Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mtu ana nafasi yake kusongesha Umoja wa Mataifa - Guterres

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakifanya doria ya usiku huko Bentiu, Sudan Kusini.
UNMISS/Gregório Cunha
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakifanya doria ya usiku huko Bentiu, Sudan Kusini.

Kila mtu ana nafasi yake kusongesha Umoja wa Mataifa - Guterres

Masuala ya UM

Miaka 78 ya Umoja wa Mataifa, bado kila mkazi wa dunia hii ana nafasi ya kusongesha malengo ya kuanzishwa kwa Umoja huo huko San Francisco, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake hii leo ambayo ni maadhimisho ya siku ya UN kukumbuka siku Chata ya chombo hicho alianza kutumika. 

Katibu Mkuu amesema  Umoja wa Mataifa ni taswira ya ulimwengu na jinsi ulivyo na matarajio ya ulimwengu ambao kila mkazi wa dunia anajua unaweza kuwa. “Ni wajibu wetu kusaidia kujenga ule ulimwengu wa amani, maendeleo endelevu na haki za binadamu kwa wote.” 

Malengo ya kuanzishwa kwa UN 1945 

Malengo ya Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa Chata iliyouanzisha ni manne: Mosi; kuendeleza amani na usalama duniani, Pili; kusongesha uhusiano wa kirafiki baina ya nchi, Tatu; kufanikisha ushirikiano wa kimataifa na Nne; kuwa kitovu cha kuratibu vitendo vya mataifa. 

Bwana Guterres anasema kila mkazi wa dunia ana uwezo wa kusongesha malengo hayo akisema Chata ya Umoja wa Mataifa  iliyoanza kutumika miaka 78 iliyopita, siku kama ya leo inaonesha njia. Zaidi ya yote, imejikita kwenye mizizi ya azma ya kuondoa migawanyiko, kurekebisha uhusiano, na kujenga amani,” akisistiza kuwa mshikamano huo utaongeza fursa ya maendeleo, kutomwacha nyuma mtu yeyote. Vile vile kuhakikisha haki kwa wote, usawa na uwezeshaji wa wanawake na wasichana. 

Halikadhalika kutoa misaada ya kuokoa maisha kwa wale wanaoihitaji, na kushughulikia changamoto ambazo hazikuwepo wakati UN ilianzishwa, kuanzia athari ya mabadiliko ya tabianchi hadi hatari na ahadi ya Akili Mnemba au (AI) 

Maadili ya UN hayapitwi na wakati lakini UN lazima iende na wakati 

Guterres amekumbusha kuwa “Umoja wa Mataifa unaongozwa na maadili na kanuni zisizomalizika wakati, lakini kamwe haupaswi kutoenda na wakati. Ndio maana lazima kila wakati tuendelee kuimarisha njia za kufanya kazi na kutumia lensi ya karne ya 21 kwa yoyote tunayofanya”. 

Ametamatisha ujumbe wake akisema “katika siku hii ya Umoja wa Mataifa hebu na tutoe ahadi tukiwa na matumaini na azma ya kujenga dunia bora ya matarajio yetu. Sisi ni dunia iligawanyika lakini lazima tuwe Umoja wa Mataifa.” 

Mzozo nchini Sudan umewakosesha makazi maelfu ya watoto na familia zao.
© UNICEF/Ahmed Elfatih Mohamdee
Mzozo nchini Sudan umewakosesha makazi maelfu ya watoto na familia zao.

Tunaadhimisha siku hii Sudan wakati mgogoro wa kibinadamu unakuwa kwa kasi 

Katika ujumbe wake wa siku hii Clementine Nkweta-Salami Naibu mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan na kaimu mratibu mkazi na wa masuala ya kibinadamu amesema, “Mwaka huu tunaadhimisha siku hii wakati Sudan ikikabiliwa na moja ya mgogoro  wa kibinadamu unaokuwa kwa kasi ukiambatana na mahitaji makubwa. Mapigano yamegeuza mgogoro huo kuwa janga kubwa. Zaidi ya watu milioni 5.6 wamefurushwa makwao, milioni 25 wanahitaji msaada, zaidi ya wanawake na wasichana milioni 4.2 wako katika hatari ya ukajtili wa kijinsia na mtoto 1 kati ya 3 hana fursa ya kwenda shule.