Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jukwaa la kimataifa la wakimbizi lahitimishwa kwa ahadi ya dola bilioni 2.2 kuboresha maisha ya wakimbizi na jamii zinazowahifadhi: UNHCR

UNHCR inasambaza misaada kwa wakimbizi wanaorejea katika kituo cha usafiri huko Renk, Sudan Kusini.
© UNHCR/Andrew McConnell
UNHCR inasambaza misaada kwa wakimbizi wanaorejea katika kituo cha usafiri huko Renk, Sudan Kusini.

Jukwaa la kimataifa la wakimbizi lahitimishwa kwa ahadi ya dola bilioni 2.2 kuboresha maisha ya wakimbizi na jamii zinazowahifadhi: UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Jukwaa la kimataifa la wakimbizi GRF linalofanyika kila baada ya miaka minne ambalo ni mkusanyiko mkubwa zaidi duniani unaojadili masuala ya wakimbizi limekunja jamvi hii leo mjini Geneva Uswisi.

Jukwaa hilo la siku tatu lililoanza 13 hadi 15 Desemba ni la pili na limeileta pamoja jumuiya ya kimataifa kwa mshikamano na wakimbizi  na limefanikiwa kukusanya adhi zaidi ya 1,6000 na limehudhuriwa na zaidi ya washiriki 4,200 kutoka nchi 168, wakiwemo wakuu watano wa nchi au serikali, mawaziri, wakuu wa mashirika ya kimataifa ikiwa ni pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika maalumu, mashirika yanayoongozwa na wakimbizi, wawakilishi wa mashirika ya kiraia, na wakurugenzi wakuu wa makampuni na taasisi, miongoni mwa wengine na zaidi ya watu 10,000 walijiunga mtandaoni.

Kilichojiri Mkutanoni

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR ambalo ndio mwenyeji wa mkutano huo “washiriki wameshirikiana mifano ya utendaji mzuri na kutangaza michango na ahadi za kubadilisha maisha ya wakimbizi na jamii zinazowahifadhi, katika maeneo kama vile elimu, upatikanaji wa soko la ajira, ujenzi wa amani, mabadiliko ya tabianchi na makazi mapya.”

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Wakimbizi, Filippo Grandi amesema "Washiriki wameonyesha uongozi, dira na ubunifu katika kutafuta suluhu la matatizo magumu. Zaidi ya yote, wamejitolea kuendelea kufanya kazi pamoja ili kuboresha maisha ya mamilioni ya wakimbizi duniani kote."

Kongamano la Kimataifa la Wakimbizi linahitimisha kazi yake katika kituo cha Palexpo huko Geneva.
UN News
Kongamano la Kimataifa la Wakimbizi linahitimisha kazi yake katika kituo cha Palexpo huko Geneva.

Ahadi zilizotolewa 

Grandi amesema ahadi za kifedha za jumla ya zaidi ya dola bilioni 2.2 zmeitangazwa na serikali, sekta binafsi, mashirika ya hisani na wakfu, mashirika ya kidini na wengine, pamoja na ahadi muhimu za kuzingatia wakimbizi na jumuiya zinazowahifadhi katika sera, vyombo vya ufadhili na programu. 

Pia amesema mataifa yameahidi kuwapa makazi wakimbizi milioni 1 ifikapo mwaka wa 2030, huku serikali na taasisi zikizindua ahadi inayoungwa mkono na hazina mpya ya kimataifa ya ufadhili kusaidia wakimbizi wengine milioni 3 kupata nchi za tatu kupitia ufadhili wa jumuiya ya kimataifa.

Julwaa hilo GRF limekusanya zaidi ya ahadi 1,600, na kuchangia katika moja au zaidi ya ahadi za washikadau wengine 43 ahadi kabambe zinazoungwa mkono na miungano ya usaidizi. 

Maendeleo muhimu yameahidiwa katika “kukuza uchumi na jamii kupitia uwekezaji katika maeneo yanayohifadhi wakimbizi, usaidizi kwa wajasiriamali wakimbizi, kazi, mafunzo ya ujuzi, huduma za kisheria za pro bono, bidhaa za kifedha na muunganisho, pamoja na kuboreshwa kwa ufikiaji wa hatua za mabadiliko ya tabianchi kwa wakimbizi, waliofurishwa makwao na wasio na utaifa, watu hao na wenyeji wao. “

Na zaidi ya dola milioni 250 katika ufadhili wa ziada ziliahidiwa na sekta binafsi.

Miradi bunifu iliyoahidiwa

Kwa mujibu wa UNHCR miongoni mwa miradi bunifu ilikuwa ni ahadi ya wadau mbalimbali kuhusu ulinzi wa kidijitali kutoka kwa serikali, sekta ya binafsi, mashirika ya kiraia, Umoja wa Mataifa na watendaji wengine, ili kusaidia kuzuia athari mbaya za kauli za chuki, habari potofu na upotoshaji.”

Jukwaa hili ambalo hufanyika kila baada ya miaka minne, GRF limeundwa kusaidia utekelezaji wa vitendo wa malengo yaliyowekwa katika Mkataba wa Kimataifa wa Wakimbizi, mfumo wa ushirikishwaji wa uwajibikaji unaotabirika zaidi na sawa kati ya mataifa, ambao ilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Desemba 2018.