Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhaba wa chakula unachangia migogoro Chad: UN

Leo nchini Chad kuna takriban wakimbizi 657,000 - asilimia 51 ni wanawake na wasichana.
OCHA/Naomi Frerotte
Leo nchini Chad kuna takriban wakimbizi 657,000 - asilimia 51 ni wanawake na wasichana.

Uhaba wa chakula unachangia migogoro Chad: UN

Msaada wa Kibinadamu

Mgogoro wa kibinadamu nchini Chad ambao umechangiwa na mchanganyiko wa sababu ikiwemo uhaba wa chakula na watu kulazimishwa kuhama makazi yao, dharura za kiafya na majanga ya mabadiliko ya tabianchi, umesababisha Umoja wa Mataifa kutoa ombi la msaada wa dharura hii leo, ili  kusaidia watu milioni 7 kati watu milioni 18 nchini humo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi leo Madeleine Alingue, Waziri wa ustawi wa kiuchumi na ushirikiano wa kimataifa wa Chad amesema “Chad ni nchi iliyo katika kanda ambayo iko na mazingira magumu na pia ambayo haina utulivu.”

Bi Alingue ameeleza kuwa Chad inawahifadhi wakimbizi kutoka nchi jirani migogoro inapozuka kama vile Niger, Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, na Sudan, ambapo imepokea zaidi ya wakimbizi 460,000 tangu April mwaka huu.

Kuongezeka kwa watu kutoka Sudan, pamoja na ufadhili usiotosha, kumeweka shinikizo kubwa katika huduma za misaada ambazo tayari ni dhaifu.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, leo hii, mtu mmoja kati ya kila watu 17 wanaoishi Chad ni mkimbizi.

Shirika hilo limeongeza kuwa Chad inakabiliwa na magonjwa ya mara kwa mara na milipuko ya magonjwa kama vile malaria, surua na homa ya uti wa mgongo, inayoathiri karibu watu milioni 1.7, nusu yao wakiwa wanawake na washichana ambao wanakabiliwa na matatizo ya kupata huduma za msingi za afya nchini kote Chad.

Mwaka jana raia nchini Chad walishuhudia msimu mbaya zaidi wa ukame katika muongo mmoja, ukiacha watu milioni 2.1 wakiwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Takwimu za Umoja wa Mataifa za mwaka wa 2023, baado zinaonysha kwamba takriban watu milioni 1.86 wanakabiliwa na tishio la uhaba mkubwa wa chakula.

Hali kadhalika Mratibu Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani (WFP) nchini Chad, Pierre Honnorat ameongeza kuwa hali nchini humo ni janga la kibadamu na anaomba Umoja wa Mataiafa ushikamane nao ili kusaidia wakimbizi na raia wa taifa hilo.