Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP28: Utaalamu wa wanawake kwenye kukabili madhara ya tabianchi utambuliwe

Hillary Clinton (katikati) na wanajopo wengine wakiwa katika picha ya pamoja kufuatia mjadala kuhusu jinsia na hali ya hewa.
© COP28/Christophe Viseux
Hillary Clinton (katikati) na wanajopo wengine wakiwa katika picha ya pamoja kufuatia mjadala kuhusu jinsia na hali ya hewa.

COP28: Utaalamu wa wanawake kwenye kukabili madhara ya tabianchi utambuliwe

Tabianchi na mazingira
  • Sera zinapitishwa lakini pekee hazitoshi 
  • Wanawke wana majawabu ya kuhimili na kukabili tabianchi 
  • Mifano iko dhahiri na inaleta ahueni kule kwenye changamoto 

Sera pekee za kujumuisha wanawake kwenye harakati za kukabili na kuhimili madhara ya mabadiliko ya tabianchi hazitoshi, badala yake ufahamu, utaalamu na stadi walizonazo wanawake vinapaswa kutambuliwa ili view na mchango Madhubuti katika hatua kwa tabianchi.  

Huo ni mtazamo kutoka COP28 ambao ni mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi,  UNFCCC unaoendelea huko Dubai, katika Umoja wa FAlme za Kiarabu.  

Wakulima wanawake. Ukuta wa kijani wasongesha amani na kurejesha ukijani.
©Artisan Productions / UNEP
Wakulima wanawake. Ukuta wa kijani wasongesha amani na kurejesha ukijani.

Ni kwa vipi wanawake na wasichana wana majawabu mujarabu?  

Mtazamo huo umetolewa wakati wa mkutano wa wanawake viongozi na wanaharakati ambao walipaza sauti zao leo kwenye mkutano ulioangalia jinsi ya kuondokana na pengo la kijinsia na kupunguza madhara makubwa ya mabadiliko ya tabianchi kwa wanawake na wasichana.  

Mila zilizoko na ukosefu wa usawa pamoja na ushiriki usio sawia kwenye mchakato wa kupitisha maamuzi, vinazuia wanawake wasichangie ipasavyo kwenye majawabu ya tabianchi.  

Na kinachotia shaka zaidi, ni ripoti iliyozinduliwa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia masuala ya wanawake, UN Women ikidokeza kuwa ifikapo mwaka 2050, mabadiliko ya tabianchi yanaweza kusukuma  wanawake na wasichana milioni 158 kwenye umaskini  na wengine milion 236 watakabiliwa na ukosefu wa kupata chakula.  

Lakini, ripoti inasema kuwa kuna matumaini, kwani wanawake wanaweza na wanabeba jukumu muhimu kwenye majawabu ya tabianchi, kama ilivyooneshwa kwenye siku ya usawa wa kijinsia katika COP28, ambapo wanawake waleta mabadiliko walionesha jinsi wao wanasongesha hatua kivitendo.  

Wanawake wanahakikisha kiwango cha joto kinazingatia makubaliano ya Paris  

Mjadala uliopatiwa jina ‘Wanawake wainuka kwa ajili ya wote’ uliandaliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya ubia ambapo ulisisitiza dhima ya uongozi ya wanawake katika kusongesha majawabu kwa mujibu wa Mkataba wa Paris.  

“Wanawake wako mstari wa mbele kwenye vita dhidi ya tabianchi. Iwe ni wanasayansi, wabunge, viongozi wa jamii za watu wa asili, vijana wanaharakati, wote wanapigania kuhakikisha kiwango cha joto hakivuki nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi, amesema Amina Mohammed, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye ujumbe wake kwa njia ya video wakati wa mjadala huo.  

Akipazia sauti ujumbe huo, Jemimah Njuki, Mchumi Mkuu wa uwezeshaji wa kiuchumi katika UN Women, amesema, “licha ya kutokuwa na rasilimali za kutosha, tunaona pia hatua nyingi zinazoongozwa na wanawake na wasichana na iwapo tutawapatia rasilimali, ikiwemo rasilimali fedha ili wachukue hatua zaidi, basi nadhani dunia yetu itakuwa bora zaidi.”  

Sima Bahous, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake akizungumza wakati wa Mazungumzo ya Ngazi ya Juu kuhusu Mabadiliko ya Haki ya Kuzingatia Jinsia na Hatua za Hali ya Hewa kwenye ukumbi wa michezo wa Al Waha wakati wa Mkutano wa …
© COP28/Christophe Viseux
Sima Bahous, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake akizungumza wakati wa Mazungumzo ya Ngazi ya Juu kuhusu Mabadiliko ya Haki ya Kuzingatia Jinsia na Hatua za Hali ya Hewa kwenye ukumbi wa michezo wa Al Waha wakati wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP28 huko Dubai, Falme za Kiarabu.

Tutafuatilia mazungumzo na mashauriano hapa COP28  

Watoa mada wanawake kwenye mkutano huo, wamesema watakuwa wanafuatilia kwa karibu maendeleo ya mashauriano kwenye COP28, hasa kuhusu suala la ufadhili wa kipindi sawia cha mpito kuelekea nishati safi na salama, kwa kuondoa nishati chafuzi kwa mazingira na kuanza kutumia nishati safi.  

“Wanawake wanaendelea kuwa kichocheo cha hatua kubwa za tabianchi hivi sasa kuliko wakati wowote ule, ikiwemo kwenye jamii zao, mijini, nchi zao na kanda zao,” amesema Naibu Katibu Mkuu,  

Kulingana n maudhui ya siku hii, matukio yalimulika jinsi wanawake wanaleta majawabu, wanaoko maisha na kulinda mbinu za kujipatia kipato, na baadhi ya majawabu hayo yanachochea mabadiliko chanya maelfu ya kilometa kutoka kwenye ukumbi wa mkutano Dubai.  

Mkurugenzi Mkuu wa UN Women, Sima Bahous amesema “haki za wanawake na wasichana lazima ziwe kitovu cha hatua kwa tabianchi, ikiwemo hapa kwenye COP28. Lazima tuhakikishe wanawake wana kiti kwenye meza ya kupitisha maamuzi. Lazima tuimarishe upitishaji maamuzi jumuishi ili sauti za wanaharakati wa masuala ya wanawake, vijana, watu wa jamii ya asili na vikundi vingine vya vuguvufu mashinani ziweze kusikika kwa sauti zaidi kutoka mashinani hadi ngazi ya kimataifa.”