Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
 Barabara inayoelekea kwenye kisiwa katika Ghuba ya Mexico katika jimbo la Louisiana nchini Marekani inamomonyoka taratibu kutokana na maji ya bahari.

Joto laendelea kuongezeka duniani kwa mwaka wa 7 mfululizo: WMO

Climate Visuals Countdown/Stacy Kranitz
Barabara inayoelekea kwenye kisiwa katika Ghuba ya Mexico katika jimbo la Louisiana nchini Marekani inamomonyoka taratibu kutokana na maji ya bahari.

Joto laendelea kuongezeka duniani kwa mwaka wa 7 mfululizo: WMO

Tabianchi na mazingira

Viashiria vinne vinavyotumika kupima hali ya hewa duniani vyote vimeonesha hali kuendelea kuwa mbaya duniani licha ya wadau kila uchao kujadiliana na kuahidi kuchukua hatua madhubuti za kulinda dunia kutoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na shughuli za kibinadamu. 

Viashiria hivyo vinne muhimu vya kuonesha mabadiliko ya hali ya hewa duniani ni viwango vya gesi chafuzi katika tabaka la ozoni, kupanda kwa kina cha bahari, joto la bahari pamoja na tindikali ya bahari kuongezeka, na kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa mapema hii leo na shirika la Umoja wa Mataifa la utabiri wa hali ya hewa duniani, WMO ambayo imethibitisha kuwa mwaka 2021 ukiwa ni mwaka wa saba mfululizo umekuwa kumekuwa na ongezeko la joto. 

Wastani wa joto lililoongezeka mwaka jana (2021) ni nyuzi joto 1.11 hii ikimaanisha ni sawa na ongezeko la nyuzi joto 0.13 katika Selsiyasi juu ya kiwango cha kawaida. Na sababu kubwa ikielezwa ni tukio la La Nina mwanzoni na mwishoni mwa mwaka 2021. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametumia ripoti hiii kutoa wito wa hatua za haraka kuchukuliwa ili kuepusha dunia kuzidi kufanya uharibifu wa hali ya hewa akieleza ni vyema dunia “Kuchukua matunda yanayo ning’inia kwa kufanya mabadiliko ya matumizi ya nishati, badala ya kusubiri mpaka kuona mwisho uliokufa wa matumizi ya mafuta ya kisukuku.”

Guterres amesisitiza umuhimu wa kutumia nishati jadidifu na kupendekeza hatua tano muhimu ili kuanza kwa mpito wa nishati hiyo mbadala zikijumuisha ufikiaji mkubwa wa teknolojia ya nishati mbadala na vifaa, kuongezeka mara tatu kwa uwekezaji wa kibinafsi na wa umma katika reli, na kukomesha kutoa ruzuku kwa nishati ya mafuta ya kisukuku ambayo kwa sasa inafikia takriban dola milioni kumi na moja (11) kwa dakika. “Nishati jadidifu ndio njia pekee salama, ya uhakika na itakayotoa hakikisho la ajira kwa watu” amesema Guteres 

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa WMO Prof. Petteri Taalas amesema kwa hali ilivyo sasa ni lazima dunia ichukue hatua katika muongo huu ili kuzuia athari za hali ya hewa zinazozidi kuwa mbaya na kuweka ongezeko la joto hadi chini ya nyuzi joto 1.5 katika selsiyasi. 

“Hali ya hewa inabadilika mbele ya macho yetu, ni suala la muda kabla hatujaona mwaka mwingine wenye joto zaidi katika rekodi," ameeleza Prof. Taalas.

Mkuu huyo wa WMO amefafanua kuwa, kupanda kwa kina cha bahari, joto la bahari kuongezeka na kuongeza kwa chumvi habarini kutaendelea kuwa na athari kwa mamia ya miaka iwapo hatua za haraka hazitavumbuliwa za kusaidia kupunguza uharibifu wa tabaka la ozoni na mpaka sasa  athari zinazidi kushamiri ulimwenguni akitolea mfano zaidi ya watu bilioni 2 tayari wana shida ya maji.