Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lazima tuongeze nishati mbadala mara mbili ya sasa katika miaka 8 ijayo: WMO

Uchafuzi wa hewa katika mji wa Ulaanbaatar, Mongolia.
© UNICEF/Tamir Bayarsaikhan
Uchafuzi wa hewa katika mji wa Ulaanbaatar, Mongolia.

Lazima tuongeze nishati mbadala mara mbili ya sasa katika miaka 8 ijayo: WMO

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO limesema usambazaji wa umeme kutoka vyanzo vya nishati safi lazima uongezeke mara mbili ndani ya miaka minane ijayo ili kupunguza ongezeko la joto duniani na iwapo hilo halitafanyika, kuna hatari kwamba mabadiliko ya tabianchi, kuongezeka kwa hali mbaya zaidi ya hewa pamoja na shida ya maji vitadhoofisha uhakika wa upatikanaji wa nishati na hata kuhatarisha usambazaji wa nishati mbadala. 

Ripoti ya kila mwaka ya hali ya huduma za hali ya hewa ya WMO, ambayo inajumuisha maoni kutoka kwa mashirika 26 tofauti, mwaka huu inaangazia nishati kwa sababu inaamini kuwa nishati ndio inayoshikilia ufunguo wa makubaliano ya kimataifa juu ya maendeleo endelevu na mabadiliko ya tabianchi kwa afya ya sayari dunia.

Katibu mkuu wa WMO Profesa Petteri Taalas amesema hakuna wakati wa kupoteza kwa kuwa hali ya hewa inabadilika mbele ya macho yetu na kwamba kunahitajika mabadiliko kamilifu ya mfumo wa nishati duniani.

“Sekta ya nishati ndio chanzo mara tatu cha uzalishaji wa gesi chafu duniani. Kubadilika kwenda kwenye uzalishaji wa nishati safi kama vile nishati ya jua, upepo na maji na kuboresha ufanisi wa nishati ni suala muhimu ikiwa tunataka kustawi katika karne hii ya 21.”

Amesema mkuu huyo wa WMO na kuongeza kuwa “Kama lengo ni kufikia kutozalisha kabisa hewa ukaa ifikapo mwaka 2050 tutaweza kufikia hapo tu iwapo tutaongeza usambazaji mara mbili wa nishati yenye kiwango cha chini cha uchafuzi katika kipindi cha miaka minne ijayo.”

WMO pia wamesisitiza umuhimu wa kupatikana kwa taarifa za uhakika za hali ya hewa, maji na mabadiliko ya tabianchi ili kuimarisha miundombinu ya nishati na kukidhi mahitaji yanayoongezeka (mpaka sasa kuna ongezeko la asilimia 30 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita).

Familia huko nchini Burkina Faso ikienda kusaka maji. Nchini humo zaidi ya watu 950,000 hawana uhakika wa chakula kutokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha ukame na hivyo kukwamisha shughuli za kilimo na ufugaji.
OCHA/Otto Bakano

Matumaini kwa Afrika

Mahitaji ya nishati ya umeme yanategemewa kuongezeka maradufu ikifapo mwaka 2050 hivyo ni vyema kuwekwa mikakati ya kuhakikisha umeme unaozalishwa hauchafui mazingira na nishati mbadala kama nishati ya jua inakuwa chanzo kikubwa zaidi cha usambazaji.

Nchi za Kiafrika zina fursa kubwa zaidi ya kuzalisha nishati mbadala na katika soko la nishati mbadala kwa kuwa ina asilimia 60% ya rasilimani bora zaidi za jua hata hivyo ina uwezo wa asilimia 1% wa kuzalisha. 

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Nishati la Kimataifa Fatih Birol anasema lazima mabadiliko yafanyike haraka katika eneo hili na yatawezekana iwapo kutakuwa na mipango ya muda mrefu pamoja na será za kuchochea uwekezaji ambazo zitatungwa kwakuangalia takwimu za mabadiliko ya hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi.

“Tunahitaji haraka kukabiliana na athari zinazoongeza za mabadiliko ya tabiachi kwenye mifumo ya nishati ikiwa tunaraja kudumisha uhakika wa nishati huku tukiharakisha kifikia uzalishaji sifuri wa hewa chafuzi.” Amesisitiza

Kauli yake hii iliungwa mkono na Mkurugenzo wa IRENA Francesco L Camera ambaye alieleza kuwa “sasa ni wakati wa kuharakisha mpito wa kufikia nishati mbadala hapo baadae. Kitu chochote kisicho na hatua Kali na za haraka kitaondoa uwezo wa kikaa kwenye njia ya kifikia 1.5°C. nishati mbadala ni chagua la kimkakati la kuleta nishati nafuu, ajira, ukuaji wa kiuchumi na mazingira thabiti kwa watu na jamii mashinani.”

Mzozo na ukame vimesababisha ukosefu wa chakula katika maeneo mengi ya Somalia
© WFP/Kevin Ouma

Lakini Afrika ndio inaathirika zaidi

Afrika tayari inakabiliwa na mlolongo wa athari za mabadliko ya tabia nchi ikiwemo ukame mkali ilihali wao ni wachangiaji wa kiwango cha chini zaidi wa tatizo la uharibifu wa mazingira.

Ili kuleta upatikanaji wa nishati ya kisasa kwa Waafrika wote kunahitaji uwekezaji wa dola bilioni 25 kila mwaka, ambayo ni karibu asilimia 1 ya uwekezaji wa nishati duniani leo.

Ni asilimia 2 tu ya uwekezaji wa nishati safi katika miongo miwili iliyopita ulifanywa barani Afrika.

Kupungua kwa gharama za teknolojia safi kunashikilia ahadi mpya kwa mustakabali wa Afrika kuweza kufanya uzalishaji na kuna fursa kubwa kwa Afrika kusaidia kuziba pengo la hitaji la nishati mbadala.

Kufikia malengo ya Afrika ya nishati na mabadiliko ya tabianchi kunamaanisha zaidi ya uwekezaji wa nishati mara mbili katika muongo huu, na ongezeko kubwa la kukabiliana na hali hiyo.

Maeneo ya makazi yaliyofurika kwenye kijiji kimoja jimboni Sindh nchini Pakistan.
© UNICEF/Asad Zaidi

Kuhusu ripoti ya WMO

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, hatua kali za kupambana na mabadiliko ya tabianchi zinaweza kuleta manufaa yenye dhamani ya kufikia dola trilioni 26  kiuchumi ifikapo 2030. Na bado, uwekezaji katika nishati mbadala ni mdogo sana, hasa katika nchi zinazoendelea na tahadhari ndogo sana inawekwa kwkauangalia umuhimu wa hali ya hewa.

WMO imetoa ripoti za kila mwaka kuhusu hali ya huduma za hali ya hewa tangu 2019 ikiwa ni kujibu ombi la Umoja wa Mataifa la kutolewa kwa taarifa juu ya mahitaji ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Toleo la mwaka huu linajumuisha maoni kutoka kwa washirika mengi zaidi kuliko hapo awali. Mashirika hayo ni pamoja na Wakala wa Kimataifa wa Nishati (IEA), Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (IRENA), Nishati Endelevu kwa Wote (SE4ALL), Nishati ya UN, Wakfu wa ENEL, Mfuko wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, Mfuko wa Hali ya Hewa ya Kijani (GCF), Global Environment Facility (GEF), Huduma ya Mabadiliko ya Tabianchi ya Copernicus (C3S) na nyinginezo, ikijumuisha sekta binafsi na mashirika ya kiraia.

Kusoma mengi kuhusu ripoti hiyo na maeneo matano ya kupigiwa mfano yaliyoanishwe kwenye ripoti hiyo ya WMO bofya hapa.