WHO yazindua kampeni ya mwaka mzima kusaidia watu milioni 100 kuacha tumbaku
WHO yazindua kampeni ya mwaka mzima kusaidia watu milioni 100 kuacha tumbaku
WHO leo imezindua kampeni ya mwaka mzima kwa jina "Jitolee kuacha kuvuta." kwa ajili ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kutovuta tumbaku kwa mwaka ujao wa 2021.
Changamoto mpya ya WHO ikifahamika kama “Quit Challenge” kwa maana ya changamoto ya kuacha kuvuta tumbaku inazinduliwa leo katika mtandao wa WhatsApp, huku chapisho kwa jina “zaidi ya sababu 100 za kuacha tumbaku” nalo likizinduliwa, yote haya yakiwa yanaashiria kuanza kwa kampeni hiyo.
Taarifa ya WHO iliyotolewa hii leo mjini Geneva Uswisi imeeleza kuwa janga la coronavirus">COVID-19 limesababisha mamilioni ya watumiaji wa tumbaku kusema wanataka kuacha. Kampeni hiyo itasaidia watu wasiopungua milioni 100 wanapojaribu kujitoa katika matumizi ya tumbaku.
"Jitolee kuacha" itasaidia kuunda mazingira yenye afya ambayo yanafaa kuacha tumbaku kwa kutetea sera kali za kukomesha tumbaku, kuongeza upatikanaji wa huduma za kukomesha, kuongeza uelewa juu ya mbinu za tasnia ya tumbaku, na kuwawezesha watumiaji wa tumbaku kufanya majaribio ya kuacha yenye mafanikio kupitia mipango ya "kuacha na kushinda".
WHO, pamoja na wadau, itaunda na kujenga jamii za kidijitali ambapo watu wanaweza kupata msaada wa kijamii wanaohitaji kuacha. Mtazamo utazingatia nchi zenye mzigo mkubwa, ambako watumiaji wengi wa tumbaku ulimwenguni wanaishi. Nchi zilizotajwa ni Timor-Leste, Ethiopia, Ujerumani, Nigeria, Brazil, Jordan, Iran, Pakistan, Bangladesh, China, India, Indonesia, Ufilipino, Poland, Afrika Kusini, Suriname, Uturuki, Urusi, Viet Nam, Mexico, Marekani na Ukrane.
WHO imekaribisha michango mipya kutoka kwa washirika, pamoja na kampuni za sekta binafsi ambazo zimetoa msaada, zikiwemo Easyway ya Allen Carr, Huduma za Wavuti za Amazon, Cipla, Facebook na WhatsApp, Google, Johnson & Johnson, Praekelt, na Soul Machines.
Kuacha tumbaku ni changamoto, hasa na misongo ya kijamii na kiuchumi ambayo imetokana na janga la COVID-19. Ulimwenguni kote karibia watu milioni 780 wanasema wanataka kuacha matumizi ya tumbaku, lakini ni asilimia 30 tu yao ndio wanapata zana ambazo zinaweza kuwasaidia kufanya hivyo. WHO pamoja na wadau, itawapa watu zana na rasilimali wanazohitaji ili kufanikisha jaribio la kuacha tumbaku.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus anasema, "uvutaji sigara unaua watu milioni 8 kwa mwaka, lakini ikiwa watumiaji wanahitaji msukumo zaidi wa kukomesha tabia hiyo, janga la COVID-19 linatoa motisha inayofaa."
WHO ilitoa muhtasari wa kisayansi mapema mwaka huu unaoonesha kuwa wavutaji sigara wako katika hatari kubwa ya kupata magonjwa makali na kifo kutoka kwa COVID-19. Tumbaku pia ni hatari kubwa kwa magonjwa yasiyoweza kuambukizwa kama ugonjwa wa moyo na mishipa, saratani, ugonjwa wa kupumua na ugonjwa wa sukari. Kwa kuongezea, watu wanaoishi na hali hizi wana hatari zaidi ya COVID-19 kali zaidi.