Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waliopoteza maisha Gaza wamezidi 5,000 na hakuna dalili ya kusitisha uhasama:UN

Baadhi ya familia zilizotawanywa Kusini mwa Gaza zikijaribu kukabiliana na hali hali kadri ziwezavyo
© UNRWA
Baadhi ya familia zilizotawanywa Kusini mwa Gaza zikijaribu kukabiliana na hali hali kadri ziwezavyo

Waliopoteza maisha Gaza wamezidi 5,000 na hakuna dalili ya kusitisha uhasama:UN

Msaada wa Kibinadamu

Idadi ya watu waliouawa huko Gaza imefikia 5,087 kulingana na ripoti zilizotolewa leo na punde kutoka kwa mamlaka za huko, huku kukiwa na mashambulizi ya anga ya Israel kujibu mashambulizi ya Hamas, na wasaidizi wa kibinadamu wakirudia wito wa dharura wa kusitishwa kwa mapigano na misafara zaidi ya misaada kuingia katika Ukanda wa Gaza.

Akirejelea ujumbe huo, mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus ametoa wito mpya leo wa kupitisha kwa njia salama mahitaji muhimu ya matibabu na mafuta ili kuhakikisha vituo vya afya vinasalia wazi.

Akiandika kwenye ukurasa wake wa X Dkt. Tedros amesisitiza kuwa "Maisha ya watu yanategemea maamuzi haya." 

Ripoti za hivi punde za vyombo vya habari zinazonukuu wizara ya afya ya Gaza zinaonyesha kuwa idadi ya watu waliouawa Gaza tangu tarehe 7 Oktoba imeongezeka hadi  kufikia watu 5,087.

Miongoni mwa idadi hiyo wanawake na watoto wamefikia zaidi ya asilimia 62 ya vifo, huku zaidi ya watu 15,273 wamejeruhiwa.

Katika taarifa yake ya karibuni ya masuala ya kibinadamu kuhusu mzozo wa Gaza na Israel ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura , OCHA, imesema kuwa zaidi ya watu 1,000 wameripotiwa kupotea na wanakisiwa kuwa wamenasa au wamekufa chini ya vifusi".

Watu akipanga foleni katika duka la mikate Gaza
© UNICEF/Ayad El Eyad
Watu akipanga foleni katika duka la mikate Gaza

Israeli: Kuongezeka mara tatu kwa vifo

Kwa mujibu wa vyanzo rasmi vya Israel vilivyonukuliwa na OCHA, takriban watu 1,400 wameuawa nchini Israel, idadi kubwa zaidi ya watu katika mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba ambayo yalizua mzozo unaoendelea wa hivi karibuni.

OCHA imesema idadi ya vifo iliyoripotiwa ni "zaidi ya mara tatu ya idadi ya Waisraeli waliouawa tangu ilipoanza kurekodi majeruhi mwaka 2005.”

Takriban raia 212 wa Israel na raia wa kigeni wanashikiliwa mateka huko Gaza, mamlaka ya Israel imesema. 

Mateka wawili waliachiliwa Ijumaa iliyopita na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amerudia wito kwa Hamas kuwaachilia mateka wote mara moja na bila masharti.

Misaada zaidi imeingia Gaza

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari msafara mpya wa misaada uliingia Gaza kutoka Misri mapema leo Jumatatu kupitia kivuko cha mpaka cha Rafah. 

Hili limekuwa ni tukio la tatu la uingizaji huo wa misaada baada ya kivuko hicho kufunguliwa Jumamosi kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mzozo huo, kufuatia juhudi kubwa za kidiplomasia.

Jumla ya malori 34 ya msaada uliotolewa na Umoja wa Mataifa na Shirika la Hilali Nyekundu la Misri yaliingia katika eneo hilo mwishoni mwa juma. 

Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa ili kukabiliana na mahitaji ya kibinadamu yanayoongezeka, angalau lori 100 za misaada kwa siku zinahitajika.

Malori yaliyosheheni msaada wa kibinadamu yakijiandaa kuingia Gaza kupitia kivuko cha Rafah
© UNICEF/Eyad El Baba
Malori yaliyosheheni msaada wa kibinadamu yakijiandaa kuingia Gaza kupitia kivuko cha Rafah

Uhitaji mkubwa wa mafuta

Haya yanajiri huku shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) likionya siku ya Jumapili kwamba linatazamiwa kukosa mafuta ndani ya siku tatu, na hivyo kuweka hatua za msaada wa kibinadamu huko Gaza katika hatari.

Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini amesema kuwa bila mafuta, "hakutakuwa na maji, hakutakuwa na hospitali zinazofanya kazi na mikate na kwamba kukosekana kwa mafuta kutawaongezea zahma zaidi watoto, wanawake na watu wa Gaza".

Pengo la elimu

Wakati huo huo, OCHA imesema kuwa zaidi ya watoto 625,000 huko Gaza wamekosa elimu kwa angalau siku 12, na shule 206 zimeharibiwa. 

Ambapo takriban shule 29 kati hizo ni taasisi zinazoendeshwa na UNRWA.

Hadi kufikia leo UNRWA imeripoti kwamba wafanyakazi wake 35 wameuawa huko Gaza tangu Oktoba 7 a karibu nusu yao ni walimu.

Katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, ongezeko hilo pia limesababisha vikwazo katika upatikanaji wa elimu. 

OCHA imesema kuwa shule zote ndani ya eneo hilo zilifungwa kuanzia tarehe 7 hadi 9 Oktoba, na kuathiri takriban wanafunzi 782,000. 

Na kufikia wiki iliyopita, zaidi ya shule 230 zinazohudumia wanafunzi 50,000 hazikuwa zimefunguliwa tena.

Alia Zaki mkuu wa mawasiliano wa WFP Palestina
UN News
Alia Zaki mkuu wa mawasiliano wa WFP Palestina

Mahitaji ni makubwa kulliko msaada

Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP, huko Palestina, Alia Zaki, amesema misaada ya kibinadamu ambayo imeingia Gaza hadi sasa ni asilimia ndogo sana ikilinganishwa na ukubwa wa mahitaji katika Ukanda huo. 

Pia ametaja changamoto zinazokabili kampuni za kuoka mikate zinazofanya kazi na mpango huo kwa kuzingatia uhaba wa mafuta.

Zaki akizungumza katika mahojiano na UN News amesisitiza kuwa “Bila mafuta, hospitali au mikate haziwezi kufanya kazi, na kwamba kuna makampuni 4 pekee ya kuoka mikate yanayofanya kazi katika sekta nzima, ambako mwanzoni mwa mzozo huu kulikuwa na makampuni 23 yaliyofanya kazi na WFP.

Zaki amesema shirika hilo “limepunguza mgao ambao kila mtu hupokea kwa siku , ili kuweza kufikia idadi kubwa zaidi ya watu.”

Hata hivyo Zaki amesema “tunakaribisha mwanzo wa kuingia kwa msaada katika Ukanda wa Gaza kupitia kivuko cha Rafah, ingawa kiasi ni kidogo sana. Siku ya Jumamosi, malori 20 yaliyokuwa yamebeba chakula, dawa na maji yalipita, kwa sababu kulikuwa na pengo kubwa katika upatikanaji wa maji na chakula huko Gaza katika kipindi cha hivi karibuni. Kulikuwa na msafara mwingine uliokuwa na malori 14, na kuna taarifa kwamba lori la tatu liliingia Ukanda huo leo.”

Ameongeza kuwa “lakini idadi hii ni ndogo sana ikilinganishwa na ukubwa wa mahitaji ndani ya Gaza. Tunazungumzia zaidi ya watu 1,400,000 ambao wamehama makazi yao, na kwa zaidi ya siku 16 wamekuwa hawana njia ya kupata chakula au dawa, kwani vifaa vilivyopo vimeisha. Kwa hivyo, kile ambacho kimeingia Gaza hadi sasa ni asilimia ndogo sana ya kile ambacho watu wanahitaji.”