Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Magenge ya uhalifu ya kimataifa yanadhoofisha serikali; tuchukue hatua- Guterres

Pikipiki zikitumika kusafirisha kiharamu nishati ya mafuta huko Dosso, Niger karibu na mpaka wa nchi hiyo.
© Harouna Ousmane Ibrahim
Pikipiki zikitumika kusafirisha kiharamu nishati ya mafuta huko Dosso, Niger karibu na mpaka wa nchi hiyo.

Magenge ya uhalifu ya kimataifa yanadhoofisha serikali; tuchukue hatua- Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema hatua zaidi thabiti zinahitajika ili kukabiliana na changamoto inayoongezeka kila uchao ya uhalifu uliopangwa ambao unafanyika kimataifa, uhalifu ambao unavuka mipaka ya kitaifa.

Guterres amesema hayo akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi, Baraza ambalo lilikutana kwenye mjadala wa wazi wa ngazi ya juu kuhusu aina hiyo ya uhalifu uliotapakaa katika maeneo mbali mbali duniani.

Katibu Mkuu amesihi nchi ziimarishe ushirikiano, utawala wa sheria na hatua za kuzuia “dhidi ya aina hii ya tishio linalojirudiarudia la amani, usalama na maendeleo endelevu, linalotokea maenoe mbali mbali ikiwemo kwenye mitandao – eneo ambalo ni fursa ya kujitajirisha kwa wahalifu.”

Uhalifu tofauti tofauti, matokeo  yanayofanana

Uhalifu wa kupangwa unaofanywa kimataifa ni sekta inayojipatia mabilioni yad ola ukihusisha utoroshaji wa fedha, biashara haramu ya silaha, usafirishaji haramu wa binadamu, usafirishaji haramu wa maliasili na bidhaa nyingine, vyote ambavyo vina uhusiano.

Ingawa ni katika aina tofauti tofauti, “madhara yake yanafanana: kudhoofisha utawala, ufisadi na ukosefu wa sheria, ghasia kufanyika kwa uwazi, vifo na uharibifu,” amesema  Bwana Guterres.

Halikadhalika, uhalifu wa kimataifa uliopangwa, pamoja na mizozo, huimarishana au kusaidiana, amesema Katibu Mkuu, na hivyo kudhoofisha mamlaka na uthabiti wa taasisi za serikali, humomonyoa utawala wa sheria, na kuvuruga mifumo ya usimamizi wa sheria.

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu uhalifu wa kupangwa wa kimtaifa Alhamisi 7, Desemba 2023.
UN Photo/Loey Felipe
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu uhalifu wa kupangwa wa kimtaifa Alhamisi 7, Desemba 2023.

Huchochea vurugu na mizozo

Guterres ametoa mfano wa uhalifu wa kupangwa wa kimataifa katika maeneo mbali mbali duniani kama vile Afghanistan na Colombia ambako uzalishaji wa dawa za kulevya na usafirishaji vimechochea mizozo ya kikatili na ya muda mrefu.

Amegusia pia Haiti, ambayo imenasa katika mzunguko wa kuporomoka kwa serikali, kuchochea uhalifu wa magenge na kuongezeka kwa biashara haramu ya silaha zinazongizwa nchini humo na kuwezesha magenge kudhibiti miundombinu kama vile bandari na hata barabara kuu.

Katika mizozo mingi, kwa muijbu wa Katibu Mkuu, shughuli za makundi yanayohusika na uhalifu wa kimataifa na makundi yaliyojihami zinaendana, na hivyo kufanya harakati za kumaliza mizozo kuwa ngumu.

Uhusiano na ugaidi

Guterres amesem kuna uhusiano kati ya uhalifu wa kupangwa wa kimataifa na ugaidi, jambo ambalo amesema linatia hofu.

Mathalani katika Ukanda wa Sahel barani Afrika, biashara haramu  ya mafuta, dawa za kulevya, silaha na maliasili, inawezesha makundi yaliyojihami kupata silah na kutishia maisha ya wananchi na mbinu zao za kujipatia kipato.

Ijapokuwa Baraza la Usalama  kwa muda mrefu limetambua hatari ya uhalifu wa kimataifa wa kupangwa kwa amani na usalama duniani, “lazima tuchukue hatua zaidi tuimarishe ulinzi wetu,” amesema Katibu Mkuu akitaja maeneo matatu ya kupatiwa kipaumbele.

Adriana Scordamaglia, mwendesha mashtaka wa masuala ya kazi nchini Brazil anaonekana hapa wakati wa zoezi la kujifunza jinsi ya kutambua na kukagua usafirishaji haramu wa binadamu.
UNODC Perú/Coral Estudio
Adriana Scordamaglia, mwendesha mashtaka wa masuala ya kazi nchini Brazil anaonekana hapa wakati wa zoezi la kujifunza jinsi ya kutambua na kukagua usafirishaji haramu wa binadamu.

Maeneo hayo mosi, ni ushirikiano na makubaliano hasa utekelezaji kwa kina wa  Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Uhalifu wa kimataifa wa kupanga  pamoja na itifaki zake tatu, na pia kushirikiana kwenye uchunguzi na ufunguliaji mashtaka watuhumiwa.

Pili ni umuhimu wa kuimarisha utawala wa sheria ambao “ndio msingi wa juhudi zetu za kusaka kwa amani suluhu za mizozo, na kushughulikia vitisho lukuki vinavyosababishwa na uhalifu wa kimataifa uliopangwa.

Tatu, ni kuchagiza ujumuishaji zaidi kwa kuchukua hatua za kuzuia kwa kujumusha pande zote zinazohusika ikiwemo kuongeza juhudi za kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu ya UN kwa maslahi ya wote.

Magenge yahusika na robo ya matukio ya mauaji duniani- UNODC

Kwa upande wake Ghada Waly, ambaye ni Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuzuia dawa za kulevya na uhalifu, (UNODC), ametilia mkazo wito wa Katibu Mkuu wa hatua za pamoja dhidi ya aina hii ya uhalifu.

Alipitia ripoti inayochapishwa Ijumaa ambayo inaonesha kuwa magenge ya uhalifu wa kupangwa yanahusika na takribani robo ya matukio yote ya mauaji duniani.

Amesema makundi hayo yamejipanga zaidi na yamefika mashinani na kuwa na wataalamu. “Tunahitaji taasisi zenye uwezo wa kutoa haki na kumaliza ukwepaji sheria, pamoja na jamii zenye mnepo. Tunahitaji kuwekeza rasilimali zaidi ili kukabili masoko haramu ya yenye thamani ya matrilioni ya dola.”

Ghada Waly, Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi y Umoja wa Mataifa ya kuzuia dawa za kulevya na uhalifu akihutubia Baraza la Usalama la UN wakati wa mkutano kuhusu uhalifu wa kupangwa wa kimataifa.
UN Photo/Loey Felipe
Ghada Waly, Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi y Umoja wa Mataifa ya kuzuia dawa za kulevya na uhalifu akihutubia Baraza la Usalama la UN wakati wa mkutano kuhusu uhalifu wa kupangwa wa kimataifa.