Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yazindua kampeni “ACHA UWONGO” dhidi ya sekta ya tumbaku

WHO inasema sekta ya tumbaku inaendelea kudanganya umma.
Unsplash/Reza Mehrad
WHO inasema sekta ya tumbaku inaendelea kudanganya umma.

WHO yazindua kampeni “ACHA UWONGO” dhidi ya sekta ya tumbaku

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni WHO, leo limezindua rasmi kampeni ya "Acha uwongo" ikiwa ni hatua muhimu ya kuwalinda vijana dhidi ya sekta ya tumbaku na bidhaa zao. 

Taarifa iliyochapishhwa hii leo kwenye ukurasa wa WHO inasema lengo la kampeni hiyo ni kupaza sauti za vijana, kufichua mbinu za sekta ya tumbaku na kuongeza uelewa wa umma juu ya haja ya kutetea sera za afya na kulinda afya ya vizazi vijavyo.

Mkurugenzi wa kukuza afya wa WHO Dkt. Ruediger Krech ameeleza kuwa “WHO inasimama pamoja na vijana ulimwenguni kote ambao wamedai serikali kuwalinda dhidi ya tasnia hatari ambayo inawalenga na bidhaa zenye madhara huku wakidanganya waziwazi athari za kiafya.”

Shirika hilo limeeleza kuwa sekta ya tumbaku ina historia ndefu ya kusema uwongo kwa umma, hata kufikia kusisitiza kwamba uvutaji sigara hausababishi saratani ya mapafu.

Dkt Krech ametoa wito kwa nchi zote “kulinda sera za afya kutokana na sekta hii hatari kwa kutoziruhusu kuwa na kiti katika meza ya kutunga sera” 

Kampeni hii inaungwa mkono na ushahidi mpya kutoka kwenye ripoti ya “The Global Tobacco Industry Interference Index 2023” ambayo inaonesha kuwa juhudi za kulinda sera ya afya dhidi ya kuingiliwa kwa sekta ya tumbaku zimedorora kote ulimwenguni. 

Acha uwongo

Sekta ya tumbaku imeelezwa kuendelea kutumia njia tofauti kueneza habari potofu, ikijumuisha kupitia watu maarufu katika mitandao ya kijamii, kufadhili matukio, na hata kufadhili wanasayansi na utafiti wenye upendeleo. 

Taarifa za mpaka sasa zinaonesha tumbaku inasababisha asilimia 25 ya saratani zote na kuua zaidi ya watu milioni 8 kila mwaka, lakini sekta hiyo inaendelea na uuzaji wa bidhaa wanazoziita 'mpya' na 'salama' ambazo zinajulikana zina madhara kiafya, huku zikiendelea kuzalisha matrilioni ya sigara kila mwaka.

WHO imesema sekta ya tumbaku inawekeza kiasi kikubwa cha pesa katika kushawishi umma dhidi ya sera za kudhibiti tumbaku na kufadhili mashirika ambayo yanaendeleza maslahi yake.

Shirika hilo limeeleza mbinu hizo za tumbaku, zikiachwa bila kudhibitiwa, huleta madhara yasiyopimika kwa afya ya umma. Zaidi ya hayo, utengenezaji na utumiaji wa bidhaa za tumbaku na nikotini una athari mbaya kwa masuala mengine muhimu kama vile mazingira, afya ya akili na ajira ya watoto.