Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanachama 189 waridhia vikwazo dhidi ya Cuba viondolewe, Marekani na Israel zapinga

Matokeo ya kura katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa yakiwa yanaonekana kwenye ubao wa kielektroniki ikiwa ni tarehe 01 Novemba 2018
UN / Evan Schneider
Matokeo ya kura katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa yakiwa yanaonekana kwenye ubao wa kielektroniki ikiwa ni tarehe 01 Novemba 2018

Wanachama 189 waridhia vikwazo dhidi ya Cuba viondolewe, Marekani na Israel zapinga

Ukuaji wa Kiuchumi

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena wamepitisha kwa kishindo azimio linalosisitiza umuhimu wa kumaliza vikwazo vya kiuchumi, kibiashara na kifedha vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Cuba.

Matokeo ya kura yalitangazwa na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Maria Fernanda Espinosa ambapo wajumbe 189 waliunga mkono ilhali nchi mbili ambazo ni Marekani na Israel zilipiga kura  ya hapana na hakuna nchi yeyote iliyojiengua kwenye upigaji kura.

Kupitia azimio hilo namba A/73/L.3 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linarejelea wito  kwa nchi wanachama kujiepusha na kueneza na kutumia sheria ambazo ni kinyume na katiba iliyoanzisha Umoja wa Mataifa mwaka 1945.

Miongoni mwa vipengele hivyo ni kile cha sheria ya kimataifa inayosisitiza uhuru wa kufanya biashara ambapo azimio linataka nchi zinazoendelea kutekeleza vikwazo vya aina hiyo viachane navyo mara moja.

Wakati wa mkutano wajumbe walipokea ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu utekelezaji wa azimio namba A72/4 la umuhimu wa kuondoa vikwazo vya kiuchumi, kibiashara na kifedha vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Cuba.

Ripoti hiyo pamoja na mambo mengine ina ripoti za nchi wanachama zikitoa maoni yao kuhusu vikwazo hivyo ambapo Kenya imesema itaendelea kupinga vikwazo hivyo dhidi ya Cuba, halikadhalika Tanzania na Uganda ambayo imesema vikwazo hivyo havijaleta manufaa yoyote zaidi ya madhila dhidi ya wananchi wa Cuba.

Wajumbe hii leo wakati wa kikao kabla ya kupiga kura walitoa msimamo wa kura ambayo watapiga,  Zambia ambayo nayo imeunga mkono azimio hilo, kupitia mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Lazarous Kapambwe imesema, "Ukuu haupo katika uwezo wa kudhibiti, lakini katika uwezo wa kunyanyua na kutia moyo. Ukuu haupo katika uwezo wa kuharibu, bali katika uwezo wa kukarabati na kujenga. Ukuu haupo  katika kujinufaisha na mamlaka, bali katika kutumia mamlaka kulinda wadogo na dhaifu na kuwezesha wasiojiweza.”

Mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Nikki Hailey akazungumza akisema, "“Wale wanaounga mkono azimio hili kila mwaka wanakosea. Sababu ya vikwazo vyetu ni kwamba Cuba imekuwa ikiwanyima . Marekani itaendelea kushikamana na wananchi wa Cuba hadi pale haki zao na uhuru wao vitakaporejeshwa, nukta. Katu hatutorudi nyuma.”

Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Bruno Rodríguez Parrilla akihutubia kabla ya upigaji kura amesema, serikali  ya Marekani haina hata mamlaka ya kimaadili ya kukosoa Cuba au mtu yeyote yule kwenye suala la  haki za binadamu. Tunakataa ulaghai unaorejelewa mara kwa mara wa haki hizi kwa maslahi ya kisiasa na upendeleo ambao mara kwa mara wanatumia.”