Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapinduzi ya kijeshi Myanmar yamechochea hali mbaya ya haki na kibinadamu: Wataalamu UN

Maelfu ya wakimbizi wa Rohingya wamekimbia Myanmar kuelekea Bangladesh kutokana na ukosefu wa usalama.
© UNICEF/Maria Spiridonova
Maelfu ya wakimbizi wa Rohingya wamekimbia Myanmar kuelekea Bangladesh kutokana na ukosefu wa usalama.

Mapinduzi ya kijeshi Myanmar yamechochea hali mbaya ya haki na kibinadamu: Wataalamu UN

Tabianchi na mazingira

Wataalamu huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo wameonya kwamba mapinduzi ya kijeshi nchini Myanmar siyo tu kwamba yamesababisha mzozo wa haki za binadamu na masuala ya kibinadamu, bali pia yameongeza mazingira magumu ya mabadiliko ya tabianchi kwa watu wa Myanmar.

Wataalam hao wamesema hayo mwanzoni mwa mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP28 unaofanyika katika Muungano wa nchi za Falme za Kiarabu au Emarat.

Wamesisitiza kuwa, "Ni muhimu kwa viongozi wa dunia kusaidia kumaliza mgogoro wa Myanmar kwa kusaidia jamii ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi."

Taarifa yao imeendelea kusema kuwa, "Ukiwa umetengwa zaidi na uchumi wa dunia na kukabiliwa na changamoto ya pesa taslimu, utawala wa kijeshi wa Junta umeongeza kasi ya unyonyaji wa maliasili za Myanmar, pamoja na mbao, madini adimu  ya jade na  kufadhili ukiukaji wake wa haki za binadamu. Kuongezeka kwa uchimbaji wa rasilimali, mara nyingi bila kudhibitiwa na kuwezeshwa na wanajeshi au vikundi vingine vyenye silaha, kunaharibu mazingira, kuchafua vyanzo vya maji, kuharibu misitu, na kuzidisha hatari za mabadiliko ya tabianchi.”

Hatarini kwa mabadiliko ya tabianchi

Pia wataalam hao wamesema "Athari za migogoro inayoingiliana na masuala ya mabadiliko ya tabianchi tayari zinatishia afya, maisha na usalama wa mamilioni ya watu nchini Myanmar, hasa watu wa jamii za asili, ambao maisha yao yanategemeana na asili na ambao wamehudumu kama walinzi wa mazingira kwa karne nyingi."

Myanmar, ambayo ni nyumbani kwa utajiri wa maliasili na mifumo mbalimbali ya kiikolojia, tayari ilikuwa moja ya nchi zilizo hatarini zaidi kwa mabadiliko ya tabianchi wakati serikali ya kijeshi ilipofanya mapinduzi haramu na kuiingiza nchi hiyo katika mzozo mkali hapo Februari 2021.

"Kwa zaidi ya miaka miwili utawala wa kijeshi wa Junta umewashikilia watu wa Myanmar, ukianzisha mashambulizi ya kiholela ambayo yamezilazimisha jamii kuhama kwa kiwango kikubwa na kupunguza uwezo wa wenyeji kuchukua hatua na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. “

Wataalam hao wamesema wanaharakati wengi wa mazingira wamekimbilia uhamishoni au kuelekeza mtazamo wao kwa kukabiliana na mgogoro.

Jamii zinaishi siku hadi siku, jambo ambalo linazuia uwezo wao wa kufuata mazoea ya kustahimili mabadiliko ya tabianchi.

Maendeleo yaliyopatikana kuelekea mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika miaka kabla ya mapinduzi yamekwama au kubadilishwa wataalam hao wamesema.

Jumuiya ya kimataifa izisaidie jamii

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed akihutubia mkutano wa maandalizi kabla ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi (COP28) utakaofanyika Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.
UN/Zumrad Normatova

Wataalam hao wameitaka jumuiya ya kimataifa kuunga mkono jamii na mashirika ya ndani kupitia ufadhili unaobadilika kwa ajili ya mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kukabiliana na kuepuka ushirikiano rasmi na utawala wa kijeshi wa Junta ambayo haina uwezo au nia ya kutekeleza sera madhubuti za mazingira na itatumia ushirikiano rasmi kwa madhumuni ya propaganda.

Kwa mujibu wa wataalam hao wa Umoja wa Mataifa, "Baadhi ya taasisi zinazounga mkono demokrasia na upinzani nchini Myanmar zinaendeleza kikamilifu sera za mabadiliko ya tabianchi na maliasili, na vikundi vingi vyenye ujasiri vya mazingira vinaendelea kutetea misitu ya Myanmar, wanyamapori na bayoanuwai. Ni lazima tuunge mkono juhudi hizo.”

Wameongeza kuwa, "Myanmar haijajitayarisha sana kukabiliana na athari zinazokaribia haraka za mabadiliko ya tabianchi. Athari mbaya za Kimbunga Mocha, ambacho kilitua kaskazini-magharibi mwa Myanmar Mei 2023, na kufuatiwa na kikwazo cha aibu cha Junta katika utoaji wa misaada kwa jamii zilizoathiriwa na kimbunga, imekuwa ni ukumbusho wa giza wa matokeo ya kushindwa kwa ulimwengu kushughulikia mabadiliko ya tabianchi Myanmar, ukandamizaji wa kijeshi na ukiukaji wa haki za binadamu.”