Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maadhimisho yamekuja katika mojawapo ya nyakati za kiza kwa watu wa Palestina

Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina.
© Unsplash/Manny Becerra
Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina.

Maadhimisho yamekuja katika mojawapo ya nyakati za kiza kwa watu wa Palestina

Masuala ya UM

Umoja wa Mataifa leo umeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina, katika nyakati ambazo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameziita mojawapo ya nyakati za kiza katika historia ya watu wa Palestina na hivyo akasisitiza mshikamano zaidi na kutafuta suluhu ya kudumu. 

Bwana Antonio Guterres kupitia ujumbe wake mahususi kwa ajili ya siku hii ya kimataifa ya mshikamano na watu wa Palestina, kwa njia ya maandishi amesema zaidi ya yote yanayoendelea, hii ni siku ya kuthibitisha mshikamano wa kimataifa na watu wa Palestina na haki yao ya kuishi kwa amani na utu. 

Guterres ameendelea kusisitiza suluhisho la Serikali mbili, kwa msingi wa maazimio ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa, ili Israeli na Palestina ziishi kwa pamoja kwa amani na usalama na mji wa Jerusalem uwe mji mkuu wa Mataifa yote mawili. 

“Umoja wa Mataifa hautayumba katika kujitolea kwake kwa watu wa Palestina,” anahitimisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akihimiza kuwa leo na kila siku, ulimwengu usimame katika mshikamano na matarajio ya wananchi wa Palestina kufikia haki zao zisizoweza kupokonywa na kujenga mustakbali wa amani, haki, usalama na utu kwa wote. 

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA, amesema, "Mshikamano wa kimataifa tunaoueleza leo unathibitisha kwamba hitaji la haki za Wakimbizi wa Kipalestina kama ilivyoainishwa katika maazimio ya Umoja wa Mataifa, ni muhimu zaidi sasa kuliko hapo awali." Kwa hiyo anatoa wito kwa ulimwengu kushirikiana kuelekea, “haki na amani kwa Wakimbizi wa Kipalestina, ambao hawahitaji msaada tu, bali suluhisho la haki na la kudumu." 

Baraza Kuu

Pia Rais wa Baraza Kuu Dennis Francis akihutubia katika tukio la maadhimisho hayo lililofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York-Marekani, amesema, "Hakika - miaka sabini na mitano iliyopita - hali ya Mashariki ya Kati iliashiria mgogoro wa kwanza muhimu kwa Umoja wa Mataifa ambao ndio kwanza ulikuwa umeanzishwa."

Ameongeza kuwa, "hali si tu kwamba bado haijatatuliwa, lakini inazidi kuzorota mbele ya macho yetu kwa kasi ya kutisha - huku raia wasio na hatia, haswa wanawake, watoto, na wazee, wakibeba mzigo mkubwa wa ghasia, kunyimwa, na kutokuwa na uhakika.”

Balozi wa Palestina

Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Palestina Mahmoud Abbas, Riyad H. Mansour, Balozi wa Palestina, amesema, "Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na watu wa Palestina, inakuja wakati watu wetu katika Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na tishio la kuwepo. Na kuwalenga kimakusudi na kwa utaratibu raia.”

Ameongeza kuwa, "Tangu tarehe 7 Oktoba, vikosi vya Israel vimefanya uhalifu wa kutisha wa kimataifa ikiwemo uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu."

Maonesho

Pia, leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, maonesho yaliyopewa jina "Palestina - Ardhi yenye Watu" yamefunguliwa kwa wageni. Maonesho hayo yanaadhimisha kumbukumbu ya Nakba ya Palestina (ikimaanisha janga), tukio la kutisha sana ambalo lilifanyika wakati wa vita ya Waarabu na Israeli ya mwaka 1948, wakati zaidi ya nusu ya watu wa Palestina walifukuzwa kutoka, au walikimbia makazi yao na kuwa wakimbizi.

Maadhimisho ya mwaka huu ya Siku hii ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina, kwa Umoja wa Mataifa yamefanyika katika makao makuu jijini New York, Marekani, Geneva Uswisi, Vienna Austria na Nairobi Kenya. 

Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina huadhimishwa na Umoja wa Mataifa kila tarehe 29 Novemba kila mwaka, kwa mujibu wa mamlaka za Baraza Kuu katika maazimio 32/40 B ya 2 Desemba 1977, na 34/65 D ya 12 Desemba 1979 na maazimio yaliyofuata yaliyopitishwa chini ya kipengele cha ajenda "Suala la Palestina." 

Tarehe 29 Novemba ilichaguliwa kwa sababu ya maana na umuhimu wake kwa watu wa Palestina. Siku hiyo ya 1947, Baraza Kuu lilipitisha azimio namba 181 (II), ambalo lilikuja kuitwa Azimio la Kugawanyika. Azimio hilo lilitoa fursa ya kuanzishwa huko Palestina "Nchi ya Kiyahudi" na "Nchi ya Kiarabu", na Jerusalem kama mji mkuu wa pamoja chini ya utawala maalum wa kimataifa. Kati ya Mataifa mawili yaliyopitishwa kuundwa chini ya azimio hili, ni moja tu, Israeli, ambalo limeundwa hadi sasa.