Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mateso na wahalifu kutowajibishwa vimeenea katika maeneo yenye migogoro ya DRC - Ripoti ya UN

Mtoto ambaye aliwahi kutumikisha vitani huko Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC
Finbarr O’Reilly
Mtoto ambaye aliwahi kutumikisha vitani huko Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC

Mateso na wahalifu kutowajibishwa vimeenea katika maeneo yenye migogoro ya DRC - Ripoti ya UN

Haki za binadamu

Idadi kubwa ya matukio ya utesaji katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) vinatokea katika maeneo yaliyoathiriwa na mizozo ambako hali ya kutoadhibiwa kwa wahalifu imeenea, imeeleza ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Jumatano ya leo mjini Geneva, Uswisi.

 

Ripoti hiyo, iliyotolewa na Ofisi ya Pamoja ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini DRC (UNJHRO) na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani DRC (MONUSCO), inahusu kipindi cha kati ya tarehe 1 Aprili 2019 na 30 Aprili 2022.  

Ripoti hiyo inawasilisha matokeo ya UNJHRO kwamba asilimia 93 ya kesi 3,618 zilizosajiliwa za utesaji, ukatili, unyama au udhalilishaji ulioathiri watu 4,946 zilirekodiwa katika maeneo yaliyoathiriwa na mapigano ya kivita. Kati ya hizi, kesi 492 zilikuwa za ukatili wa kijinsia, na kuathiri watu 761. 

Walinzi wa usalama wanahusika 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, askari wa vikosi vya ulinzi na usalama walihusika na matukio 1,293 huku matukio mengine 1,833 yakihusishwa na wanachama wa vikundi vilivyojihami kwa silaha, ambao wakati mwingine waliyafanya matukio hayo wao wenyewe lakini katika muktadha fulani waliwatesa watu kwa kushirikiana na askari wa usalama wa nchi. 

Aidha ripoti hiyo inaonesha kuwa watu waliteswa na kudhulumiwa walipokuwa wakitekeleza haki zao za kimsingi, kama vile uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani, au wakati wa kuwekwa kizuizini. 

Kulingana na ripoti hiyo, “vurugu zinazofanywa katika usimamizi wa haki, katika vizuizi vya demokrasia au katika maeneo ya kizuizini zinaonesha jinsi utesaji unavyoenea katika muktadha wa ukosefu wa kuadhibiwa kwa watekelezaji wa matendo hayo mabaya kwa sababu malalamiko machache dhidi ya watuhumiwa wa utesaji na wengine, unyanyasaji au adhabu ya kikatili, ya kinyama, au ya kudhalilisha huwasilishwa au kufaulu. Hii inachangia kutothaminiwa kwa tatizo na ukubwa wake”. 

Mazingira wezeshi ya mateso 

Licha ya ukubwa wa ukiukaji na unyanyasaji uliofanywa,  wakati wa kuripoti ni maafisa wawili tu wa jeshi, maafisa wa polisi wa kitaifa 12 na wanachama 75 wa makundi yaliyojihami kwa silaha walipatikana na hatia ya mateso hayo. 

Ripoti hiyo inaashiria kwamba kutowawajibisha watekelezaji wa matendo hayo mabaya kwa binadamu, hutengeneza mazingira wezeshi kwa mateso kuendelea na inaeleza watu kutokuwa na imani na maafisa wa kutekeleza sheria na mfumo wa haki. 

Bintou Keita 

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa MONUSCO Bintou Keita amesema, "MONUSCO inaendelea kuunga mkono serikali katika juhudi zake za kuzuia na kupambana na mateso."  

Bintou Keita amesisitiza zaidi kwamba, "kamati za ufuatiliaji wa ukiukaji wa haki za binadamu unaotokana na jeshi la taifa na polisi, iliyoundwa na mamlaka ya kitaifa na kuungwa mkono na MONUSCO, zimeonekana kuwa muhimu katika kusaidia mafunzo katika eneo hili na kuhakikisha ufuatiliaji wa kesi za mateso.” 

OHCHR iko tayari kusaidia 

Kwa upande wake Kaimu Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Nada Al-Nashif amesema, "mateso hayawezi kamwe kuhalalishwa, bila kujali mazingira. Mamlaka za DRC lazima zichukue hatua kwa uharaka na azma ya kukomesha janga hili.”  

Kwa kutambua juhudi zinazofanywa na Serikali ya DRC, kama vile kupitishwa kwa Itifaki ya Ziada ya Mkataba dhidi ya Mateso na kuundwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia Mateso (CNPT), "mengi zaidi bado yanapaswa kufanywa ili kuzuia, kutokomeza kabisa na kuhukumu utesaji nchini nchini DRC.” Amesisitiza Nada Al-Nashif. 

Al-Nashif ameongeza kuwa katika miaka ya hivi karibuni Serikali ya DRC imekuwa ikijihusisha na sehemu tofauti za mfumo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na Kamati ya Kupambana na Mateso na Mapitio ya Mara kwa Mara ya Baraza la Haki za Kibinadamu kwa lengo la kurekebisha sheria na mazoea yake ili kufuata sheria za kimataifa kuhusu kuzuia na kutokomeza mateso. 

Kaimu Kamishna Mkuu huyo wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa amehitimisha kwa kusema vyombo hivi vimeelezea mapendekezo maalum ya kukomesha mateso mara moja na kwa wote, lakini machache yametekelezwa. Kufanya hivyo ni muhimu ili kuzuia watu wengi zaidi kuwa waathiriwa wa mateso na ukatili na kwamba, “Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa iko tayari kusaidia DRC katika jitihada hii yenye changamoto lakini muhimu.”