Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

HABARI KWA UFUPI: 21 NOVEMBA 2023

Watoto wakihahamishwa kutoka hospitali ya Al-Shifa huko Kaskazini mwa Gaza kuelekea eneo la Kusini mwa ukanda huo wa Gaza huko Mashariki ya Kati kutokana na mapigano  yanayoendelea hivi sasa kati ya Israel na wapiganaji wa kipalestina wa Hamas
© UNICEF/Eyad El Baba
Watoto wakihahamishwa kutoka hospitali ya Al-Shifa huko Kaskazini mwa Gaza kuelekea eneo la Kusini mwa ukanda huo wa Gaza huko Mashariki ya Kati kutokana na mapigano yanayoendelea hivi sasa kati ya Israel na wapiganaji wa kipalestina wa Hamas

HABARI KWA UFUPI: 21 NOVEMBA 2023

Amani na Usalama

Siku ya 45  ya mapigano huko Ukanda wa Gaza tunakupatia kwa ufupi yanayoendelea hii leo na kile ambacho mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasema.

WHO

Tunaanzia Ukanda wa Gaza, Mashariki ya Kati ambako mapigano yakiendelea hii leo ikiwa ni siku ya 45 tangu kuanza kwa mzozo eneo hilo kati ya Israeli na wanamgambo wa kipalestina wa Hamas, shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO linasema kila siku watoto takribani 160 wanauawa, ikimaanisha mtoto mmoja kila baada ya dakika 10. WHO inasema wakati huo huo watoto 180 wanazaliwa kila siku eneo hilo na zaidi ya 20 wanahitaji huduma mahsusi ambazo kwa sasa ni changamoto kubwa.

UNICEF

Tukisalia Gaza, msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF James Elder akizungumza na waandishi wa  habari huko Geneva, Uswisi hii leo amesema ukosefu wa maji kwenye eneo hilo  unatishia usalama wa watoto. Amegusia pia mateka watoto wanaoshikiliwa na Hamas akisema,… “lazima waachiliwe huru. Inachukiza kufikiria kuhusu hofu yao; machungu ya familia zao. Hii lazima ikome.”

COP28

Na kuelekea mkutano wa mabadiliko ya tabianchi huko Falme za kiarabu mwishoni mwa mwezi huu, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaesma wanawake wajawazito, watoto wachanga na watoto wanakabiliwa na hatari kubwa za kiafya kutokana na majanga ya mabadiliko tabianchi hivyo hatua za kukabili tabianchi zisiwaengue.

MWISHO WA HABARI KWA UFUPI