Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Urusi: Mvutano waendelea duniani kati ya ‘wengi walioamka’, na wachache walio mashakani kupoteza uthabiti wao

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa 23 Septemba 2023 New York, Marekani.
UN /Cia Pak
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa 23 Septemba 2023 New York, Marekani.

Urusi: Mvutano waendelea duniani kati ya ‘wengi walioamka’, na wachache walio mashakani kupoteza uthabiti wao

Amani na Usalama

Urusi imesema mustakabali wa dunia unaumbwa hivi sasa na mapambano kati ya walio wengi duniani wanaounga mkono mgao wenye haki wa maslahi ya dunia na utofauti wenye ustaarabu ilhali upande mwingine ni wachache wanaotumia mbinu za ukoloni mamboleo kuendeleza utawala wao dhidi ya wengine, utawala ambao wanashuhudia ukiyoyoma mbele ya macho yao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov amesema hayo akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA78 hii leo jijini New York, Marekni.

Amesema jambo ambalo limekuwa ni la kipekee zaidi tangu kumalizika kwa vita baridi, ni mazoezi ya hivi karibuni ya pamoja kati ya Marekani na washirika wake wa Umoja wa kujihami wa nchi za magharibi, NATO barani Ulaya kwa lengo la kuandaa mazingira ya kutumia silaha za nyuklia dhidi ya Urusi.

Hao wachache wanachochea mizozo

“Lengo ni kuishinda Urusi kimkakati,” ameeleza Bwana Lavrov akidai kuwa Marekani na washirika wake wanaendelea kuchochea mizozo ambayo inagawa binadamu katika makundi yenye chuki na kukwamisha malengo yao ya msingi.

Amesisitiza kuwa wanafanya kila kitu ili waweza kuzuia kuanzishwa kwa mwelekeo wa dhati wa kimataifa, “wanajaribu kushinikiza dunia kuwa na mwelekeo kwa mujibu wa watakavyo wao na kwa mujibu wa kanuni walizotunga wao. Napenda kusihi wanasiasa wa nchi za magharibi wasome tena Chata ya Umoja wa Mataifa.”

Bwana Lavrov amegusia hali inayoendelea ya mapigano nchini Sudan na athari za kushindwa kwa nchi za magharibi kushinikiza sera zao za kidemokrasia akisema, “kumekuweko na hali ya kutisha nchini Sudan. Na si kitu kingine zaidi ya athari za kushindwa kwa majaribio ya nchi za magharibi kuingiza nchini humo mfumo wao wa kidemokrasia nchini humo. Tunaunga mkono mipango bora ya kuongeza kasi ya usimamizi au utatuzi wa wasudan wenyewe wa tatizo lao.”

Marekebisho ya Baraza la Usalama na taasisi za kimataifa

Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Urusi amegusia suala la marekebisho ya taasisi za kimataifa likiwemo shirika la fedha duniani, IMF na Benki ya Dunia.

“Ni wakati sasa kurekebisha miundo ya usimamizi duniani. Hakuna kuchelea tena ugawaji mpya wa uwiano wa upigaji kura IMF na Benki ya Dunia. Nchi za magharibi lazima zitambue uwezo halisi wa kiuchumi na kifedha ambao nchi za kusini zinao.”

Amegusia pia shirika la biashara duniani, WTO akisema nalo pia uwakilishi wake uangaliwe sambamba na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akisema “kuna umuhimu wa kupanua ujumbe wa Baraza la Usalama kwa kuongeza uwakilishi wa mataifa mengine duniani na kuwapatia ujumbe wa kudumu kutoka bara la Asia, Afrika na Amerika ya Kusini.

Soma hotuba nzima hapa kwa lugha ya kirusi.

Tazama video hapa yenye mkalimani.