Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukimwi unapigika, hebu tumalize kazi kwa kuziunga mkono jamii – Katibu Mkuu UN

Phiona anafanya kazi katika kituo cha afya nchini Uganda kama mwanaharaki wa rika ya akina mama, anasaidia kutoa mafunzo na kusaidia akina mama kujifungua watoto wasio na VVU.
© UNICEF/Karin Schermbrucker
Phiona anafanya kazi katika kituo cha afya nchini Uganda kama mwanaharaki wa rika ya akina mama, anasaidia kutoa mafunzo na kusaidia akina mama kujifungua watoto wasio na VVU.

Ukimwi unapigika, hebu tumalize kazi kwa kuziunga mkono jamii – Katibu Mkuu UN

Afya

Vifo vinavyotokana na Ukimwi vimepungua kwa karibu asilimia 70 tangu vilipokuwa katika  kiwango cha juu zaidi mwaka 2004, na maambukizi mapya ya VVU yako katika kiwango cha chini zaidi tangu miaka ya 1980 lakini Ukimwi bado unachukua maisha kila dakika, ndivyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alivyouanza ujumbe wake kwa ajili ya Siku ya Ukimwi Duniani akipigia chepuo ushirikishwaji wa jamii nzima.

“Tunaweza - na lazima - kukomesha UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030. Kufikia lengo hili kunamaanisha kuzingatia Kauli mbiu ya mwaka huu: Achia Jumuiya Ziongoze. Njia ya kukomesha Ukimwi inapitia katika jamii.” Anasema Guterres.

Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa anaeleza kwamba harakati inabidi zihusishe watu wote kuanzia kuwaunganisha watu na matibabu, huduma na usaidizi wanaohitaji - hadi kwa wanaharakati wa mashinani wanaoshinikiza kwa ajili ya hatua ili watu wote waweze kutambua haki yao ya afya.

Anahamasisha kuwaunga mkono walio mstari wa mbele  dhidi ya Ukimwi akisema, “hivyo ndivyo tunavyoshinda.”

Hiyo ina maana kuweka uongozi wa jamii katikati ya mipango, programu, bajeti na ufuatiliaji wa Virusi vya Ukimwi, VVU.

Ufadhili

Aidha Bwana Guterres anasema kwamba ni lazima pia tuondoe vizuizi kwa uongozi wa jamii na kuhakikisha nafasi kwa vikundi vya asasi za kijamii kuendeleza kazi ya muhimu lakini “zaidi ya yote, tunahitaji ufadhili.”

Mapambano dhidi ya Ukimwi katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati yanahitaji zaidi ya dola bilioni 8 zaidi kwa mwaka ili kufadhiliwa kikamilifu.

Hii lazima ijumuishe ufadhili ulioongezwa kwa programu za ndani zinazoongozwa na watu wanaoishi na VVU, na mipango ya kuzuia inayoongozwa na jamii.

Guterres anahitimisha akisema, “Ukimwi unapigika. Tumalizie kazi kwa kusaidia jamii ili kukomesha janga hili katika maeneo yao, nchi zao na kote ulimwenguni.”

Siku ya Ukimwi Duniani huadhimishwa duniani kote tarehe 1 Desemba kila mwaka. Imekuwa mojawapo ya siku za afya za kimataifa zinazotambulika zaidi na fursa muhimu ya kuongeza ufahamu, kuwakumbuka waliofariki, na kusherehekea ushindi, kama vile kuongezeka kwa upatikanaji wa matibabu na huduma za kinga.