Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maktaba ya Little Voice Deep Within inavyosaidia watoto katika maeneo duni Kenya

Moja ya vyumba katika maktaba binafsi ya Little Voice Deep Within  mtaani Kariobangi South, Kenya.
Thelma Mwadzaya
Moja ya vyumba katika maktaba binafsi ya Little Voice Deep Within mtaani Kariobangi South, Kenya.

Maktaba ya Little Voice Deep Within inavyosaidia watoto katika maeneo duni Kenya

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Siku ya walimu duniani huadhimishwa tarehe 5 Oktoba kila mwaka.Mada kuu kwa mwaka huu ni walimu tunaohitaji kwa elimu tunayoitaka. Kenya imepiga hatua kwenye sekta ya elimu kwa kuzindua mfumo unaojikita katika kukuza vipaji na uwezo wa mwanafunzi, CBC,ila uhaba wa walimu ni kikwazo cha utekelezaji. Baadhi ya walimu wa kujitegeme wamechukua hatua mikononi mwao na kuanzisha maktaba za binafsi ili kuwapa watoto nafasi ya kusoma nje ya mazingira ya shule.

Maktaba ya Little Voice Deep Within iko mtaani Kariobangi South jijini Nairobi katikati ya makaazi ya umma.Hii ndiyo taswira unayokumbana nayo unapowasili.Watoto wanacheza nje au kusoma vitabu wakiwa ndani.

Kila siku ina ratiba yake ima ni kusoma, sanaa au kujifunza kutumia kompyuta .

Eric Odhiambo ni mwalimu wa kujitegemea na muasisi wa maktaba binafsi ya Little Voice Deep Within na anaamini kuwa kila mtoto ana haki ya kupata elimu mujarab nje ya mazingira ya shule kwani,”Watoto wa mtaani hawana maktaba.Unakuta mtoto anafikiria tu kutazama vibonzo kwenye televisheni hakuna kingine cha kufanya.Hakuna kituo ambapo mtoto anaweza kupitisha muda au kusoma na kufanya kitu fulani.Niliona ni bora kuwaletea maktaba karibu ili mtoto akitaka kusoma au ambaye hajui kusoma anapata msaada.”

Kusoma vitabu ni njia mujarab ya kuepusha utundu

Maktaba hii ina vitabu vya lugha na mada tofauti mahsusi kwa watoto wa kila rika.Siku ya walimu duniani huadhimishwa tarehe 5 Oktoba kila mwaka na mada kuu mwaka huu ni walimu tunaowahitaji kwa elimu tunayoitaka.Kwa mujibu wa takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Sayansi na utamaduni,UNESCO, walimu milioni 44 bado wanahitajika ili kutimiza lengo la kusambaza elimu ya msingi na sekondari kwa wote ifikapo 2030.Walimu wana mchango muhimu kwenye maisha ya wanafunzi na ni sawa na walezi. Evelyne Wambui ni mzazi na binti yake Joy anapata mafunzo kwenye kituo cha Little Voice Deep Within , anakiri kwa mba mwanawe amebadilika na kwa sasa,”Mwanzo wa mwaka mwalimu aliwaandikia vile vitabu vinavyohitajika kununuliwa. Mimi kama mzazi niliweza kununua vitabu vinne....hivyo vyengine vilinunuliwa na viko huko Vinamsaidia. Akipewa kazi ya ziada ya nyumbani.Yeye ana vitabu vya msingi vya Kiswahili, Hesabu na Sayansi.Vingine anavipata huku.”

Tweet URL

Watoto hujifunza pia vitu vingine kama kufuma mitandio na vitambaa wanapokuja kwenye kituo hiki.Kadhalika wanapata ujuzi wa kuchora kulingana na uwezo na umri wao.Ili kuiongeza kasi ya kutimiza lengo la 4 la maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa,SDGs ya elimu bora,UNESCO inashirikiana na mataifa hasa ya eneo la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara na kusini mwa Asia ili kuimarisha sera zinazowahusu na kuunga mkono mifumo ya kutoa mafunzo kwa walimu.Susan Muthoni ni mwalimu wa hiari kwenye kituo hiki cha watoto na anawafunza kufuma vitambaa na mitandio kwa upande wake anaamini kuwa masomo ya kutengeza bidhaa kwa mikono yana umuhimu mkubwa katika maisha ya usoni lakini,”Kwanza ni kuwa na walimu wanaowaelewa watoto.Kwenye shule kama hizi za umma,unapata kuwa kama mtoto wako huwa wa kwanza ataendelea hivyo na kama huwa wa mwisho anaendelea kuvuta mkia. Kwahiyo upo umuhimu wa kuwa na njia maalum ya kuwasomesha hawa watoto...kuwe na walimu wa kuwasomesha masomo mengine.Ukiona mtoto haelewi masomo ya kuandika anaweza kupata ujuzi wa kazi za mikono.”

UNESCO,shirika la lazi la Umoja wa Mataifa ILO,shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF na Education International ndiyo mashirika yanayosimamia siku ya walimu duniani na dhamira ni kuzishajiisha serikali na mashirika ya kijamii kuipa fani ya ualimu sifa nzuri zaidi ili kuwavutia wengi kujiunga hasa vijana.UNESCO imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa haki ya elimu inakuwa mchango muhimu kwenye misingi ya haki za binadamu na kulinda amani.Hata hivyo,kwa mujibu wa UNESCO nadharia hii itatimia iwapo walimu wanaungwa mkono kuwafunza wanafunzi ipasavyo.Eunice Monare yeye ni mzazi mtaani Kariobangi South…. mwanawe Moses anashiriki kwenye kituo cha Little Voice Deep Within na anakiri kuwa masomo yake yameimarika shuleni na,”Walimu wananiambia ameimarika kabisa.Hata wanashangaa vile alivyokuwa anapenda kucheza huko lakini kwa sasa amebadilika kabisa.Hasumbui wala kuwa mkaidi.

Walimu wanakata tamaa mapema

Tathmini za UNESCO zimebaini kuwa walimu wanaacha kazi kwa kukosa motisha na mazingira duni ya kazi yanayowavunja moyo.Changamoto wanazokumbana nazo ni pamoja na kwamba idadi ya wanafunzi darasani kuwa ni kubwa ikilinganishwa na nyenzo zilizopo.Eric Odhiambo, mwalimu na muasisi wa kituo na maktaba binafsi ya Little Voice Deep Within anaamini kuwa mfumo wa elimu una mchango mkubwa katika mafunzo ya maisha pia,”Ningependa elimu ambayo inatolewa Kenya isijikite katika kupita mtihani na kuwa nambari moja pekee.Hapana.Wacha mtoto aelimishwe.Awe wa kwanza au wa mwisho haijalishi lakini awe tofauti.Ajifunze apate kitu na kuirutubisha nafsi yake.”

Kwenye ujumbe wake wa siku ya walimu duniani,hii leo mkurugenzi mkuu wa UNESCO ,Audrey Azoulay amesisitizia umuhimu wa walimu katika jamii na kutaka fani hiyo ithaminiwe..Bi Azoulay alibainisha kuwa taaluma ya walimu inakabiliana na kipindi kigumu.Baadhi ya maeneo hayana wanafunzi.Mengine,walimu wanaacha kazi kwa wingi katika miaka ya mwanzo ya kuwa kazini.Kwa hali zote mbili: jibu ni moja,lazima tuwathamini,tuwafunze vizuri na kuwaunga mkono zaidi walimu.

Tuzo ya mwalimu bora duniani

Yote hayo yakiendelea, kwa mara ya pili tangu 2019 Kenya imewasilisha jina la mwalimu atakayewania Tuzo ya mwalimu bora duniani.Millicent Cassianes ameteuliwa kuwa mmoja ya wagombea 50 kuwania tuzo ya dola milioni moja za Marekani ya mwalimu bora duniani inayofadhiliwa na wakfu wa Varkeys kwa ushirikiano na UNESCO.Mwalimu Millicent Cassianes anafundisha kwenye shule maalum ya watoto walio na ulemavu wa kusikia iliyoko Karunga .kaunti ya Migori.Jumla ya walimu kutokea mataifa 130 waliwasilisha maombi ya kuwania tuzo hiyo iliyotua Kenya kwa mara ya kwanza mwaka 2019 aliposhinda mwalimu Peter Tabichi.