Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maadili yaliyoanzisha Umoja wa Mataifa hayana muda wa kumalizika

Utiaji saini wa Katiba au Chata ya UN tarehe 26 mwezi Juni mwaka 1945  kwenye jengo la maveterani huko San Fransisco, Marekani.
UN Photo/Yould
Utiaji saini wa Katiba au Chata ya UN tarehe 26 mwezi Juni mwaka 1945 kwenye jengo la maveterani huko San Fransisco, Marekani.

Maadili yaliyoanzisha Umoja wa Mataifa hayana muda wa kumalizika

Masuala ya UM

Hii leo ni siku ya Umoja wa Mataifa ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema miaka 76 iliyopita, Umoja wa Mataifa uliundwa kama gari la kuleta matumaini kwa ulimwengu uliokuwa unaibuka kutoka kivuli cha mzozo mbaya wa Vita Kuu ya Pili ya dunia.

Katika ujumbe wake wa siku hii ya Umoja wa Mataifa inayoadhimishwa tarehe 24 ya mwezi Oktoba kila mwaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema janga la ugonjwa wa Corona au coronavirus">COVID-19, mizozo, njaa, umaskini na dharura ya mabadiliko ya tabianchi “vinatukumbusha kuwa bado kuna safari ndefu kwa dunia yetu kutokuwa na dosari. Ingawa vinaweka bayana kuwa mshikamano ndio jawabu pekee la kusonga mbele.”

Amesema ni kwa mantiki hiyo hii leo  wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, wake kwa waume wameendelea kubeba matumaini hayo ulimwenguni kote, na kutoa wito kwa watu wote kuja pamoja kutatua changamoto zinazoikabili dunia ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu SDGs.
 
Katibu Mkuu amesema hayo yanawezekana “kwa kuhakikisha kuwa kila mtu, kila mahali, anapata chanjo za COVID-19 mapema kuliko baadaye. Kwa kupata na kudumisha haki na utu wa watu wote, hasa masikini na wasiojiweza zaidi, wasichana na wanawake, watoto na vijana.

Sanamu ya "Ushindi Mzuri wa Uovu", iliyoko Makao Makuu ya UN huko New York, inayo onesha Mt.George wa mfano akimuua joka aliye na vichwa viwili - ishara ya vita vya nyuklia vilivyoshindwa na mikataba ya kihistoria kati ya Soviet Union na Marekani
UN/Ingrid Kasper
Sanamu ya "Ushindi Mzuri wa Uovu", iliyoko Makao Makuu ya UN huko New York, inayo onesha Mt.George wa mfano akimuua joka aliye na vichwa viwili - ishara ya vita vya nyuklia vilivyoshindwa na mikataba ya kihistoria kati ya Soviet Union na Marekani

Ameongeza maeneo mengine kuwa ni “Kwa kutafuta kumaliza migogoro inayoitia doa dunia yetu. kwa kutoa ahadi za kijasiri dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuzitekeleza ili kuokoa na kulinda sayari yetu. Na kwa kujenga utawala wa ulimwengu ambao ni jumuishi, unaowaleta watu pamoja na wenye ufanisi kama ilivyoelezwa kwenye ripoti yangu ya hivi karibuni ya Ajenda Yetu ya Pamoja.”

Katibu Mkuu huyo amesema amani, maendeleo, haki za binadamu na fursa kwa wote ni maadili yaliyowezesha mkataba wa Umoja wa Mataifa kudumu kwa miaka 76, na maadili hayo hayana tarehe ya kumalizika muda wake.
 
Amehitimisha ujumbe wake kwa kusema wakati dunia inaadhimisha siku ya Umoja wa Mataifa, “ ni vyema watu wote tuungane kwa kuzingatia maadili hayo na kuyaishi na kuwa na matumaini kwa Umoja wa Mataifa.”

Maadhimisho ya Umoja wa Mataifa hufanyika kukumbuka kuanzishwa kwa chombo hicho tarehe 24 mwezi Oktoba mwaka 1945 baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.