Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya Walimu Duniani, UNESCO na wadau wahimiza serikali kuwapa kipaumbele walimu katika kurejesha elimu mahali pake  

Wanafunzi nchini Uganda wakijadili katika klabu yao ya Wasichana katika Elimu, suala la ukatili dhidi ya wanawake wakiwa na muongozaji wao.
© UNICEF/Jimmy Adriko
Wanafunzi nchini Uganda wakijadili katika klabu yao ya Wasichana katika Elimu, suala la ukatili dhidi ya wanawake wakiwa na muongozaji wao.

Siku ya Walimu Duniani, UNESCO na wadau wahimiza serikali kuwapa kipaumbele walimu katika kurejesha elimu mahali pake  

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO na wadau wake linasema ufufuaji wa elimu unaofanikiwa unategemea kuongezeka kwa uwekezaji katika ustawi, mafunzo, ukuzaji wa kitaalam na hali ya ufanyaji kazi ya waalimu milioni 71 ulimwenguni ili kurejea katika hali nzuri baada ya kupotea kwa muda wa masomo kutokana na Covid-19.

 

Huo ndio ujumbe muhimu wa Siku ya Walimu Duniani, siku inayoadhimishwa kila tarehe 5 mwezi Oktoba, mwaka huu ikiwa na kauli mbiu "Walimu katika kiini cha kupona kwa elimu." Siku hii inatoa wito kwa serikali na jamii ya kimataifa kuzingatia walimu na changamoto zinazoikabili taaluma ya walimu. 

Katika taarifa ya pamoja, wakuu wa mashirika waandaaji wa maadhimisho ya siku hii ya Walimu Duniani, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Augrey Azoulay, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataufa la kuhudumia watoto, UNICEF, Henrietha Fore, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la kimataifa la kazi ILO, Guy Ryder na Katibu Mkuu wa shirika la Education International Bwana David Edwards wamesema, “leo tunasherehekea kujitolea kwa kipekee na ujasiri wa walimu wote, uwezo wao wa kubadilika na ubunifu katika hali ngumu sana na isiyo na uhakika. Ndio wahusika wakuu wa juhudi za kufufua elimu ulimwenguni na ni muhimu katika kuharakisha maendeleo kuelekea elimu bora iliyo jumuishi na yenye usawa kwa kila mwanafunzi, katika kila hali.” 

Viongozi hao wameongeza wakisema, “sasa ni wakati wa kutambua jukumu la kipekee la walimu na kuwawezesha na mafunzo, ukuzaji wa taaluma, msaada na mazingira ya kazi wanayohitaji kupeleka vipaji au talanta zao. Ufufuaji wa elimu utafanikiwa ikiwa utafanywa kwa mkono na walimu, kuwapa sauti na nafasi ya kushiriki katika kufanya uamuzi.” 

Uvurugwaji elimu uliosababishwa na Covid-19 umeonesha jukumu muhimu la walimu katika kudumisha mwendelezo wa ujifunzaji. Walimu wamekuwa kiini cha kielimu, kuanzia katika kutumia teknolojia kwa ubunifu hadi kutoa msaada wa kijamii na kihisia kwa wanafunzi wao na kufikia wale walio katika hatari zaidi ya kurudi nyuma pia Covid-19 imeziweka wazi changamoto kubwa zinazoikabili taaluma ya ualimu, pamoja na ukosefu wa fursa za maendeleo ya kazi katika ufundishaji mtandaoni na ujifunzaji kwa njia ya masafa, kuongezeka kwa mzigo wa kazi unaohusishwa na madarasa ya zamu mbili.  

Kwa mujibu wa utafiti wa UNESCO, asilimia 71 ya nchi zimewapa kipaumbele walimu katika chanjo, lakini ni nchi 19 tu ndizo zilizowajumuisha walimu katika chanjo ya kwanza, wakati nchi 59 hazijawapa kipaumbele walimu katika mipango yao ya chanjo.