Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OHCHR yataka uchunguzi Gaza kufuatia madai ya ukatili wa kingono wakati wa shambulio la Hamas

Wanawake huko Gaza wakisafirisha vifurushi vya chakula vinavyosambazwa na WFP. (Maktaba)
© WFP/Ali Jadallah
Wanawake huko Gaza wakisafirisha vifurushi vya chakula vinavyosambazwa na WFP. (Maktaba)

OHCHR yataka uchunguzi Gaza kufuatia madai ya ukatili wa kingono wakati wa shambulio la Hamas

Amani na Usalama

Kamishina Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk leo amelaani vikali ukiukaji mkubwa wa haki wa kingono dhidi ya Waisraeli unaodaiwa kutekelezwa na wanamgambo wa Hamas wakati wa mashambulizi yao ya kigaidi kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, huku wahudumu wa kibinadamu huko Gaza wakionya kuhusu hali mbaya ya raia, kutokana na kunaendelea kwa mashambulizi ya mabomu na watu kutawanywa eneo la Kusini.

Juliette Touma, ambaye ni msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, wakati wa mahojiano na vyombo vya habari yaliyochapishwa mtandaoni leo kuhusu hali ya Gaza amesema "Nadhani tumegonga mwamba na ni hatua ya mabadiliko katika vita hivi  hali inazidi kuwa mbaya kila dakika tunapokea simu za mara kwa mara za dharura kutoka kwa wafanyakazi wenzetu na marafiki."

Mashambulizi ya anga na ya roketi

Taarifa za hivi karibuni kutoka ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA, zinaonyesha "kuongezeka kwa kiasi kikubwa kwa mashambulizi ya Israel kutoka angani, nchi kavu na baharini kote Gaza tangu Jumatatu mchana.”

Urushaji wa maroketi na makundi ya wapalestina yenye silaha kwenda nchini Israel pia umeongezeka limesema shirika la OCHA.

Kumekuwa na "mapigano makali kati ya majeshi ya Israel na makundi yenye silaha ya Palestina, hasa katika mji wa mashariki wa Gaza, katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia inayoripotiwa kuwa imezingirwa kaskazini, na katika maeneo ya mashariki ya Khan Younis upande wa kusini, ambapo makumi ya maelfu ya watu wametafuta usalama na jamaa zao katika makazi ya shirika la UNRWA ambayo tayari yamejaa pomoni.

"Tumekuwa na watu 60,000 wanaowasili katika saa chache zilizopita," amesema Bi Touma.

Wakimbizi wa ndani wakipumzika katika kambi karibu na hospitali ya Nasser Khan Yunis Kusini mwa Gaza
© UNFPA/Bisan Ouda
Wakimbizi wa ndani wakipumzika katika kambi karibu na hospitali ya Nasser Khan Yunis Kusini mwa Gaza

Suluhu ya Serikali Mbili

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Bwana. Türk amerejea wito wa awali wa kutaka mapigano yasitishwe haraka na kwa nchi zenye ushawishi kwa wapiganaji kuhakikisha kuwa kuwalinda raia kunakuwa kipaumbele, kulingana na sheria za vita.

Maoni hayo yamekuja baada ya Ofisi yake kusema kwamba "mtindo wa mashambulizi ambayo yanalenga raia au athari kwa miundombinu ya kiraia unaleta wasiwasi mkubwa juu ya Israeli kufuata sheria za kimataifa za kibinadamu na huongeza kwa kiasi kikubwa hatari ya uhalifu wa ukatili".

Ameongeza kuwa "Kama hatua ya haraka, natoa wito wa kusitishwa mara moja kwa uhasama. Pande zote zinafahamu ni nini kinahitajika ili kufikia amani na usalama kwa watu wa Palestina na Israel, vurugu na kisasi vinaweza tu kusababisha chuki zaidi na itikadi kali. Njia pekee ya kumaliza mateso yanayoongezeka ni kumaliza kazi na kufikia suluhisho la Serikali mbili.”

Mkuu huyo wa haki za Umoja wa Mataifa pia amelaani matukio ya maafa yanayotokea Gaza tangu vikosi vya ulinzi vya Israel kuanza kulipiza kisasi shambulio la kigaidi lililoongozwa na Hamas tarehe 7 Oktoba.

Hakuna viwango viwili

Bwana Türk pia amesisitiza wasiwasi wake mkubwa kuhusu taarifa za kudhalilisha utu na uchochezi zilizotolewa na maafisa wa ngazi za juu wa Israeli na wa zamani, pamoja na wapiganaji wa Hamas.

Amesema "Historia imetuonyesha ni wapi aina hii ya lugha inaweza kuongoza. Hili sio tu halikubaliki, lakini mahakama yenye uwezo inaweza kuona taarifa kama hizo, katika mazingira ambayo zilitolewa, kama uchochezi wa uhalifu wa kikatili."

Kamishna Mkuu pia amekanusha madai ya kuwa na viwango viwili kuhusu msimamo wa Umoja wa Mataifa juu ya mgogoro wa Gaza na kubainisha kuwa alikuwa amefahamishwa kuhusu madai ya unyanyasaji wa kijinsia  na kingono wakati wa shambulio la Hamas kwa jamii za kusini mwa Israeli.

Ilikuwa bayana kwa uchungu mkubwa kwamba “mashambulizi ya kikatili yanapaswa kuchunguzwa kikamilifu na kwa uchunguzi huru kwa sababu hilo ndilo deni letu kwa waathirika", amesema.

Lakini Türk pia amebainisha kuwa uchunguzi mkubwa vile vile wa haki za binadamu kama vile ule unaodaiwa kuwa wa mauaji ya halaiki ya raia huko Bucha, Ukraine, na vikosi vya Urusi Aprili 2022, ulichukua miezi tisa kuanzishwa.

Wapeni fursa wachunguzi wa UN 

Turk amesisitiza kwamba "Tuna deni kwa waathirika kwamba kuna uchunguzi wa kina juu ya madai hayo na kwamba haki inatendeka." 

Ameongeza kuwa Ofisi yake ilitoa ombi kwa Israeli katika wiki ya pili ya Oktoba kuruhusu timu ya wachunguzi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kufika kutekeleza kazi zao.

"Nimerudia wito huu na natumai utasikilizwa," ameongeza.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, tangu kuanza tena kwa mapigano tarehe 1 Disemba na hadi 5 Disemba, Wapalestina wasiopungua 1,207 wameuawa, ambapo asilimia 70 walikuwa watoto na wanawake.

Msaada wa kibinadamu umefikia makazi ya UNRWA huko Zawaida, Gaza ya Kati.
UN News/Ziad Taleb
Msaada wa kibinadamu umefikia makazi ya UNRWA huko Zawaida, Gaza ya Kati.

Usambazaji mdogo wa misaada

Taarifa ya OCHA imebainisha kuwa makumi ya malori ya misaada yaliyokuwa yamebeba vifaa vya kibinadamu na mafuta yaliingia kutoka Misri hadi Gaza jana Jumanne, lakini kwa siku ya tatu mfululizo, mkoa wa Rafah wa Gaza ndio pekee ambapo usambazaji mdogo wa misaada ulifanyika.

Katika eneo la karibu la Khan Younis, "usambazaji wa misaada ulisitishwa kwa kiasi kikubwa kutokana na kuongezeka kwa uhasama", ofisi ya misaada ya Umoja wa Mataifa imesema, wakati eneo la Kati la Gaza "limetenganishwa kwa kiasi kikubwa na kusini, kufuatia vikwazo vilivyowekwa kwenye barabara kuu na majeshi ya Israeli”. 

Ufikiaji wa maeneo ya kaskazini mwa Wadi Gaza ulisitishwa tarehe 1 Disemba na kuanza tena uhasama Ijumaa iliyopita ambao ulihitimisha usitishaji wa msaada kibinadamu wa wiki moja, OCHA imeongeza.

Miongoni mwa matukio mabaya zaidi ya hivi karibuni yaliyoripotiwa ambayo baadhi yake yaligonga majengo ya makazi OCHA inasema tarehe 4 Desemba "karibu saa 2:40 usiku, watu saba, ikiwa ni pamoja na wasichana wawili, waliripotiwa kuuawa huko Deir al-Balah. Mnamo tarehe 4 Desemba, karibu saa 3.40 usiku, watu saba waliripotiwa kuuawa huko Khan Yunis, tarehe 5 Desemba, karibu saa 7.30 asubuhi, watu 15 waliripotiwa kuuawa huko Jabalia, tarehe 5 Desemba, karibu saa 8.50 asubuhi, watu 10 wameripotiwa kuuawa katika kambi hiyo mpya ya Nuseirat, Eneo la Kati.”

Ni vigumu kufikisha misaada 

Mbali na mzozo wa kiafya unaokuja katika eneo hilo ambao ni matokeo ya msongamano wa watu na mazingira machafu ya kiafya, Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa Duniani WFP, pia limeonya jana kwamba kuanza tena kwa vita huko Gaza "kutazidisha janga la njaa ambalo tayari linatishia kuwashinda raia.”

Taarifa ya WFP imeeleza kuwa "mapigano mapya yanafanya usambazaji wa misaada kuwa karibu na kutowezekana na kuhatarisha maisha ya wafanyakazi wa kibinadamu".

Takriban Wapalestina 16,248 wameuawa huko Gaza wakati wa ongezeko la hivi karibuni la machafuko na karibu asilimia 70 walikuwa wanawake na watoto, OCHA imesema hayo ikitoa mfano wa takwimu za mamlaka ya afya ya Gaza. Imeongeza kuwa watu wengi hawajulikani waliko, labda wamefunikwa chini ya vifusi, wakisubiri kuokolewa