Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji ya waandishi wa habari hufanyika kwenye nchi zenye amani- UN

Waandishi wa habari nchini Somalia wakihudhuria mkutano.
UN Photo/Fardosa Hussein
Waandishi wa habari nchini Somalia wakihudhuria mkutano.

Mauaji ya waandishi wa habari hufanyika kwenye nchi zenye amani- UN

Sheria na Kuzuia Uhalifu
  • Jukumu la waandishi wahabari kufichua ukweli mashakani 
  • Wanalengwa hasa kwenye nchi zenye amani kwa kusema ukweli 
  • Nchi ziweke mifumo ya wanaowashambulia wasikwepe sheria 

Nafasi adhimu ya wanahabari kutumia tasnia yao kuwezesha demokrasia na kuwajibisha mamlaka iko hatarini kwa sababu kujitolea kwao kuchunguza na kufichua ukweli huwatumbukiza kwenye kulengwa, kushambuliwa, kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria na hata kuuawa.  

Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake hii leo ambayo ni siku ya kimataifa ya kupinga ukwepaji sheria dhidi ya vitendo vya uhalifu wanavyofanyiwa waandishi wa habari.  

Akithibitisha hatari zinazokumba waandishi wa habari, Guterres amenukuu shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO ambalo linasema mwaka 2022 pekee, waandishi wa habari 88 waliuawa kwa kufanya kazi zao, idadi ambayo ni ongezeko kubwa kulinganisha na miaka iliyopita.   

“Mzozo wa sasa wa Israeli na wanamgambo wa kipalestina wa Hamas, kwenye eneo linalokaliwa la Palestina linaongeza vifo vya waandishi wa habari,” amesema Guterres.   

Cha ajabu wanaouawa wako kwenye nchi zenye amani 

Lakini cha ajabu, kwa mujibu wa Guterres idadi kubwa ya waandishi wa habari wanaouawa sio wale wanaohusika na uandishi wa habari za vita.  

Badala yake wanafanya kazi katika nchi ambazo zina amani, kuchunguza ufisadi, biashara haramu ya binadamu, ukiukaji wa haki za binadamu na masuala ya mazingira.   

“Nimesikitishwa sana na takwimu hizi, na kuongezeka kwa vitisho vya kila aina dhidi ya waandishi wa habari. Kuswekwa ndani kwa waandishi wa habari kumeongezeka sana. Waandishi wa habari kunyanyaswa mtandaoni, hasa wanawake, kunatumiwa kama nyenzo ya kuwanyamazisha. Tunahitaji ulinzi bora zaidi ili kuwatetea waandishi wa habari wanaotuhabarisha,” amesema Guterres.   

Ametaka mataifa kutumia siku ya leo  kuzuia ukatili dhidi ya waandishi wa habari, “kuwawekea mazingira salama ya kufanya kazi zao, kuwafikisha mahakamani wale wanaofanya uhalifu dhidi ya waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari na kuhakikisha msaada kwa waathiriwa na walionusurika.”    

Kwa kumalizia Bw. Guterres amesema kuwa, “leo na kila siku, tunawashukuru wanahabari na wanataaluma wote wa vyombo vya habari wanaohatarisha afya na maisha yao ili kutuhabarisha, na kuweka ukweli hai.  

Je wajua?  

  • Mwaka 2020-2021 Waandishi wa habari waliouawa ni 117 

  • Amerika ya Kusini na Karibea 38%  

  • Asia na Pasifiki 32% 

  • Idadi ya wanawake wanahabari waliouawa 2021 iliongezeka maradufu kulinganisha na kipindi kilichotangulia. 

  • Kesi za kuuawa kwa wanahabari zilizofikishwa mahamani ni %14 pekee.