Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tufanye kila tuwezalo kupunguza mateso ya watu wa Palestina-Katibu Mkuu wa UN

Wanafunzi wa wakimbizi wa Palestina katika Shule ya Msingi ya  ya UNRWA Khawla wanafurahi kurudi shuleni baada ya miezi 5 ya mapumziko.
© 2020 UNRWA./Khalil adwan
Wanafunzi wa wakimbizi wa Palestina katika Shule ya Msingi ya ya UNRWA Khawla wanafurahi kurudi shuleni baada ya miezi 5 ya mapumziko.

Tufanye kila tuwezalo kupunguza mateso ya watu wa Palestina-Katibu Mkuu wa UN

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake wa siku ya mshikamano na Wapalestina ametoa wito kwa dunia kujitolea upya kusaidia Wapalestina katika harakati zao za kufikia haki zao na kujenga mustakabali wa amani, utu, haki na usalama. 

Bwana Guterres ameanza ujumbe wake kwa kueleza kuwa wakati Umoja wa Mataifa ukiadhimisha miaka 75 tamgu kuanzishwa kwake, suala la Palestina bado halijatatuliwa.  

Aidha Guterres ameeleza namna ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona ambavyo umeongeza chumvi kwenye kidonda akisema janga la COVID-19 limedhoofisha uchumi wa Palestina na kudhoofisha hali ambayo tayari ilikuwa dhaifu ya kibinadamu, kiuchumi na  hali ya kisiasa huko Gaza, ikharibiwa zaidi na vikwazo vya kutembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine.  

Tweet URL

 

Vilevile Bwana Guterres amesema wakati huo huo, matarajio ya suluhisho linayowezekana la mataifa mawili yanasogea mbali zaidi. Sababu kadhaa zinaendelea kusababisha shida kubwa ikiwemo upanuzi wa makazi haramu, ongezeko kubwa la uvunjaji wa nyumba na majengo ya Wapalestina, vurugu pamoja na kuendelea kwa shughuli za kijesshi. Viongozi wa Israeli na wa Palestina wana jukumu la kutafuta kila namna ya kurejesha matumaini na kufikia suluhisho la mataifa mawili.  

Katibu Mkuu Guterres ameongeza akisema, “ninaendelea na ahadi ya kusaidia wapalestina na waislaeli kusuluhisha mzozo na kumaliza kazi kulingana na maazimio husika ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na makubaliano ya pande mbili katika kutekeleza maono ya Mataifa mawili Israeli na Palestina huru, ya kidemokrasia, jumuishi wakiishi bega kwa bega kwa amani na usalama, ndani ya mipaka salama na inayotambuliwa, kwa msingi wa mipaka ya kabla ya mwaka 1967, na Yerusalemu kama mji mkuu wa Nchi zote mbili.” 

Hata hivyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonesha kuwa pamoja na hayo ana matumaini kuwa maendeleo ya hivi karibuni yatawahamasisha viongozi wa Palestina na Israeli kushiriki tena katika mazungumzo ya maana, kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa, na itatoa fursa za ushirikiano wa kikanda. 

“Lazima pia tufanye kila tuwezalo kupunguza mateso ya watu wa Palestina.” Amesema Bwana Gurettes.  

Kuhusu UNRWA 

Bwana Guterres ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuchangia shirika la Umoja wa Mataifa la kusaidia wakimbizi wa Palestina, UNRWA ili kuliwezesha kufikia mahitaji muhimu ya kibinadamu kwa wakimbizi wa Palestina wakati wa janga la corona.   

“Nina wasiwasi sana na hali ya kifedha inayoikabili UNRWA. Shirika hilo lina jukumu muhimu kama mtoaji mkuu wa msaada wa moja kwa moja na mara nyingi kuokoa maisha kwa wakimbizi milioni 5.7 wa Palestina.” Amesema Guterres.  

Pia Katibu Mkuu Guterres amesema katika Siku hii ya mshikamano na watu wa Palestina pia natoa pole zangu za dhati kuhusu kufariki kwa Dkt Saeb Erakat, Katibu Mkuu wa Shirika la Ukombozi wa Palestina, PLO na Msuluhishi Mkuu wa Wapalestina katika Mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati.