Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP28 yakunja jamvi kwa muafaka wa mataifa  kuanza kuondokana na mafuta kisukuku

Rais wa COP28, Sultan Al Jaber (katikati), Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa, Simon Stiell (wa nne kutoka kushoto) na washiriki wengine wakiwa jukwaani wakati wa Kufunga Mkataba wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28,…
COP28/Christopher Pike
Rais wa COP28, Sultan Al Jaber (katikati), Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa, Simon Stiell (wa nne kutoka kushoto) na washiriki wengine wakiwa jukwaani wakati wa Kufunga Mkataba wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, kwenye Expo City huko Dubai, Falme za Kiarabu.

COP28 yakunja jamvi kwa muafaka wa mataifa  kuanza kuondokana na mafuta kisukuku

Tabianchi na mazingira

Mataifa hii leo katika mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP28 uliokunja jamvi mjini Dubai Falme za nchi za Kiarabu wamepitisha makubaliano yanayotoa mwelekeo wa mpito wa kuondokana na mafuta kisukuku au fossil fuel  yakiwa ni ya kwanza kwa mkutano huo wa Umoja wa Mataifa lakini muafaka huo haukutimiza wito uliotakwa na wengi kwa muda mrefu wa "kukomesha matumizi ya mafuta kisukuku, makaa ya mawe na gesi.”

Akitoa kauli yake baada ya kupitishwa kwa hati ya matokeo ya mkutano huo , Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema kutajwa kwa mchangiaji mkuu wa mabadiliko ya tabianchi (mafuta kisukuku) kunakuja baada ya miaka mingi ambapo mjadala wa suala hili ulizuiwa.

Amesisitiza kuwa zama za nishati ya mafuta kisukuku lazima ziishe kwa haki na usawa.

Kwa wale waliopinga kuainisha wazi utokomezaji wa nishati ya mafuta kisukuku katika waraka wa COP28, amesema "kwamba utokomezaji wa mafuta kisukuku haiwezi kuepukika watake wasitake. Hebu tutumaini kwamba hautachelewa sana. "

Mkutano huu wa karibuni kabisa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi umekuwa ukifanyika huko Dubai, jiji kubwa zaidi katika Umoja wa Falme za Kiarabu, tangu tarehe 30 Novemba.

COP28 ilikuwa imepangwa kufungwa siku ya Jumanne, lakini mazungumzo makali yaliyojumuisha wito wa "kupunguza au kutokomeza nishati inayoongeza joto la sayari dunia kama mafuta kisukuku, gesi na makaa ya mawe yalilazimu majadiliano ya mkutano huo kuingia katika muda wa ziada.

Suala hili kubwa liliweka wanaharakati na nchi zilizo katika mazingira magumu ya hali ya hewa kwenye mvutano dhidi ya baadhi ya mataifa makubwa kwa muda wa wiki mbili zilizopita.

Wajumbe wakisherehekea makubaliano ya makubaliano katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa, COP28.
UNFCCC/Kiara Worth
Wajumbe wakisherehekea makubaliano ya makubaliano katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa, COP28.

Sayansi iko bayana

Katika taarifa yake, Bwana. Guterres amesema kupunguza kiwango cha joto duniani hadi nyuzijoto 1.5°C, mojawapo ya shabaha kuu zilizowekwa katika Mkataba wa Paris wa 2015, "Haitawezekana bila kutokomeza nishati ya mafuta kisukuku na hii inatambuliwa na muungano unaokua na wa nchi tofauti”.

Wajumbe katika COP28 pia wamekubaliana juu ya ahadi za uwezo wa kuongeza upya mara tatu na kuongeza mara mbili ufanisi wa nishati jadidifu ifikapo mwaka 2030 na kupiga hatua kuhusiana na marekebisho na ufadhili wa fedha.

Maendeleo mengine pia yalifanywa kuhusiana na kujenga mnepoufadhili wa fedha, ikiwa ni pamoja na uendeshaji wa mfuko wa hazina kwa jili ya Hasara na Uharibifu, ingawa ahadi za kifedha ni ndogo sana, kulingana na Katibu Mkuu.

Lakini mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba mengi zaidi yanahitajika ili kutoa haki ya mabadiliko ya tabianchi kwa wale walio mstari wa mbele wa mgogoro huo.

Amesema “Nchi nyingi zilizo hatarini zinazama katika madeni na ziko katika hatari ya kuzama katika bahari inayoongezeka kina. Ni wakati wa kuongeze fedha, ikiwa ni pamoja na kujenga mnepo, kukabiliana na hasara na uharibifu na mageuzi ya usanifu wa fedha wa kimataifa.

Ameongeza kuwa ulimwengu hauwezi kumudu "ucheleweshaji, kutokuwa na uamuzi, au hatua nusu na akasisitiza kwamba “Licha ya tofauti nyingi, ulimwengu unaweza kuungana na kukabiliana na changamoto ya janga la mabadiliko ya tabianchi. Ushirikiano wa kimataifa unasalia kuwa tumaini bora la ubinadamu." 

"Ni muhimu kukusanyika pamoja karibu na suluhisho halisi, la vitendo na la maana la mabadiliko ya tabianchi ambalo linalingana na kiwango cha janga la tabianchi."

Taasisi ya kiraia yenye makao yake makuu nchini Nepal ya Digo Bikas Institute inashikilia hatua juu ya hasara na uharibifu wakati wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) katika Jiji la Expo huko Dubai, Falme za Kiarabu.
COP28/Christopher Edralin
Taasisi ya kiraia yenye makao yake makuu nchini Nepal ya Digo Bikas Institute inashikilia hatua juu ya hasara na uharibifu wakati wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) katika Jiji la Expo huko Dubai, Falme za Kiarabu.

Ni njia ya kuelekea na sio mwisho wa safari

Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi Simon Stiell amesema, "hatua za kweli za kusonga mbele zimepigwa katika COP28, lakini mipango iliyotangazwa huko Dubai ni "njia ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na, sio mwisho wa safari hiyo."

Bwana. Stiel amesema uhakiki wa kimataifa  ambao unalenga kusaidia mataifa kuoanisha mipango yao ya kitaifa ya tabianchi na Mkataba wa Paris imefichua wazi kwamba maendeleo si ya haraka vya kutosha, lakini "bila shaka yanaongezeka kwa kasi.”

Amesema bado, mwelekeo wa sasa uko chini ya nyuzijoto 3C za ongezeko la joto duniani linalosababisha mateso makubwa ya binadamu, ndiyo maana COP28 ilihitaji kusogeza sindano zaidi kuhusu suala hili.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa mkutano, Bwana. Stiell amesema COP28 inahitajika kuashiria kukomesha kwa changamoto kuu ya mabadiliko ya tabianchi ambalo ni janga la kinadamu  ambayo ni "mafuta kisukuku na uchafuzi wake unaopasha moto a sayari".

Amesema ingawa hawakufungua ukurasa mpya kabisa wa kutokomeza mafuta kisukuku Dubai lakini makubaliano hayo yanayoa ishara ya kuanza utokomezaji wa mafuta hayo ambayo ni kichocheo kikubwa cha mabadiliko ya tabianchi. 

Stiel ameongeza kuwa “makubaliano hayo yameweka msingi wa mpito wa haraka, wa haki na usawa, unaounga mkono kupunguzwa kwa kiasi kikubwa kwa uzalishaji wa hewa chafuzi na kuongezwa kwa ufadhili. Mkataba huu ni sakafu kabambe, sio dari. Kwa hivyo, miaka muhimu inayokuja lazima iendelee kukuza tamaa na hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi”.

Wanawake wanatembea katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab iliyofurika kaskazini mashariki mwa Kenya.
© UNHCR/Mohamed Maalim
Wanawake wanatembea katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab iliyofurika kaskazini mashariki mwa Kenya.

Nini kingine kilichojiri COP28

1. Mfuko wa hazina ya hasara na uharibifu iliyoundwa kusaidia nchi zinazoendelea zilizo hatarini kwa mabadiliko ya tabianchi ilianzishwa katika siku ya kwanza ya COP28. Nchi zimeahidi mamia ya mamilioni ya dola kufikia sasa kwa ajili ya mfuko huo.

2. Ahadi za thamani ya dola bilioni 3.5 kujaza rasilimali za Mfuko wa Hali ya Hewa unaojali mazingira.

3. Matangazo mapya ya jumla ya zaidi ya dola milioni 150 kwa Hazina ya Nchi Zinazoendelea (LDC) na Hazina Maalum ya Mabadiliko ya Tabianchi (SCCF)

4. Ongezeko la dola bilioni 9 kila mwaka la Benki ya Dunia ili kufadhili miradi inayohusiana na mabadiliko ya tabianchi (2024 na 2025);

5. Takriban nchi 120 ziliunga mkono Azimio la mabadiliko ya tabianchi na afya la COP28 la UAE ili kuharakisha hatua za kulinda afya ya watu kutokana na athari zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi.

6. Zaidi ya nchi 130 zimetia saini Azimio la COP28 la UAE kuhusu Kilimo, Chakula na mabadiliko ya tabianchi ili kusaidia uhakika wa chakula wakati wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi;

7. Ahadi ya Kupoza Ulimwenguni imeidhinishwa na nchi 66 ili kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi unaohusiana na vifaa vya kupoza au kuweka baridi kwa asilimia 68 kuanzia leo.

Nini kinafuata?

• Awamu inayofuata ya mipango ya kitaifa ya utekelezaji wa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi au Michango Iliyoamuliwa Kitaifa inakuja mwaka wa 2025, wakati nchi zinatarajiwa kuimarisha kwa vitendo ahadi zao.

• Azerbaijan ilitangazwa kuwa mwenyeji rasmi wa COP29 kuanzia Novemba 11 hadi 22 mwaka ujao baada ya kupokea uungwaji mkono wa mataifa ya Ulaya Mashariki kufuatia kujiondoa kwa Armenia kwenye zabuni.

• Brazili imejitolea kuandaa COP30 huko Amazon mwaka 2025.

Hisia tofauti kuhusu matokeo ya mkutano

Licha ya duru nyingi za makofi ndani ya kikao hicho, sio wajumbe wote waliofurahishwa na matokeo ya mazungumzo hayo ya tabianchi.

Wawakilishi wa mashirika ya kiraia na wanaharakati wa tabianchi, pamoja na wajumbe kutoka nchi za visiwa vidogo vinavyoendelea walionekana kutofurahishwa na matokeo.

Anne Rasmussen, mwakilishi wa Samoa na mshiriki mkuu wa majadiliano wa Muungano wa Nchi za Visiwa Vidogo (AOSIS), alidokeza kutofurahishwa na uamuzi huo ulitolewa wakati wa kutokuwepo kwao katika chumba cha mashauriano kwa vile kundi lao lilikuwa bado linaratibu majibu yake kwa maandishi.

Amelalamika kwamba hawawezi "kumudu kurudi kwenye visiwa vyao na ujumbe kwamba mchakato huu umetushinda."

Akisisitiza umuhimu wa mchakato wa uhakiki wa kimataifa amesema "GST hii ya kwanza ina umuhimu fulani. Ndiyo GST pekee ambayo ina umuhimu wa kuhakikisha kwamba bado tunaweza kupunguza ongezeko la joto duniani hadi nyuzijoto 1.5C.”

Bi. Rasmussen amesikitishwa na kushindwa "Kurekebisha mwelekeo na ameonyesha kusikitishwa na maendeleo ya ziada kuhusu biashara kama kawaida, wakati tulichohitaji sana ni mabadiliko makubwa katika vitendo na msaada wetu."

Katibu Mkuu António Guterres akiwa na wanaharakati vijana wa hali ya hewa katika Mkutano wa Utekelezaji wa Hali ya Hewa huko COP27 huko Sharm el-Sheikh, Misri.
UNFCCC/Kiara Worth
Katibu Mkuu António Guterres akiwa na wanaharakati vijana wa hali ya hewa katika Mkutano wa Utekelezaji wa Hali ya Hewa huko COP27 huko Sharm el-Sheikh, Misri.

Mara tu baada ya kutolewa kwa hati ya mwisho, Harjeet Singh, mkuu wa mkakati wa kisiasa wa kimataifa katika Climate Action Network International ameiambia UN News kwamba "Baada ya miongo kadhaa ya ukwepaji, COP28 hatimaye imetoa mwangaza wa wazi juu ya wahusika halisi wa mgogoro wa tabianchi ambao ni nishati ya mafuta kisukuku, mwelekeo wa muda mrefu wa kuondoka kutoka kwenye makaa ya mawe, mafuta, na gesi umewekwa.

"Lakini azimio hilo limegubikwa na mianya ambayo inatoa fursa kwa tasnia ya mafuta kuwa na njia nyingi za kutoroka, kutegemea teknolojia ambazo hazijathibitishwa na zisizo salama.

Bwana. Singh pia amedokeza kwa kile alichokiona kama "unafiki wa mataifa tajiri  yanapoendelea kupanua shughuli za mafuta kwa wingi huku wakitoa huduma ya mdomo kwa mabadiliko ya tabianchi."

Nchi zinazoendelea ambazo bado zinategemea nishati ya mafuta, amesema, zimeachwa bila hakikisho thabiti la usaidizi wa kutosha wa kifedha katika "mabadiliko yao ya haraka na ya usawa kuelekea nishati mbadala. Wakati COP hii imetambua upungufu mkubwa wa kifedha katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi matokeo ya mwisho yanamapungufu na kulazimisha mataifa tajiri kutimiza majukumu yao ya kifedha”.