Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bila marekebisho ya mazingira ya walimu, fani ya ualimu inatoweka

Mwalimu mkimbizi Hassanie Ahmad Hussein akifundisha kwenye darasa lililo nje kwenye kambi ya wakimbizi ya Kouchaguine-Moura mashariki mwa Chad
© UNHCR/Colin Delfosse
Mwalimu mkimbizi Hassanie Ahmad Hussein akifundisha kwenye darasa lililo nje kwenye kambi ya wakimbizi ya Kouchaguine-Moura mashariki mwa Chad

Bila marekebisho ya mazingira ya walimu, fani ya ualimu inatoweka

Utamaduni na Elimu

Hii leo ikiwa ni siku ya walimu duniani, viongozi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, kazi duniani ILO na la kuhudumia watoto UNICEF wametoa ujumbe wa pamoja wakianza kwa kunukuu msemo ya kwamba huwezi kufundisha leo kama ulivyofundisha jana ili kuandaa wanafunzi wa kesho.

Nukuu hiyo ni ya John Dewey na viongozi hao ni Audrey Azoulay, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Gilbert F. Houngbo, Mkurugenzi Mkuu ILO na Catherine Russell, Mkurugenzi Mtendaji UNICEF.

Wametoa nukuu hiyo wakitambua umuhimu wa marekebisho ya mfumo wa elimu ili yaweze kumuandaa mtoto kukabiliana na dunia ya sasa inayobadilika kila uchao.

Mkataba mpya wa kijamii kuhusu elimu

“Dunia imeazimia kurekebisha mfumo wa elimu na kushughulikia vikwazo vikuu vinavyozuia walimu kuwa viongozi wa marekebisho hayo,” umesema ujumbe wao wa pamoja wakisema kuwa ripoti ya hivi karibuni kutoka Kamisheni ya Kimataifa kuhusu mustakabali wa elimu inatoa wito kwa mkataba mpya wa kijamii na elimu, ambamo kwao walimu ndio kitovu cha marekebisho na tasni yao inathaminiwa na kufikiriwa upya.

Bila kazi ya walimu haiwezekani kutoa elimu jumuishi, yenye usawa na bora kwa kila mwanafunzi. Wao ni muhimu katika kujikwamua baada ya janga la COVID-19 na kuandaa wanafunzi wa zama zijazo.

Viongozi hao wamesema bila ya kurekebisha mazingira ya kazi wanamofanyia walimu, ahadi ya elimu ya kukabili mabadiliko ya dunia itasalia kuw ani ndoto isiyofikiwa.

Wamenukuu yale yaliyopitishwa katika mkutano wa hivi karibuni wa Marekebisho ya Mfumo wa Elimu wakisema hii inahitaji idadi sasa ya walimu wenye uwezo, wenye motisha, wenye sifa na watendaji kwenye sekta ya elimu walio na stadi zinazotakiwa.

Image
Patrick Abale, Mwalimu Mkuu msaidizi katika shule ya msingi ya Yangani huko Yumbe, kaskazini maw Uganda akifundisha watoto wakimbizi kutoka Sudan Kusini. (Picha:UNHCR/Isaac Kasamani)

Matarajio na kilichopo ni sawa na ‘kiza na nuru’

Wakuu hao wa mashirika ya UNICEF, ILO na UNESCO wamesema kinachoshuhudiwa sasa kwenye maeneo mengi duniani ni madarasa yaliyofurika, walimu ni wachache na kama hiyo haitoshi wanafanya kazi kupita kiasi, hawana motisha na hawasaidiwi.

“Ndio maana tunashuhudia idadi kubwa isiyo ya kawaida ya walimu wakiacha kazi hiyo sambambana kupungua kwa idadi ya watu wanaotaka kusomea ualimu. Iwapo masuala haya hayatashughulikiwa, hasara itokanayo na kupotea kwa fani ya ualimu itakuwa pigo kubwa katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs hususan namba 4.”

Walimu wawepo wa kutosha na walipwe ujira stahiki

Ni kwa mantiki hiyo wanataka kuwepo kwa walimu wa kutosha na wenye sifa hadi kwenye maeneo ya ndani zaidi vijijini.

Mazingira mazuri ya kazi yaende sambamba na  ujira bora, wamesema viongozi hao.

Makadirio ya hivi karibuni yanaonesha kuwa walimu milioni 2.4 zaidi wanahitajika kwa ajili ya shule za msingi na milioni 4.4 kwa shule za sekondari iwapo dunia inataka kufanikisha elimu ya msingi kwa wote ifikapo mwaka 2030.