Mtu mmoja kati ya 3 DRC anakabiliwa na njaa kali, wengi wategemea mzizi Taro 

6 Aprili 2021

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, hali ya ukosefu wa chakula inazidi kuwa mbaya ambapo mtu mmoja kati ya watu watatu anakabiliwa na njaa kali, yamesema hii leo mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la chakula na kilimo, FAO na lile la mpango wa chakula duniani, WFP.  

 

WFP na FAO wanasema idadi hiyo ya watu kukosa chakula ni kubwa kuwahi kutokea na ni saw ana watu milioni 27.3 nchini kote, na wamebaini baada ya uchambuzi wa kitakwimu, IPC. 

Mwakilishi wa WFP nchini DRC Peter Musoko amenukuliwa kupitia taarifa ya WFP na FAO iliyotolewa leo mjini Kinshasa, DRC na Roma, Italia, akisema, “Kwa mara ya kwanza kabisa tumeweza kuchambua idadi kubwa ya wananchi na hiyo imetusaidia kupata taswira kamili ya kiwango cha ukosefu wa chakula DRC.” 

Amesema DRC ina uwezo wa kulisha wananchi wake na kuuza chakula cha ziada nje ya nchi na hivyo haipaswi kuwa na watoto wanalala njaa na familia zikikosa mlo kwa siku nzima. 

Mashirika hayo yamesema mizozo imesalia kuwa sababu kuu ya njaa DRC ambapo eneo kubwa lililoathirika ni majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Tanganyika yaliyoko Mashariki mwa nchi Pamoja na eneo la Kasai ambalo hivi karibuni lilikumbwa na mzozo mkubwa zaidi. 

Sababu nyingine ni kutwama kwa uchumi wa DRC Pamoja na janga la Corona, au COVID-19 ambalo limekuwa na madhara kiuchumi na kijamii. 

Mwakilishi wa FAO DRC Ongone Obame ameesma mizozo ya mara kwa mara inatia hofu kubwa na kwamba “Utulivu wa kisiasa na kijamii ni muhimu ili kuimarisha upatikanaji wa chakula na kujenga mnepo miongoni mwa jamii zilizo hatarini zaidi.” 

Nyuma ya pazia la ukosefu wa chakula ni simulizi za wazazi ambao wameporwa ardhi au kulazimishwa kuhama kuokoa maisha huku wakishuhudia watoto wao wakiugua kwa sababu ya ukosefu wa chakula. 

Familia nyingine zimesimulia jinsi zilivyorejerea vijijini mwao na kukuta nyumba zao zimetiwa moto na mazao yameporwa huku wengine wakilazimika kuishi kwa kula Taro ambao ni mzizi wa mti upatikanao porini, au kisamvu kilichochemshwa kwa maji pekee. 

FAO na WFP wanatoa wito kwa hatua za dharura kusaidia janga linalokumba wananchi wa DRC ambapo FAO inalenga kuongeza fursa ya kaya kupata pembejeo na mbegu, mifugo na maeneo ya hifadhi ya chakula, ikilenga kufikia watu milioni 1.1 kwenye maeneo yaliyo na uhaba mkubwa wa chakula. 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter