Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tume za kiuchumi za UN ni matanuru ya fikra

Katibu Mkuu Antonio Guterres akutana na wafanyakazi katika sekta ya ujenzi huko Havana, Cuba.
ECLAC
Katibu Mkuu Antonio Guterres akutana na wafanyakazi katika sekta ya ujenzi huko Havana, Cuba.

Tume za kiuchumi za UN ni matanuru ya fikra

Ukuaji wa Kiuchumi

Umoja wa Mataifa umetaka nchi wanachama zitumie vyema mafaniko yanayoibuka na kile kinachoitwa mapinduzi ya nne ya viwanda duniani.

Katibu Mkuu Antonio Guterres amesema hayo leo huko Havana, Cuba wakati akihutubia kikao cha 37 cha tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa nchi za Amerika ya Kusini na Karibea, ECLAC.

Amesema dunia inazidi kugawanyika, maendeleo yakiwa hayamfikii kila mtu hivyo ni vyema kuwa na ainisho jipya la neno maendeleo.

Bwana Guterres amesema hatua hiyo ni muhimu zaidi kwa nchi zilizo katika mpito wa maendeleo na pia za kipato cha kati ikiwemo zile za Amerika ya Kusini na Karibea.

Amesema kinachohitajika ni mfumo wa kiuchumi duniani ambao unanufaisha watu wote, na kuweka fursa  kwa wote bila ubaguzi.

Kuhusu umuhimu wa tume hizo za uchumi za kikanda za Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu amesema zinapaswa kutambuliwa kuwa matanuru ya fikra ya Umoja wa Mataifa kwa maeneo husika.

Amepongeza ECLAC kwa jinsi ambavyo imeweza kuchochea ushiriki wa nchi wanachama katika kusongesha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs akisema ni kwa ushirikishaji huo, Hakuna mtu yeyote atakayeachwa nyuma.