Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 19.7 wakabiliwa na njaa kali Afghanistan, msaada wahitajika haraka:WFP/FAO

Takribani asilimia 83 ya raia wa Afghanistan wenye umri wa zaidi ya miaka 18 hawana ajira. Kutokana na kukosekana kwa mapato ya kimsingi na kupanda kwa bei za vyakula, upatikanaji wa chakula umekuwa tatizo kubwa zaidi kwa watu waliokimbia makazi yao.
IOM 2021/Paula Bonstein
Takribani asilimia 83 ya raia wa Afghanistan wenye umri wa zaidi ya miaka 18 hawana ajira. Kutokana na kukosekana kwa mapato ya kimsingi na kupanda kwa bei za vyakula, upatikanaji wa chakula umekuwa tatizo kubwa zaidi kwa watu waliokimbia makazi yao.

Watu milioni 19.7 wakabiliwa na njaa kali Afghanistan, msaada wahitajika haraka:WFP/FAO

Msaada wa Kibinadamu

Watu milioni 19.7, karibu nusu ya idadi ya watu wote wa Afghanistan, wanakabiliwa na njaa kali kulingana na ripoti ya uchambuzi wa hivi karibuni wa tathimini ya hali ya uhakika wa chakula (IPC) iliyofanywa mwezi Januari na Februari 2022 na washirika wa masuala ya uhakika wa chakula na kilimo, ikiwa ni pamoja na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO, shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP na mashirika mengi yasiyo ya kiserikali au NGOs. 

 

Ripoti hiyo inatabiri kuwa mtazamo wa Juni hadi Novemba 2022 unaonesha kuboreka kidogo kwa hali ya uhakika wa chakula, na kupungua kwa idadi ya watu wanaokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula hadi kufikia watu milioni 18.9.  

Hii inatokana kwa kiasi fulani na mavuno ya ngano yanayofanyika kuanzia mwezi huu wa Mei hadi Agosti, na uratibu mzuri wa mwaka huu wa upanuzi wa wigo wa msaada wa kibinadamu wa chakula pamoja na kuongezeka kwa msaada wa maisha ya kilimo.  

Hata hivyo, faida itakuwa ndogo inaonya ripoti. Ukame unaoendelea na mzozo mkubwa wa kiuchumi unamaanisha kuwa njaa isiyo na kifani itaendelea kutishia maisha ya mamilioni ya watu kote Afghanistan. 

Kwa mara ya kwanza kuna hofu kubwa ya njaa Afghanistan 

 

Kwa mujibu wqa ripoti hiyo jambo la kutia wasi wasi ni kwamba kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa IPC nchini Afghanistan mwaka 2011 hali ya viwango vya janga na uhaba wa chakula au IPC daraja la 5 vimebainika nchini humo.  

Zaidi ya watu 20,000 katika mkoa wa kaskazinimashariki wa Ghor wanakabiliwa na viwango vya janga la njaa kwa sababu ya kipindi kirefu cha baridi kali na hali mbaya ya kilimo. 

"Viwango ambavyo havijawahi kushuhudiwa vya usaidizi wa kibinadamu vinavyolenga kuimarisha uhakika wa chakula vimeleta mabadiliko. Lakini hali ya uhakika wa chakula ni mbaya. Usaidizi wa kibinadamu unasalia kuwa muhimu sana, kama vile mahitaji ya kujenga upya maisha na kuimarisha kilimo kilichosambaratika na kuunganisha tena wakulima na jamii za vijijini kwenye soko la vijijini na mijini ambalo limeathirika nchini kote.Endapo haya yatatokea, hakutakuwa na njia ya kutoka katika mgogoro huu,” amesema Richard Trenchard, mwakilishi wa FAO nchini Afghanistan. 

Msaada ndio mkombozi pekee kwa sasa

 

Mary-Ellen McGroarty,mkurugenzi na mwakilishi wa WFP nchini Afghanistan kwa upande wake amesema “Msaada wa chakula na usaidizi wa dharura wa kujikimu ndio mkombozi wa sasa wa maisha kwa watu wa Afghanistan. Tumeanzisha oparesheni kubwa zaidi ya msaada wa chakula duniani katika muda wa miezi kadhaa, na na lengo ni kufikia zaidi ya watu milioni 16 tangu Agosti 2021.” 

Ameongeza kuwa “Tunafanya kazi na wakulima, wasagishaji wa chakula na viwanda vya kutengeneza mikate, pia tunatoa mafunzo kwa wanawake na kutengeneza nafasi za ajira ili kusaidia uchumi wa mashinani. Kwa sababu watu wa Afghanistan wangependelea zaidi kazi, wanawake wanataka kuwa na uwezo wa kufanya kazi, na wasichana wote wanastahili kwenda shule. Kuruhusu uchumi kufanya kazi kama kawaida ndiyo njia ya uhakika ya kuondokana na mzozo, vinginevyo mateso yataongezeka pale ambapo mazao hayawezi kupatikana.”

 

Ripoti inasema wanatumai kuwa msimu ujao wa maavuno utaleta ahueni kwa mamilioni ya familia zinazokabiliana na upotevu wa mapato na uhaba wa chakula.  

Hata hivyo, kwa wengi, mavuno yatatoa tu unafuu wa muda mfupi na fursa ndogo sana ya kujikwamua.

 

Vita nchini Ukraine vinaendelea kuweka shinikizo kwa usambazaji wa ngano nchini Afghanistan, bidhaa za chakula, pembejeo za kilimo, na bei ya mafuta. Na upatikanaji wa mbegu, mbolea na maji kwa ajili ya umwagiliaji ni mdogo, fursa za wafanyakazi ni chache na madeni makubwa yamepatikana kwa sababu ya kununua chakula katika miezi michache iliyopita.

 

UN kuelendea kuisaidia Afghanistan 

 

FAO na WFP wamesema wataendelea kuongeza programu zao za msaada kote nchini.  

WFP imefikia zaidi ya watu milioni 16 hadi sasa mwaka huu wa 2022 kwa msaada wa dharura wa chakula, na inasaidia masoko ya ndani, ikifanya kazi na wachuuzi wa reja reja na wasambazaji wa ndani.  

 

WFP pia inaendelea kuwekeza katika maisha ya watu kupitia mafunzo ya ujuzi na miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili familia ziweze kulima ardhi yao na kulima chakula chao wenyewe. 

 

FAO kwa upande wake inaendelea kuongeza msaada wake kwa wakulima na wafugaji katika maeneo ya vijijini na itasaidia zaidi ya watu milioni 9 mwaka huu wa 2022 kupitia afua mbalimbali zinazosaidia uzalishaji wa mazao, mifugo na mboga mboga, uhawilishaji fedha na ukarabati wa miundombinu na mifumo muhimu ya umwagiliaji. 

 

Kusaidia kilimo ni uingiliaji kati wa gharama nafuu na wa kimkakati ambao huleta athari chanya kubwa za muda mfupi kama usaidizi wa kuokoa maisha, wakati unafungua njia ya kujikwamua kwa muda mrefu na maendeleo endelevu.