Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake na wasichana 35,000 DRC wakumbwa na ukatili wa kijinsia Januari hadi Juni mwaka huu

Msemaji wa UN Stéphane Dujarric akizungumza na waandishi wa habari jijini New York.
UN Photo/Evan Schneider (Maktaba)
Msemaji wa UN Stéphane Dujarric akizungumza na waandishi wa habari jijini New York.

Wanawake na wasichana 35,000 DRC wakumbwa na ukatili wa kijinsia Januari hadi Juni mwaka huu

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC matukio ya ukatili wa kijinsia hasa kwenye majimbo yaliyogubikwa na mapigano yamezidi hadi kutoa hofu Umoja wa Mataifa.

“Kuanzia mwezi Januari hadi Juni mwaka huu manusura 35,000 wa ukatili wa kijinsia wameripotiwa kupatiwa msaada na ofisi ya Umoja wa Mataifa baada ya kukumbwa na visa hivyo katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini,” amesema Stéphane Dujarric, msemaji wa Umoja wa Mataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani hii leo, Bwana Dujarric amesema vitendo hivyo vinaongezeka na kutia hofu kubwa kwa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA.

“Idadi inaweza kuwa kubwa zaidi,” amesema Bwana Dujarric kwa maelezo kuwa ni kiasi kidogo sana cha waathirika ambao wanasaka usaidizi au wanaripoti matukio hayo.

Idadi kubwa ya manusura hao wa ukatili wa kijinsia ni wanawake na wasichana na hivyo OCHA imetoa wito wa hatua za haraka kuimarisha ulinzi wa makundi hayo.

Licha ya uzito na ukubwa wa matukio ya ukatili wa kijinsia nchini DRC, bado miradi ya kusaidia na kulinda manusura imefadhiliwa kwa asilimia 18 pekee, hali inayokwamisha uwezo wa kutoa huduma stahiki kwa manusura.