Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili haukukoma, vivyo hivyo matumaini yangu, asema mwathirika wa ukatili Sudan: UNFPA

Semira baada ya siku ndefu akitoka kukata nyasi huko Nyala, nchini Sudan
@UNFPA/Sufian Abdulmouty 05 December 2022
Semira baada ya siku ndefu akitoka kukata nyasi huko Nyala, nchini Sudan

Ukatili haukukoma, vivyo hivyo matumaini yangu, asema mwathirika wa ukatili Sudan: UNFPA

Haki za binadamu

Siku 16 za uhamasishaji jamii kuhusu ukatili dhidi ya wanawake zikiendelea kote duniani leo tunakupeleka Sudan, kutana na Semira anaeishi kwenye kambi ya Otash nchini huko ambaye ameonja shubiri ya ukatili wa kijinsia. 

"Nilipopata kipigo nilikimbilia kwa wazazi wangu, lakini walinirudisha kwa mume wangu mnyanyasaji."  

Hivi ndivyo Semira, mwenye umri wa miaka 25 kutoka Sudan, anakumbuka kuhusu ndoa yake, ambayo ilianza alipokuwa mtoto mdogo kwani kwa mujibu wa shirika la umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani na masuala ya afya ya uzazi UNFPA, alikua mama akiwa na umri wa miaka 14. 

"Vurugu hazikukoma, niliizoea," Semira ameliambia shirika la UNFPA. 

Hali ilizidi kuwa mbaya mwaka 2020 wakati mapigano ya silaha yalipoenea hadi mji wake wa Mashariki wa Jebel Marra. 

Familia ilikimbilia kambi ya Otash ya wakimbizi wa ndani, ambapo wamekuwa wakiishi tangu wakati huo, na ambapo ugumu wa Semira umeongezeka mara mbili. 

Alikuwa na watoto watano wa kuwatunza, hata hivyo aliendelea kulala kwa shida,usingizi wa mang’amung’amu au akikesha kila mara kwa hofu ya kile ambacho mume wake angemfanyia asubuhi. 

UN
Wanafunzi wa shule ya ukunga huko El Fasher jimboni Darfur kaskazini nchini Sudan wakiandamana kupinga ukatili wa kijinsia
UN

Fursa ya kujikwamua 

Siku moja, rafiki wa Semira alimtembelea na kuona mguu wake umeungua. Semira aliangua kilio, akieleza kuwa mumewe, kwa hasira, alikuwa amemchoma mguu wake kwa mafuta ya kupikia. 

Rafiki alijua nini cha kufanya. Siku iliyofuata, alimpeleka Semira kwenye kituo cha wanawake kinachoungwa mkono na UNFPA kambini hapo.  

Mfanyakazi wa kijamii anayeitwa Aisha alitambua kuwa Semira alikuwa akiugua kiwewe na msongo wa mawazo na hivyo akampeleka kwenye kituo kingine kinachoungwa mkono na UNFPA, cha huduma ya msaada kwa wanawake kinachoitwa "kona ya siri" kilichopo katika hospitali ya Nyala. 

Hospitali ilitibu mguu wake, na mfanyakazi wa masuala ya visa vya ukatili wa kijinsia alianza kukutana na Semira mara kwa mara. 

Kuwawezesha wanawake 

Vituo vya msaada kwa wanawake ni maeneo salama ambapo wanawake na wasichana wanaweza kuunganishwa na kupata usaidizi wa kisaikolojia na kijamii, rufaa Kwenda kupata huduma bora zaidi na vile vile msaada wa vifaa vya heshima lkama vile vya usafi na hedhi.  

Vituo hivyo pia huwa na mikutano ya kukuza uelewa kuhusu masuala muhimu, kupanga shughuli za elimu na burudani, na kuwapa maelezo kwa waathirika na manusura wa ukatili wa kijinsia ya wapi wanaweza kwenda kupata msaada wa kisheria. 

Ili kuhakikisha kituo kinakidhi mahitaji maalum ya wanawake katika jamii, kinaendeshwa na kamati inayoundwa na wanajamii wenyewe, wanaoshiriki katika kuandaa na kupanga shughuli zinazofanyika. 

Mizozo na ukosefu wa utulivu vinaweza kuchochea viwango vya juu vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana
© UNICEF/STARS/Kristian Buus
Mizozo na ukosefu wa utulivu vinaweza kuchochea viwango vya juu vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana

Semira ni miongoni mwa manusura hao 

Hivi karibuni Semira akawa mwenyeji katika kituo hicho. "Hapa, wanawake na wasichana wanakunywa chai wanaposhiriki hadithi zao kwa uhuru. Nilihisi msukumo wa kutembelea mahali hapa mara kwa mara ili kupata usaidizi na ustawi wangu wa kisaikolojia," amesema. 

Akiwa na mfanyakazi kesi kesi yake na jumuiya inayomuunga mkono, Semira alianza kuzingatia chaguzi zake.  

Aliamua kutomwacha mume wake au kujihusisha na huduma za kisheria kwa sababu ya unyanyapaa na matatizo ambayo akina mama wasio na waume wanakumbana nayo.  

Badala yake, alitafuta njia za kuimarisha cheo chake ndani ya familia na jumuiya. 

Alianza kushiriki katika shughuli za mafunzo ya ufundi stadi kama vile kutengeneza sabuni na alifaulu.  

Leo hii anaendesha biashara ndogo ya kutengeneza na kuuza sabuni kambini, na anapata pesa za kutosha kuwatunza wazazi wake na wakwe zake.  

Sasa kwa kuwa amepata mapato, usaidizi wa jamii na kujiamini, mivutano nyumbani imepungua.  

Semira anaripoti kwamba mume wake sasa anamuheshimu zaidi na hana jeuri na hata husaidia katika biashara yake mara kwa mara. 

Amekuwa na ujuzi wa kutosha wa kuwafunza wanawake wengine kambini, na anawaelekeza wanawake wengine katika jamii hadi katika kituo alikopata msaada ili wao pia waweze kusaidiwa. 

Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wakitembelea makao ya wanawake  waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia.
UN Photo/Marie Frechon
Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wakitembelea makao ya wanawake waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia.

Ni mmoja miongoni mwa mamilioni 

Semira ni mmoja miongoni mwa takriban wanawake na wasichana milioni 2.7 nchini Sudan wanaohitaji ulinzi, kinga, na huduma za kukabiliana na unyanyasaji na ukatili wa kijinsia. 

Katika kukabiliana na hitaji hili kubwa, UNFPA imeanzisha vituo vitano vya wanawake kwa ufadhili wa msaada wa kibinadamu kutoka Muungano wa Ulaya EU.  

Vituo hivyo viko katika maeneo ya Gedaref, Darfur Kaskazini na Darfur Kusini, na vituo hivyo vinatoa huduma kwa zaidi ya wanawake na wasichana 26,000  walio katika mazingira magumu zaidi. 

"Kwa maelfu ya wanawake na wasichana nchini Sudan, matumaini ni kitu pekee walichobakiza. Tuko hapa kugeuza matumaini haya kuwa kweli ambapo wanaweza kustawi katika mazingira salama, kutimiza ndoto zao, na kufunua na kufikia uwezo wao," amesema Mohamed Lemine, mwakilishi wa UNFPA nchini Sudan. 

Jina Semira lililotumika si jina halisi bali ni katika kumlinda muathirika.