karibu iliharibu maisha yake ya baadaye.

“Baada ya kuhitimu, tuliambiwa kwamba tulikuwa tumebalehe. Kwa wengi wetu, hilo lilimaanisha kwamba tulikuwa tayari kwa ndoa. Niliamua kujaribu yale tuliyojifunza na nikajikuta katika uhusiano wa kimapenzi,” anafafanua Fanny.

Mafunzo  ya unyago yamtumbukiza Fanny kwenye mapenzi

Mpenzi wa Fanny alikuwa amemzidi umri kwa miaka michache zaidi, na mapenzi yalivyozidi, Fanny alianza kupoteza hamu ya shule.

“Nilikubaliana naye tufunge ndoa, lakini mama yangu aliposikia, alitafuta usaidizi kwa polisi jamii. Kwa kuwa nilikuwa na umri mdogo, niliamua kuondoka eneo hilo kwenda kuishi na bibi ili wasije wakamkamata mpenzi wangu.”

Habari ilikuwa tayari imeenea kuhusu uhusiano wake, hata hivyo, na punde ikafika masikioni mwa chifu wa eneo hilo, ambaye aliamua kuingilia kati.

Bila hatua kuchukuliwa na vingozi wa kijiji, Fanny Galeta asingalirudi shuleni kwa masomo baada ya sherehe yake ya unyago.
© UNFPA Malawi
Bila hatua kuchukuliwa na vingozi wa kijiji, Fanny Galeta asingalirudi shuleni kwa masomo baada ya sherehe yake ya unyago.

Jamii yaingilia kati, Fanny arejea shuleni

Bila uingiliaji kati wa viongozi wa jamii, Fanny huenda asingerejea shuleni baada ya mafunzo hayo. Viongozi wa mitaa wanajitokeza kukabiliana na changamoto hiyo.

 Mkuu wa kikundi kwenye kijiji chao, Fraiton Pintu anasema, “wilaya yetu inajulikana kwa mila mbaya na potofu ambazo zimeharibu mustakabali wa wasichana wengi. Tunahitaji kubadilisha hili. Ikiwa tutashindwa, tutaacha urithi ambao utachukiwa na vizazi vijavyo."

Zaidi ya asilimia 40 ya wasichana nchini Malawi wameolewa wakiwa bado watoto, licha ya  katiba mpya ya mwaka wa 2017, iliyoongeza umri wa kisheria wa mtoto kuwa ni hadi miaka 18, kukiuka haki zao za ngono na uzazi na mara nyingi kukatiza masomo yao. 

Bwana. Pintu ni mtetezi mwenye shauku  wa elimu kwa wasichana na Mwenyekiti wa Mtandao wa Mlirima Development unaofadhliwa na UNFPA. Mtandao wao unapiga vita ukatili wa kijinsia na ndoa za utotoni, ambapo aliandaa mkutano na  Fanny.

"Alitusikiliza na akakubali kurudi shuleni. Pia tulihakikisha kwamba mvulana huyo hayuko naye kwa kumwonya kwamba tungemripoti kwa polisi ikiwa angeendelea kumuona,” amesema Bwana Pintu.

Mafunzo ya UNFPA kwa jamii yamejengea uwezo kijiji

Viongozi kutoka mtandao huo walipewa mafunzo na UNFPA kuhusu usawa wa kijinsia na haki chini ya mpango wa Safeguard Young People, unaofadhiliwa na Uswisi. 

Mpango huu umejengwa katika kukuza uelewa wa mila potofu  kama vile ndoa za utotoni na unyanyasaji wa kijinsia na kuwawezesha waathirika kudai haki zao. Hadi sasa mtandao huo umesaidia zaidi ya wasichana 30 kuepuka ndoa za utotoni na kuwaunga mkono katika kurejea masomoni. Mmoja wa wasichana hao alikuwa Fanny, ambaye alifanya mitihani ya cheti chake cha shule ya msingi na kufaulu.

"Nimefurahi kwamba nilisikiliza ushauri wao, sasa mimi ni fahari ya familia yangu kwani mimi ndiye msichana pekee aliyesoma sekondari,” anafafanua Fanny.

 Ili kuwalinda wasichana, Mkuu wa Kikundi cha Kijiji , Bwana Pintu ameweka sheria ndogo inayozuia sherehe  unyago zinazofanyika wakati wa muhula wa shule.

Ili kulinda watoto wa ike, Mkuu wa Kikundi cha Kijiji, Fraiton Pintu (aliyesimama) ametunga sheria ndogo kusitisha sherehe za unyago wakati wa muhula wa shule.
© UNFPA Malawi
Ili kulinda watoto wa ike, Mkuu wa Kikundi cha Kijiji, Fraiton Pintu (aliyesimama) ametunga sheria ndogo kusitisha sherehe za unyago wakati wa muhula wa shule.

Unyago wafanyika lakini ukiengua mila zilizopitwa na wakati

Anasema, "nyakati zimebadilika, bado tulikuwa na wanawake wazee wanaofundisha wasichana wadogo mila zilizopitwa na wakati. Tulichagua wanawake vijana ambao walikuwa na maendeleo ili wasimamie sherehe unyago. Hatuwezi kuwaondoa kabisa kwani ni sehemu ya utamaduni wetu, lakini tunaweza kuwarekebisha kutoka ndani.”

UNFPA inaunga mkono wanawake na wasichana duniani kote kudai haki yao ya kujitawala na kusimamia miili yao, kampeni kama za Bwana Pintu ni hatua muhimu katika kuziba mapengo yaliyosalia kufikia usawa wa kijinsia na kuruhusu wanawake na wasichana kuishi bila unyanyasaji, alisema Dkt. Natalia Kanem Mkuu wa UNFPA katika siku ya kimataifa ya haki za binadamu.

Hanna Mkamwa, mwenye umri wa miaka 35, anajivunia kukabidhiwa jukumu hilo kama mwanzilishi mpya na anatarajia kutoa taarifa zitakazowatayarisha vyema wasichana hao kuchagua maisha yao ya baadaye.

“Nimekuwa nikifanya kazi na wasichana kwa muda kama mshiriki wa kikundi cha akina mama, na najua sana matatizo wanayopitia wanapokuwa wakubwa. Sasa kwa kuwa mimi ni mwanzilishi, nitatumia ujuzi wangu kuwatengeneza wasichana kuwa viongozi wa baadaye na si watoto wa kuolewa,” anasema Bi.Mkamwa.