Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuwajibike wote kudhibiti kuenea kwa nyuklia- Urusi

Sergey V. Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi akihutubia mjadala mkuu wa UNGA74 kwenye Baraza Kuu la UN 27 Septe 2019
UN Photo/Loey Felipe
Sergey V. Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi akihutubia mjadala mkuu wa UNGA74 kwenye Baraza Kuu la UN 27 Septe 2019

Tuwajibike wote kudhibiti kuenea kwa nyuklia- Urusi

Amani na Usalama

Urusi imezungumzia mtazamo wake kuhusu hali inayoendelea nchini Iran, mzozo nchini Syria, vibali vya kuingia Marekani kwa maafisa wake wa kibalozi na masuala mengine nyeti kwenye ajenda ya kimataifa.

 

Mtazamo huo wa Urusi ulitolewa na Waziri wake wa Mambo ya Nje Serrgey Lavrov wakati akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA74 jijini New York, Marekani.
Mathali kuhusu Iran, amezungumzia kitendo cha Marekani kujitoa kwenye makubaliano ya pamoja ya kufuatilia mpango wa nyuklia wa Iran, JCPOA uliopitishwa na Baraza la Usalama la Umoa jwa Mataifa kupitia azimio lake namba 2231.

“Naonya kuhusu mashambulizi dhidi ya sheria ya kimataifa. Marekani si tu imepinga wajibu wake kwa mujibu wa azimio hio, bali pia imeanza kutaka wengine wacheze mchezo wake na kuhujumu utekelezaji wa mpango huo,” amesema Lavrov.

Kuhusu harakati za kudhibiti silaha za nyuklia, Lavrov amesema, “tunatiwa wasiwasi na ukosefu wa muda mrefu wa jibu la pendekezo letu kwa wenzetu wa Marekani mwaka mmoja uliopita, la kutaka kupitishwa kwa taarifa ya pamoja ya viongozi wa ngazi ya juu wa Marekani na Urusi juu ya kutokukubali na kutokuwa halali suala la vita vya nyuklia ambayo kwa ainisho lolote haiwezi kuwa na mshindi.”

Ametoa wito kwa mataifa yote kuunga mkono mpango huo.

Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Urusi akatangaza mipango ya kuanzisha rasimu ya azimio la mkataba wa kuimarisha na kuendeleza mfumo wa udhibti wa silaha, kuenea kwa silaha na uendelezaji wa silaha.

Amesema, “tunamkaribisha kila mmoja kufanya mazungumzo ya kina. Kupitishwa kwa azimio hilo kutachangia kwa kiasi kikubwa uwekaji wa mazingira ya mkutano wa mwaka ujao wa mapitio ya  mkataba wa kudhibiti kuenea kwa nyuklia, NPT .”

Akizungumza na wanahabari baada ya kuhutubia Baraza Kuu, Lavrov aliulizwa kuhusu suala la vibali vya maafisa wake wa kibalozi kuingia Marekani ambapo amesema, “nilitoa maoni yangu kuhusu suala hilo jana kwenye vyombo vya  habari na pia nimezungumzia suala hilo katika mkutano wangu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo.Ningependa kusema tena kuwa sina shaka kuwa si yeye wala rais wa Marekani walitambua hilo, na hawakutoa agizo la maafisa hao kunyimwa viza au vibali vya kuingia Marekani. Na mfanyakazi mwenzangu alinithibitishia hilo.”

Alipoulizwa kuhusu mazungumzo kwa njia ya simu kati ya Rais wa Marekani na yule wa Ukraine, Bwana Lavrov amesema, “Ningependa kusema kwamba kuna wazo la njia ya kidiplomasia ya kwamba kuleta masuala yote hadharani, kuwa muwazi sana kwenye mawasiliano kuhusu utawala huu au ule, iwapo hawataonesha nyaraka fulani kwa baadhi  ya wadau wake, basi huu utawala utasalimishwa. Hii ni aina gani ya demokrasia?”

Kuhusu hali ya Syria, Bwana Lavrov amesema anadhani wanajaribu kuelewa vyema ni jinsi gani wanaweza kusaidia wasyria wakubaliane kuhusu nchi yao ili wadau wote wa nje bila kujali yeyote, wataheshimu mamlaka za Syria.