Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Kenya kwa kutumia Sheria ya Uhalifu wa Kimataifa- UN

Mji mkuu wa Nairobi, Kenya
World Bank/Sambrian Mbaabu
Mji mkuu wa Nairobi, Kenya

Heko Kenya kwa kutumia Sheria ya Uhalifu wa Kimataifa- UN

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Türk ameipongeza serikali ya Kenya kwa kile alichoeleza ni hatua muhimu ya kuelekea uwajibikaji kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Kenya, kufuatia uamuzi wake wa wa kutumia Sheria ya Uhalifu wa Kimataifa kuwafungulia mashitaka maafisa wakuu wa polisi kwa mauaji, ubakaji na utesaji kama uhalifu dhidi ya ubinadamu kufuatia vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo mwaka 2017

Taarifa iliyotolewa hii leo huko Geneva, Uswisi na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu imemnukuu Kamishna Mkuu wa Umoja wa Matifa wa Haki za binadamu Volter Turk akipongeza Kenya na kusema hii ni mara ya kwanza kwa Kenya kutumia Sheria ya Kimataifa ya Uhalifu kushtaki uhalifu dhidi ya ubinadamu katika mahakama zake za ndani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wakati wa uchaguzi mkuu wa Kenya mwaka 2017, Tume ya Taifa  ya Haki za Kibinadamu ilirekodi vifo 94 na matukio 201 yakihusiana na unyanyasaji wa kingono na zaidi ya majeruhi 300 wengi wao wakieleza kufanyiwa vitendo hivyo na vikosi vya usalama.

Bwana Turk amesema “Uamuzi uliochukuliwa leo na Kenya ni wa msingi, ni hatua nzuri kuelekea haki na uwajibikaji kwa waathirika na familia za waathirika, wa ghasia za uchaguzi, na inaweza kuimarisha na kuzuia ukiukaji wa haki za binadamu kwa siku zijazo.”

Amebainisha kuwa uamuzi huo wa Kenya unatokana na maendeleo ya hivi karibuni ya taasisi za Kenya  zinazoungwa mkono na Ofisi yake ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu katika kuimarisha uwajibikaji kwa ukiukaji wa haki za binadamu.

Kamishna Mkuu Türk amesema ofisi yake itaendelea kujitolea kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Kenya kuendeleza uwajibikaji kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na kushughulikia mauaji ya kiholela na kulazimisha watu kutoweka.