GAZA: Kikao Maalum cha Dharura cha UNGA kufanyika Alhamisi hii
GAZA: Kikao Maalum cha Dharura cha UNGA kufanyika Alhamisi hii
- Ni baada ya nchi wanachama ikiwemo Urusi kuwasilisha barua
- Rais wa UNGA amepokea barua 3
- Kikao kitakuwa mwendelezo wa kilichoahirishwa mwaka jana 2022
Baada ya rasimu mbili za maazimio kuhusu hali ya Mashariki ya Kati na hususan Suala la Palestina kugonga mwamba kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hivyo baraza hilo kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kusaka amani na usalama kwenye mapigano yanayoendelea Mashariki ya Kati, kati ya jeshi la Israeli na wanamgambo waliojihami wa kipalestina, Hamas, sasa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wameamua ‘kurusha karata’ nyingine kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kwa mujibu wa Chata ya UN yenye wanachama 193.
Nchi hizo wanachama zimechukua hatua kwa kuwasilisha jumla ya barua tatu kwa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Balozi Dennis Francis, zikimtaka aitishe Kikao Maalum cha Dharura, ESS, haraka iwezekanavyo kujadili hali Mashariki ya Kati.
Barua zimetoka wapi?
Barua ya hivi karibuni zaidi imepokelewa leo asubuhi na imetiwa saini na wawakilishi wa kudumu wa Bangladesh, Brunei-Darussalam, Cambodia, Indonesia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Lao, Malaysia, Maldives, Timor-Leste na Viet Nam.
Nimepokea pia barua kutoka Wawakilishi wa Kudumu wa Nicaragua, Urusi na Mkuu wa Utawala kwenye Ubalozi wa Syria wote wakitaka pia kikao cha dharura, amesema Balozi Francis kwenye barua aliyoandikia nchi wanachama wa UN na zile zenye hadhi ya uangalizi.
Halikadhalika tarehe 19 mwezi Oktoba mwaka 2023 Balozi Francis alipokea barua kutoka kwa Balozi Mahmoud Hmoud, Mwakilishi wa Kudumu wa Jordan kwenye Umoja wa Mataiufa, ambaye ni Mwenyekiti wa Kundi la nchi za kiarabu na kutoka kwa Balozi Sidi Mohamed Laghdaf, Mwakilishi wa Kudumu wa Mauritania ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Nchi za Kiislamu, (OIC) wakimtaka aitishe haraka iwezekanavyo Kikao Maalum Cha 10 cha Dharura cha Baraza hilo kilichoahirishwa mwaka jana.
Kikao Alhamisi Oktoba 26
Balozi Francis amesema kwa mujibu wa azimio namba ES-10/20 la tarehe 13 mwezi Juni mwaka 2018, ataitisha mjadala wa 39 wa kikao cha 10 cha dharura cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Alhamisi ya Oktoba 26 mwaka 2023 saa nne asubuhi kwenye ukumbi wa Baraza Kuu jijini New York, Marekani.
Kupitia barua yake kwa nchi wanachama, Balozi Francis amesema iwapo mjumbe yeyote anataka kuwasilisha hotuba, basi ajisajili mtandaoni kupitia ukurasa wa e-deleGATE.
Mchakato wa vikao maalum vya dharura UNGA
Kwa mujibu wa kanuni za Umoja wa Mataifa, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lina uwezo wa kuitisha kikao maalum cha dharura kwa ombi la nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, na ataitisha kikao hicho ndani ya siku 10 tangu mjumbe mmoja au zaidi atumie kura tufuru kuzuia azimio.
Tarehe 18 mwezi huu wa Oktoba, Marekani ilitumia turufu yake kuzuia rasimu ya azimio juu ya mzozo wa Israel na Palestina, hivyo Baraza lina hadi tarehe Mosi mwezi ujao wa Novemba kuitisha kikao hicho. Siku zinazohesabiwa ni siku za kazi.