Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Cuba: Baraza Kuu kwa mara ya 31 laitaka Marekani kuondoa vikwazo

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepigia kura juu ya umuhimu wa kukomesha vikwazo vya kiuchumi, kibiashara na kifedha vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Cuba.
UN Photo/Evan Schneider
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepigia kura juu ya umuhimu wa kukomesha vikwazo vya kiuchumi, kibiashara na kifedha vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Cuba.

Cuba: Baraza Kuu kwa mara ya 31 laitaka Marekani kuondoa vikwazo

Masuala ya UM

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo Alhamisi limepiga kura kwa asilimia kubwa kupinga vikwazo vya kiuchumi na kibiashara vya Marekani dhidi ya Cuba, vilivyowekwa kwa mara ya kwanza mwaka 1960.

Azimio hilo limeungwa mkono na mataifa 187 lakini mataifa mawili Marekani na Israel yakapiga kura ya kupinga, huku Ukraine haikupiga kura.

Tweet URL

Kwa miaka 31 mfululizo Baraza Kuu limekuwa likitaka kuondolewa kwa vikwazo hivyo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Cuba. Mnamo mwaka 1992, azimio liliungwa mkono na nchi 59, mwaka 2017 nchi 191, mwaka jana 2022 nchi 185, na mwaka huu wa 2023 nchi 187. Mnamo mwaka 2016, Marekani haikupiga kura "ya kupinga" lakini haikupiga kura yoyote na vikwazo vikaendelea.

Katika kuelezea uamuzi wao wa aina ya kura zao, wazungumzaji wengi katika kikao cha Baraza, mmoja baada ya mwingine, wamesisitiza kuhusu uharamu wa vikwazo dhidi ya Cuba, wakitangaza kwamba ni ukiukaji wa wazi na ulioratibiwa dhidi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Aidha wajumbe wamezungumza kuhusu uharibifu unaofanywa na vikwazo kwa watu wa Cuba, na kuwanyima mapato ya kimsingi na mahitaji ya kimsingi, zikiwemo dawa.