Asanteni Umoja wa Mataifa mmetunusuru- Wanufaika wa miradi ya  UN

Wanufaika wa miradi inayotekelezwa na FAO nchini Somalia
©FAO/Arete/Ismail Taxta
Wanufaika wa miradi inayotekelezwa na FAO nchini Somalia

Asanteni Umoja wa Mataifa mmetunusuru- Wanufaika wa miradi ya  UN

Masuala ya UM

Kuelekea maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa tarehe 24 mwezi huu wa Oktoba, wanufaika wa miradi ya chombo hicho mashinani wamepaza sauti zao kutoa shukrani kwa jinsi maisha yao yamebadilika kutokana na miradi inayotekelezwa kupitia mashirika ya Umoja wa Mataifa.
 

Tukianzia na Pembe ya Afrika hususan nchini Somalia, tunamulika ufugaji ambako Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la chakula na kilimo, FAO limepatia wakulima, wafugaji na wavuvi msaada wa fedha na mafunzo ili kupata pembejeo bora za kuimairisha njia zao za kujipatia kipato. Safiya Mahdi Cise ni mkulima mfugaji. 
Bi. Cise anasema,“tumeona mabadiliko makubwa katika mifugo yetu hususan kiwango cha maziwa tunayokamua sasa ni mengi. Tunashukuru sana FAO. Mradi huu hakika unasaidia kukimu mahitaji yetu. Ikiwemo afya ya mifugo yetu na watoto wetu.” 

Safiya Mahdi Cise, mnufaika wa mradi wa FAO wa kuboresha ufugaji akiwa amembeba ndama wa kondoo huko kijiji cha  Duudwayne, wilaya ya Baki nchini Somalia
© FAO / Isak Amin / Arete
Safiya Mahdi Cise, mnufaika wa mradi wa FAO wa kuboresha ufugaji akiwa amembeba ndama wa kondoo huko kijiji cha Duudwayne, wilaya ya Baki nchini Somalia

Mfugaji BAshir Xasan Muse naye mnufaika wa zaidi ya watu milioni 1 nchini Somalia waliopatiwa fedha na FAO kupitia mradi huo akafunguka zaidi, “mradi umeimarisha maisha ya watu wengi ikiwemo kwa chakula na dawa. Umepunguza athari zitokanazo na janga la Corona au COVID-19 pamoja na baa la nzige.  na kimatibabu.  

Natumai mbegu tulizopatiwa zitaokoa maisha yangu na familia yangu-Mkulima Somalia

Ali Mahmud Rubaax ni mkulima aliyepatiwa pembejeo ikiwemo mbegu, akiwa shambani akipanda mbegu hakusita kuelezea shukrani zake kwa Umoja wa Mataifa akisema, “msaada ambao FAO imetupatia ulikuwa muhimu sana kwa sababu maisha yetu yanategemea ardhi. Hatukuweza kununua mbegu wala kulipa wafanyakazi tuliokuwa tumeajiri kwa sababu nzige waliharibu mashamba. Natumai mbegu hizo ninazopanda sasa zitaimarisha maisha ya baadaye ya kwangu na familia yangu.” 

Kutoka pembe ya Afrika tunafunga safari hadi kusini mwa Afrika hususan nchini Zambia ambako Umoja wa Mataifa  kupitia shirika lake la kuhudumia watoto duniani, UNICEF nchini humo pamoja na wadau wananusuru watoto wa kike waliocha shule kwa sababu mbalimbali ili waweze kurejea shuleni na kupata haki yao ya msingi ya elimu. Miongoni mwao ni Jelina Mbewe. 

Jelina Mbewe ni miongoni mwa wasichana walionasuliwa kutoka ndoa za umri mdogo kutokana na mradi wa UNICEF na YWCA wa kuelimisha wasichana kuondokana na madhila hayo na badala yake kwenda shuleni.
UNICEF VIDEO
Jelina Mbewe ni miongoni mwa wasichana walionasuliwa kutoka ndoa za umri mdogo kutokana na mradi wa UNICEF na YWCA wa kuelimisha wasichana kuondokana na madhila hayo na badala yake kwenda shuleni.

Jelina arejea shuleni, asante UNICEF na wadau

“Niliacha shule nikiwa darasa la 8 kwa sababu nilkuwa sifaulu chochote. Kutokana na ushawishi wa  marafiki nikaacha kwenda shule. 
Wazazi wake waliona wasipoteza fedha wakaamua Jelina aolewe lakini mradi wa UNICEF na mdau wake YWCA ukawa mkombozi. Jelina anasema, “shirika la YWCA lilikuja na baada ya kushiriki mikutano yao nilijifunza mambo mengi ikiwemo kukomesha ndoa za umri mdogo.” YWCA walizungmza na mzazi wa Jelina nao wakakubali arejee shuleni. 

Ni kwa mantiki hiyo Jelina anasema, “sasa nimerejea shule, na nimefauli mitihani ya darasa la 9. Nimejitahidi sana na sasa Niko darasa la 11. Ninafurahi sana sasa nina ufahamu na hata kama nitakamilisha mafunzo ya YWCA nitafundisha wengine nilichofundishwa kwa sababu kimebadili maisha  yangu. ”