Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ahadi 7 za Kenya kwa wakimbizi

Mwanafunzi kutoka Sudan Kusini akiwa darasani katika shule moja nchini Kenya. (Maktaba)
© UNHCR/Charity Nzomo
Mwanafunzi kutoka Sudan Kusini akiwa darasani katika shule moja nchini Kenya. (Maktaba)

Ahadi 7 za Kenya kwa wakimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Jukwaa la pili la kimataifa la wakimbizi, GRF, linalowakutanisha takribani watu 4000 kutoka nchi 165 limeingia siku yake ya pili leo huko Geneva, Uswisi ambapo washiriki wanatoa ahadi zao kuhusu namna bora ya kushughulikia suala la wakimbizi.  

Katika tamko la Kenya lililochapishwa kwenye ukurasa rasmi wa mkutano huo, Kenya imeeleza namna ilivyotekeleza ahadi yake iliyotoa kwenye mkutano wa kwanza miaka minne iliyopita kwa kuwapa uraia Washona, Wamakonde na Wapemba.  

Katika mkutano huu wa mwaka 2023, Kenya imeahidi kufanya mambo saba 

Ahadi ya kwanza ni kuhusu SHIRIKA Plan; Mpango wa mageuzi wa Kenya ambao unabadilisha kambi za wakimbizi kuwa makazi jumuishi. Mbinu hii bunifu inalenga kuhakikisha ushirikishwaji wa kijamii na kiuchumi wa wakimbizi na jamii zinazowapokea. 

Ahadi ya pili ni hati za wakimbizi na upatikanaji wa huduma ili kuimarisha taratibu za usajili na upatikanaji wa huduma kwa wakimbizi.  

Ahadi ya tatu ya Kenya ni usawa wa afya - ahadi ya kutoa huduma bora za afya zinazolingana, endelevu na zinazoweza kupatikana kwa wakimbizi na jamii zinazowapokea. 

Ahadi ya nne ya Kenya ni ulinzi wa kijamii na kiuchumi kuwajumuisha wakimbizi katika mifumo yake ya ulinzi wa kijamii.  

Ahadi ya tano ni mipango jumuishi ya maendeleo inayojikita katika uimarishaji endelevu wa michakato ya utawala.   

Ahadi ya sita ya Kenya ni ahadi ya kutokomeza ukosefu wa utaifa. “Tunaelewa kuwa kila mtu anastahili kitambulisho cha kisheria na haki zinazoambatana nacho.” Inasema Kenya. 

Ahadi ya saba inahusisha utekelezaji wa Mkakati wa Elimu na Mafunzo kwa Wakimbizi na Jamii Wenyeji nchini Kenya. 

Ahadi hizi zinasisitiza kujitolea kwa Kenya kuunda mustakabali ambapo wakimbizi sio tu wanapata makazi bali pia wanastawi kama wanajamii wanaothaminiwa.