Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kunyamazia aina yoyote ya chuki ni ishara ya ushirika – Guterres

Kambi ya maangamizi ya Auschwitz-Birkenau kusini mwa Poland
Unsplash/Jean Carlo Emer
Kambi ya maangamizi ya Auschwitz-Birkenau kusini mwa Poland

Kunyamazia aina yoyote ya chuki ni ishara ya ushirika – Guterres

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hii leo “tunakumbuka wayahudi milioni 6, wanaume, wanawake na watoto walioteketea katika mauaji ya maangamizi au Holocaust, pamoja na waroma na wasinti na wengine wengi ambao walikuwa waathirika wa kisanga hicho cha kutisha na ukatili uliopangwa.”

Katika ujumbe wake huo alioutoa kwa njia ya video kwenye kumbukizi iliyofanyika jijini New York, Marekani, Bwana Guterres amesema mauaji ya maangamizi yanaainisha Umoja wa Mataifa kwa kuwa jina lenyewe la chombo hicho kilichoundwa mwaka 1945, limelenga kuelezea ushirika wa kukabili utawala wa manazi na washirika wao.

Amesema Chata ya Umoja wa Mataifa ilitungwa mjini San Francisco wakati kambi ya maangamizi ya Dachau ilipokombolewa kwa hivyo, “Umoja wa Mataifa ni lazima kila wakati uwe mstari wa mbele kupambana na chuki dhidi ya wayahudi na aina nyingine zote za ubaguzi wa kidini na wa rangi.”

Chuki dhidi ya wayahudi inaongezeka kila uchao

Amesema leo hii dunia inashuhudia kuibuka kwa kutisha kwa chuki ikiwemo chuki dhidi ya wageni na kwamba chuki dhidi ya wayahudi – ubaguzi wa kale zaidi na ulioota mizizi – unaanza kuibuka tena.

Na kinachosikitisha zaidi, “majaribio ya kupuuza au kupotosha uwepo wa mauaji ya maangamizi dhidi ya wayahudi yanaendelea.”

Viatu vya wafungwa walioangamizwa katika kambi ya maangamizi ya Auschwitz nchini Poland
Unsplash/William Warby
Viatu vya wafungwa walioangamizwa katika kambi ya maangamizi ya Auschwitz nchini Poland

Guterres amesema hakuna jamii iliyo na kinga dhidi ya ukosefu wa mantiki na stahmala.

“Katu hatupaswi kusahau kuwa mauaji ya maangamizi yangaliweza kuepukika. Vilio vya waathirika vilitumbukia kwenye masikio yasiyosikia. Watu wachache sana walizungumza, wachache sana walisikilizwa – wachache zaidi walisimama kidete kwa mshikamano.”

Katibu Mkuu amesema kukumbuka yaliyopita ni muhimu katika kulinda mustakabali na kwamba ukimya mbele ya chuki ni ishara ya ushirika na ametamatisha ujumbe wake akisema, “leo hii hebu na tuazimie katu hatutakuwa kimya kwenye machungu ya wengine, na katu hatutosahau kile kilichotokea, au tuache wengine wasahau. Hebu na tuahidi kila wakati kuwa macho na kuheshimu haki za binadamu na utu wa kila mtu.”