Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano Gaza yanaathiri misaada katika hali ambayo tayari ni jehanam: UN

Wanaume wakitembea kwenye vifusi na uchafu kutoka kwa majengo yaliyoharibiwa katika Jiji la Gaza, Oktoba 2023.
© WHO Wanaume wanatembea katika mitaa iliyoharibiwa ya Gaza.

Mapigano Gaza yanaathiri misaada katika hali ambayo tayari ni jehanam: UN

Amani na Usalama

Miezi miwili kabla ya siku ambayo mashambulizi ya kigaidi ya Hamas nchini Israel yachochee mashambulizi ya kulipiza kisasi kikubwa cha jeshi la Israel huko Gaza, hali katika eneo lililokumbwa na vita inazidi kuwa mbaya huku uhasama ukifanya juhudi za misaada ya kibinadamu kuelekea kushindikana wameonya leo  wahudumu wa misaada wa Umoja wa Mataifa.

Katika taarifa ya pamoja ya mashirika 27 ya misaada yakiwemo mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wao wametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano hayo, na kusisitiza kuwa hali ya Gaza ni "miongoni mwa hali mbaya zaidi ambayo tumeishuhudia".

Wakati huohuo leo wanajeshi wa Israel wameripotiwa kuingia katika mji wa Khan Younis kusini mwa Gaza, ambapo mamia ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao wamekuwa wakihifadhiwa.

Hakuna chakula ni mabomu tu

Mashambulizi makali ya Israel katika Ukanda wa Gaza na urushaji wa maroketi unaofanywa na makundi ya Wapalestina wenye silaha kwenda nchini Israel yameendelea katika muda wa siku mbili zilizopita, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA imesema, ambapo zaidi ya watu 100 wameripotiwa kuuawa jana Jumatano katika shambulio kwenye "majengo mengi ya makazi katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Gaza.”

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP katika eneo linalokaliwa la Palestina Samer AbdelJaber, ameandika kwenye ukurasa wake wa jukwaa la kijamii la X kwamba "Hakuna mtu katika eneo la Gaza aliye na chakula cha kutosha. Katika baadhi ya maeneo, watu tisa kati ya 10 wanalala mchana na usiku bila chakula,” wakati shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kupitia msemaji wake James Elder, ambaye hivi karibuni alirejea kutoka Gaza, ametoa muhtasari wa hali katika eneo hilo kuwa "Hakuna maji, hakuna usafi wa mazingira, hakuna chakula ni mabomu tu."

 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito kwa Baraza la Usalama jana Jumatano akitumia nyenzo adimu lakini yenye nguvu ya kifungu cha 99  cha katiba ya umoja wa Mataifa "kushinikiza kuepusha janga la kibinadamu na kuungana katika wito wa kusitishwa kikamilifu kwa mapigano kwa minajili ya kibinadamu.”

Katika barua kwa Baraza hilo, ambalo linatarajiwa kukutana katika kikao maalum katika siku zijazo, ameangazia "athari ambazo haziwezi kutenduliwa kwa Wapalestina kwa ujumla na kwa amani na usalama katika eneo hilo".

Mtu aliyevaa hoodie nyekundu akitafuta kifusi na uchafu katika jengo lililoharibiwa katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat.
© UNRWA/Ashraf Amra Watu wanatafuta mali zao kwenye vifusi katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat huko Gaza.

Tunahitaji amani kwa ajili ya afya

Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ameelezea kuunga mkono barua ya Bwana Guterres, akisisitiza kuwa "Mfumo wa afya wa Gaza umesambaratika. Tunahitaji amani kwa ajili ya afya,"

Kufikia jana Jumatano, WHO ilikuwa imeorodhesha mashambulio 212 dhidi ya huduma ya afya katika Ukanda huo yaliyoathiri vituo 56 na magari 59 ya kubeba wagonjwa. Ni hospitali 14 tu kati ya 36 za Gaza ambazo angalau zinafanya kazi kwa kiasi fulani.

Kituo cha hivi punde zaidi kilichoacha kufanya kazi, hospitali ya Kamal Adwan huko Jabalia, kimeshuhudia jana Jumatano uhamishaji wa wagonjwa na wafanyikazi wengi na mamlaka ya afya ya Gaza kutokana na mapigano makali na ukosefu wa mahitaji muhimu.

"Hii itawanyima maelfu ya watu huduma muhimu ya kuokoa maisha," ameonya Dkt. Tedros wa WHO.

Katika taarifa siku ya leo mtaalam huru aliyeteuliwa na Umoja wa Mataifa amelaani vikali vita visivyoisha vya Israel dhidi ya mfumo wa afya huko Gaza. "Tumeingia kwenye kina kirefu ambacho lazima tutoke humo haraka," amesema Tlaleng Mofokeng, Mtaalamu huyo Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya afya.

 Wataalam huru wa Umoja wa Mataifa huteuliwa na Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa na sio wafanyikazi wa Umoja wa Mataifa na hawapati malipo kwa kazi yao.

Usambazaji wa misaada umezuiwa

Wakati huo huo, malori yaliyokwama, kukatika kwa mawasiliano ya simu na kutokuwa na uwezo wa wafanyikazi kuripoti kwenye kivuko cha mpaka cha Rafah kutokana na uhasama imekuwa kikwazo kwa uwezo wa Umoja wa Mataifa kupokea misaada inayoingia, limesema shirika la OCHA.

 Kwa siku ya nne mfululizo jana Jumatano Rafah ilikuwa jimbo pekee huko Gaza ambalo ugawaji wa misaada ulifanyika.

Kwa mujibu wa OCHA, nguvu ya mapigano "ilisimamisha operesheni katika mkoa jirani wa Khan Younis. Hakujakuwa na njia ya kutoka kusini hadi maeneo ya kaskazini mwa Gaza tangu kusitishwa kwa mapigano kumalizika tarehe 1 Desemba.”

Mwanamume Mpalestina akiwabeba watoto wawili wadogo kupitia eneo lenye vifusi huko Gaza wakati wa mapumziko ya kibinadamu.
© UNRWA/Ashraf Amra Mwanamume akiwapeleka watoto wake kuelekea eneo salama wakipitia katika ardhi iliyolipuliwa kwa bomu katika Ukanda wa Gaza wakati wa usitishaji vita kwa ajili ya kufikisha msaada wa kibinadamu. (Maktaba)

 Jana Jumatano malori 80 ya misaada na lita 69,000 za mafuta yaliingia kupitia Rafah hadi Gaza ikiwa ni "chini ya wastani wa kila siku wa malori 170 na lita 110,000 za mafuta zilizoingia wakati wa usitishaji wa kibinadamu wa mapigano", OCHA imesisitiza.

Uokozi katika kambi ya Khan Younis

 Mapigano katika mji wa Khan Younis yamesukuma makumi ya maelfu ya watu kukimbilia Rafah katika siku chache zilizopita, limesema shirika hilo la misaada ya kibinadamu. 

Jana pia shule tano zinazosimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA na zinazohudumu kama makao ya muda katika mkoa wa mashariki wa Khan Younis zilihamishwa kufuatia amri kutoka kwa jeshi la Israel.

 Zaidi ya hayo, eneo linalochukua takriban robo ya jiji la Khan Younis liliteuliwa na jeshi la Israel kwa ajili ya kuhamishwa mara moja.

 Huko Rafah, makazi yamezidiwa uwezo wake na watu wanaowasili wamekuwa wakifikia mitaani na katika maeneo ya wazi kote jijini. 

UNRWA inawasaidia waliokimbia makazi yao kwa mahema huku WFP ikisambaza vyakula vya moto, katikati ya kile ambacho shirika hilo la mpango a chakula la Umoja wa Mataifa limekiita "janga kubwa la njaa katika Ukanda huo.