Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamii ina mchango mkubwa katika vita dhidi ya UKIMWI:UN 

Utepe mwekundu- ishara ya kimataifa ya kampeni ya kupambana na VVU na ukimwi
Public Health Alliance/Ukraine
Utepe mwekundu- ishara ya kimataifa ya kampeni ya kupambana na VVU na ukimwi

Jamii ina mchango mkubwa katika vita dhidi ya UKIMWI:UN 

Afya

Umoja wa Mataifa umesema jamii ikiwa ni pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali, asasi za kiraia na wanaharakati wana mchango mkubwa katika vita dhidi ya UKIMWI. 

Kupitia ujumbe wake wa siku ya ukimwi duniani Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ili kutokomeza janga la ukimwi ifikapo mwaka 2030 , kama ilivyoahidi kwenye malengo ya maendeleo endelevu kutahijati juhudi endelevu za pamoja.

Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa, serikali, asasi za kiraia na washirika wengine wamekuwa wakifanyakazi kwa pamoja kuongeza kasi ya mchakato wa huduma za afya na kukomesha maambukizi mapya ya VVU.

Na kwa kiasi kikubwa matuda yameanza kuonekana.“Zaidi ya watu milioni 23 wanaoishi na VVU walipatiwa matibabu mwaka 2018.Jamii kote duniani ziko katika kitovu cha hatua hizi, kusaidia watu kudai haki zao, kuchagiza fursa za kupata huduma za jamii na za afya zisizo na unyanyapaa , kuhakikisha kwamba huduma zinawafikia wale wanaozihitaji zaidi na waliotengwa na kushinikiza kubadilisha sheria ambazo zinabagua kama yanavyoainisha mauadhui ya siku ya mwaka huu , jamii zinaleta mabadiliko.”

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema bado kuna mahitaji ambayo hajatimizwa, kuna watu milioni 38 wanaoishi na VVU hivi sasa na rasilimali za kukabiliana na ugonjwa wa ukimwi zilipungua kwa dola bilioni 1 mwaka jana. Sasa kuliko wakati mwingine wowote amesisitiza “tunahitaji kukumbatia jukumu la mashirika yanayoongozwa na jamii ambayo yanapigania wenzao, yanayopeleka huduma za VVU, yanayotetea haki za binadamu na kutoa msaada.” Amesema mahali ambako jamii zimehusishwa mabadiliko yakitokea, uwekezaji ukitoa matokeo na pia  usawa, heshma na utu vimekuwepo.

Winnie Byanyima ambaye ni mkurugenzi mtendaji mpya wa UNAIDS
UN Photo/Amanda Voisard
Winnie Byanyima ambaye ni mkurugenzi mtendaji mpya wa UNAIDS

Akiunga mkono hilo mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana na ukimwi UNAIDS Winnie Byanyima maesema kwa kupitia jamii dunia inaweza kutokomeza ukimwi“Ninaimani na jamii, jamii zinaleta mabadiliko, jamii ndio matumaini yetu makubwa ya kutokomeza ukimwi , kwa sababu jamii zimepambana dhidi ya HIV tangu mwanzo.”

Na amesema bila jamii “Watu milioni 24 wasingekuwa katika matibabu leo hii, bila jamii zinazoongezwa na wanawake wanaoishi au kuathirika na VVU tusingekaribia kukomesha maambukizi mapya miongoni mwa watoto, na kulea yatima pamoja na kuhudumia wagonjwa.”

Hata hivyo amehimiza juhudi zaidi katika vita hivi ikizingatiwa kwa mwaka 2018 watu milioni 1.7 walipata maambukizi mapya ya VVU, watu milioni 37.9 walibainika kuishi na VVU na watu 770,000 walikufa kuttokana na magonjwa ayanayohusiana na ukimwi.